The chat will start when you send the first message.
1BWANA akanionesha, na tazama, vikapu viwili vya tini, vimewekwa mbele ya hekalu la BWANA, baada ya Nebukadneza, mfalme wa Babeli, kumchukua mateka Yekonia, mwana wa Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, na wakuu wa Yuda, pamoja na mafundi na wafua chuma, kutoka Yerusalemu, kuwaleta Babeli.[#Amo 7:1; 2 Fal 24:12; 2 Nya 36:10; Yer 22:24]
2Kikapu kimoja kilikuwa na tini nzuri sana, kama tini zilizotangulia kuiva; na kikapu cha pili kilikuwa na tini mbovu sana zisizoweza kuliwa, kwa kuwa zilikuwa mbovu sana.
3Ndipo BWANA akaniambia, Unaona nini Yeremia? Nikasema, Naona tini; tini nzuri zilizo nzuri sana; na tini mbovu zilizo mbovu sana, zisizoweza kuliwa, kwa kuwa ni mbovu sana.
4Kisha neno la BWANA likanijia, kusema,
5BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kama zilivyo tini hizi nzuri, ndivyo nitakavyowaangalia mateka wa Yuda, niliowatoa katika mahali hapa, waende mpaka nchi ya Wakaldayo, wapate mema.[#Zek 13:9; Ebr 2:11]
6Kwa maana nitawaelekezea macho yangu, wapate mema, nami nitawaingiza katika nchi hii tena; nami nitawajenga, wala sitawabomoa; nitawapanda wala sitawang'oa.[#Eze 36:24; Yer 12:15; 23:3; 32:41; 33:7]
7Nami nitawapa moyo, wanijue ya kuwa mimi ni BWANA; nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao; kwa maana watanirudia kwa moyo wao wote.[#Kum 30:6; Isa 51:16; Eze 11:19; 14:11; Yer 7:23; 30:22; 29:13; Zek 8:8; Zab 119:2]
8Na habari za tini zile mbovu, zisizoweza kuliwa, kwa kuwa ni mbovu sana; hakika, asema, BWANA, ndivyo nitakavyomtoa Sedekia, mfalme wa Yuda, na wakuu wake, na mabaki ya Yerusalemu, waliosalia katika nchi hii, na hao wanaokaa katika nchi ya Misri.[#Yer 29:17; 43:1]
9Naam, nitawatoa watupwe huku na huko katika falme zote za dunia, wapate mabaya; wawe kitu cha kulaumiwa, na mithali, na dhihaka, na laana, katika mahali pote nitakapowafukuzia.[#Zab 44:13]
10Nami nitatuma upanga, na njaa, na tauni, kati yao, hata watakapopotelea mbali katika nchi niliyowapa, wao na baba zao.