The chat will start when you send the first message.
1BWANA akasema hivi, Nenda ukanunue gudulia la mfinyanzi, ukachukue pamoja nawe baadhi ya wazee wa watu, na baadhi ya wazee wa makuhani;[#Eze 8:11]
2ukatoke uende mpaka bonde la mwana wa Hinomu lililo karibu na mahali pa kuingia kwa lango la vigae, ukahubiri huko maneno nitakayokuambia,[#Yos 15:8; 2 Nya 28:3; Mit 1:20; 2 Fal 23:10; Yer 7:30-32; 32:34-35]
3ukisema, Lisikieni neno la BWANA, enyi wafalme wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu; BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli asema hivi, Angalieni, nitaleta mabaya juu ya mahali hapa, ambayo mtu yeyote akisikia habari yake, masikio yake yatawasha.
4Kwa sababu wameniacha mimi, nao wamepafanya mahali hapa kuwa mahali pageni, nao hapa wamewafukizia uvumba miungu mingine wasiowajua, wala wao, wala baba zao, wala wafalme wa Yuda; nao wamepajaza mahali hapa damu ya wasio na hatia;[#Kum 28:20; Isa 65:11; Yer 17:13; 2 Fal 21:16]
5nao wamemjengea Baali mahali pake palipo juu, ili kuwachoma moto wana wao, wawe sadaka za kuteketezwa kwa Baali; tendo nisiloliamuru mimi, wala kulinena, wala halikuingia moyoni mwangu;[#Law 18:21]
6basi, angalieni, siku zinakuja, asema BWANA, ambazo katika siku hizo mahali hapa hapataitwa tena Tofethi, wala Bonde la mwana wa Hinomu, bali, Bonde la Machinjo.[#Yos 15:8]
7Nami nitalitangua shauri la Yuda na Yerusalemu mahali hapa; nami nitawaangusha kwa upanga mbele za adui zao, na kwa mkono wa watu watafutao roho zao; na mizoga yao nitawapa ndege wa angani na wanyama wakali wa nchi, iwe chakula chao.[#Law 26:17; Kum 28:25,26; Yer 9:21; 7:33; Zab 79:2; Ufu 19:18]
8Nami nitaufanya mji huu kuwa kitu cha kushangaza watu, na kuzomewa; kila mtu apitaye karibu nao atashangaa, na kuzomea kwa sababu ya mapigo yake.[#Law 26:22; 1 Fal 9:8; Yer 18:16; Omb 2:15,16; Sef 2:15]
9Nami nitawalazimisha kula nyama ya wana wao, na nyama ya binti zao, nao watakula kila mmoja nyama ya rafiki yake, wakati wa mazingira na dhiki, ambayo adui zao, na watu wale watafutao roho zao, watawatesa.[#Law 26:29; Kum 28:53; Isa 9:20; Omb 4:10]
10Ndipo hapo utalivunja gudulia lile, mbele ya macho ya watu wale waendao pamoja nawe,[#Yer 51:63]
11na kuwaambia, BWANA wa majeshi asema hivi, Hivyo ndivyo nitakavyowavunja watu hawa, na mji huu, kama mtu avunjavyo chombo cha mfinyanzi, kisichoweza kutengenezwa tena na kuwa kizima; nao watazika watu katika Tofethi hata pasibaki mahali pa kuzikia.[#Zab 2:9; Isa 30:14; Omb 4:2; Yer 7:32]
12Hivyo ndivyo nitakavyopatenda mahali hapa, asema BWANA, nao wakaao humo, hata kufanya mji huu kuwa kama Tofethi;
13na nyumba za Yerusalemu, na nyumba za wafalme wa Yuda, zilizotiwa unajisi, zitakuwa kama mahali pa Tofethi; naam, nyumba zote ambazo juu ya madari yake wamelifukizia uvumba jeshi lote la mbinguni, na kuwamiminia miungu mingine sadaka za kunywewa.[#2 Fal 23:10; Sef 1:5; Yer 32:29; 7:18]
14Kisha Yeremia akatoka huko Tofethi, huko ambako BWANA alimtuma atoe unabii; naye akasimama katika ua wa nyumba ya BWANA, akawaambia watu wote,[#2 Nya 20:5]
15BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, nitaleta juu ya mji huu, na juu ya vijiji vyake vyote, mabaya yote niliyoyanena juu yake; kwa sababu wamefanya shingo zao kuwa ngumu, wasiyasikie maneno yangu.[#2 Nya 36:16,17; Yer 7:26; Zek 7:11-14; Mdo 7:51,52]