Yeremia 18

Yeremia 18

Mfinyanzi na udongo

1Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, kusema,

2Ondoka, ukashuke mpaka nyumba ya mfinyanzi, na huko nitakusikizisha maneno yangu.

3Basi nikashuka mpaka nyumba ya mfinyanzi, na tazama, alikuwa akifanya kazi yake kwa magurudumu.

4Na chombo kile, alichokuwa akikifinyanga, kilipoharibika mkononi mwake yule mfinyanzi, alikitengeneza tena kuwa chombo kingine, kama alivyoona vema yule mfinyanzi kukifanya.[#Rum 11:15]

5Ndipo neno la BWANA likanijia, kusema,

6Ee nyumba ya Israeli, je! Siwezi mimi kuwatendea ninyi vile vile kama mfinyanzi huyu alivyotenda? Asema BWANA. Angalieni, kama udongo ulivyo katika mkono wa mfinyanzi, ndivyo mlivyo ninyi katika mkono wangu, Ee nyumba ya Israeli.[#Isa 45:9; 64:8]

7Wakati wowote nitakapotoa habari za taifa, na habari za ufalme, kuung'oa, na kuuvunja, na kuuangamiza;[#Yer 1:10]

8ikiwa taifa lile nililolitaja litageuka, na kuacha maovu yake nitaghairi, nisitende mabaya yale niliyoazimia kuwatenda.[#Amu 10:15,16; 2 Nya 12:6,7; Isa 1:16-19; Eze 18:21; Lk 13:3-5; Yon 3:10]

9Na wakati wowote nitakapotoa habari za taifa, na habari za ufalme, kuujenga na kuupanda,

10ikiwa watatenda maovu mbele za macho yangu, wasiitii sauti yangu, basi nitaghairi, nisitende mema yale niliyoazimia kuwatendea.

11Haya! Basi, ukawaambie watu wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu, ukisema, BWANA asema hivi, Tazama, ninafinyanga mabaya juu yenu, na kuwaza mawazo juu yenu; rudini sasa, kila mmoja na aiache njia yake mbaya; zitengenezeni njia zenu, na matendo yenu.[#2 Fal 17:13; Isa 1:16-19]

Ujeuri wa uzinzi wa Israeli

12Lakini wao wasema, Hakuna tumaini lolote; maana sisi tutafuata mawazo yetu wenyewe, nasi tutatenda kila mmoja wetu kwa kuufuata ushupavu wa moyo wake mbaya.

13Basi, kwa ajili ya hayo, BWANA asema hivi, Ulizeni sasa katika mataifa, ni nani aliyesikia habari za mambo kama hayo; bikira wa Israeli ametenda tendo lichukizalo sana.[#Yer 2:10; 1 Kor 5:1]

14Je! Theluji ya Lebanoni itakoma katika jabali la kondeni? Au je! Maji ya baridi yashukayo toka mbali yatakauka?

15Maana watu wangu wamenisahau, wameufukizia ubatili uvumba; nao wamewakaza katika njia zao, katika mapito ya zamani, ili wapite katika njia za kando, katika njia isiyotengenezwa;[#Yer 2:13; 10:15; 6:16; Kum 32:21; Isa 53:6]

16ili kufanya nchi yao kuwa kitu cha kushangaza, na cha kuzomewa daima; kila mtu apitaye karibu nayo atashangaa, na kutikisa kichwa chake.[#Yer 49:13; Kum 29:24; 1 Fal 9:8; Omb 2:15; Mik 6:16]

17Nami nitawatawanya mbele ya adui, kama kwa upepo wa mashariki; nami nitaviangalia visogo vyao, wala si nyuso zao, siku ya msiba wao.[#Yer 13:24; Zab 48:7]

Njama juu ya Yeremia

18Hapo ndipo waliposema, Njooni na tufanye mashauri juu ya Yeremia; maana sheria haitampotea kuhani, wala shauri halitampotea mwenye hekima, wala neno halitampotea nabii. Njooni, na tumpige kwa ndimi zetu, wala tusiyaangalie maneno yake yoyote.[#Yer 11:19; Mdo 7:51; 2 Tim 4:3; Law 10:11; Mal 2:7]

19Niangalie, Ee BWANA, ukasikilize sauti ya wanaoshindana nami.

20Je! Mabaya yalipwe badala ya mema? Maana wameichimbia nafsi yangu shimo. Kumbuka jinsi nilivyosimama mbele zako, ili niseme mema kwa ajili yao, nikaigeuze ghadhabu yako isiwapate.[#Zab 109:4; 35:7]

21Kwa sababu hiyo, uwatoe watoto wao waone njaa, uwatoe nguvu za upanga ziwapate; wake zao wafiwe na watoto wao, na kufiwa na waume zao; wanaume wao wauawe, na vijana wao wapigwe kwa upanga vitani.

22Kilio na kisikiwe kitokacho katika nyumba zao, hapo utakapoleta kikosi juu yao kwa ghafla; kwa maana wamenichimbia shimo waninase, nao wameifichia miguu yangu mitego.

23Lakini wewe, BWANA, unajua mashauri yao yote juu yangu, ya kuniua; usiwasamehe uovu wao, wala usifute dhambi yao mbele za macho yako; bali wakwazwe mbele zako; uwatende mambo wakati wa hasira yako.[#Neh 4:5]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya