Yeremia 25

Yeremia 25

Utekaji wa Babeli watabiriwa

1Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, katika habari za watu wote wa Yuda; katika mwaka wa nne wa Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda mwaka ule ndio mwaka wa kwanza wa Nebukadneza, mfalme wa Babeli;[#2 Fal 24:1; Dan 1:1; Yer 36:1; 46:2]

2ambalo Yeremia, nabii, aliwaambia watu wote wa Yuda, na wenyeji wote wa Yerusalemu, kusema,

3Tangu mwaka wa kumi na tatu wa kutawala kwake Yosia, mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda, hata siku hii ya leo, miaka hii ishirini na mitatu, neno la BWANA limenijia, nami nimesema nanyi, nikiamka mapema na kusema; lakini ninyi hamkusikiliza.[#Yer 1:2]

4Naye BWANA ametuma kwenu watumishi wake wote, hao manabii, akiamka mapema na kuwatuma, lakini ninyi hamkusikiliza, wala hamkutega masikio yenu, msikilize.[#2 Nya 36:15; Yer 7:13,25; 11:7; 26:5; 29:19]

5Akasema, Rudini sasa, kila mtu na aiache njia yake mbaya; uacheni uovu wa matendo yenu, mkae katika nchi ambayo BWANA aliwapa, ninyi na baba zenu, tangu zamani za kale na hata milele;[#2 Fal 17:13; Eze 18:30; Lk 13:3-5]

6wala msiwafuate miungu mingine, ili kuwatumikia na kuwasujudia, wala msinikasirishe kwa kazi ya mikono yenu; basi, mimi sitawadhuru ninyi kwa dhara lolote.

7Lakini ninyi hamkunisikiliza, asema BWANA; ili mnikasirishe kwa kazi ya mikono yenu, na kujidhuru nafsi zenu.[#Yer 1:19; 32:30]

8Basi BWANA wa majeshi asema hivi, Kwa kuwa hamkuyasikiliza maneno yangu,

9angalieni, nitatuma watu na kuzitwaa jamaa zote za upande wa kaskazini, asema BWANA, nami nitatuma ujumbe kwa Nebukadneza, mfalme wa Babeli, mtumishi wangu, nami nitawaleta juu ya nchi hii, na juu yao wakaao ndani yake, na juu ya mataifa haya yote yaliyoko pande zote; nami nitawaangamiza kabisa, na kuwafanya kitu cha kushangaza, na kitu cha kuzomewa, na ukiwa wa daima.[#Yer 1:15; 40:2; 18:16]

10Tena, nitawaondolea sauti ya kicheko, na sauti ya furaha, sauti ya bwana arusi, na sauti ya bibi arusi, sauti ya mawe ya kusagia, na nuru ya mishumaa.[#Yer 7:34; 16:9; Ufu 18:22-23]

11Na nchi hii yote pia itakuwa ukiwa, na kitu cha kushangaza; nayo mataifa haya yatamtumikia mfalme wa Babeli miaka sabini.[#2 Nya 36:21; Yer 29:10; Dan 9:2]

12Na itakuwa miaka hiyo sabini itakapotimia, nitamwadhibu mfalme wa Babeli, na taifa lile, asema BWANA, kwa sababu ya uovu wao, na nchi ya Wakaldayo pia; nami nitaifanya kuwa ukiwa wa milele.[#Yer 29:10; Dan 9:2; Isa 13:19]

13Nami nitaleta juu ya nchi ile maneno yangu yote niliyoyanena juu yake, naam, yote yaliyoandikwa ndani ya kitabu hiki, aliyotabiri Yeremia juu ya mataifa haya yote.

14Kwa maana mataifa mengi na wafalme wakuu watawatumikisha; naam, hao pia; nami nitawalipa kwa kadiri ya matendo yao, na kwa kadiri ya kazi ya mikono yao.[#Yer 50:41; 27:7; 50:29; 51:6,24]

Kikombe cha ghadhabu ya Bwana

15Maana BWANA, Mungu wa Israeli, aniambia hivi, Pokea kikombe cha divai ya ghadhabu hii mkononi mwangu, ukawanyweshe mataifa yote, ambao nitakupeleka kwao;[#Ayu 21:20; Zab 11:6; 75:8; Isa 51:17,22; Ufu 14:10]

16nao watakunywa, na kupepesuka, na kufanya wazimu, kwa sababu ya upanga nitakaoutuma kati yao.[#Nah 3:11]

17Ndipo nikakipokea kikombe kile mkononi mwa BWANA, nikawanywesha mataifa yote, ambao BWANA alinituma kwao;

18yaani, Yerusalemu, na miji ya Yuda, na wafalme wake, na wakuu wake, ili kuwafanya kuwa ukiwa, na ajabu, na mazomeo, na laana; vile vile kama ilivyo leo;[#Zab 60:3; Eze 9:8; Dan 9:12; Amo 2:5]

19Farao, mfalme wa Misri, na watumishi wake na wakuu wake na watu wake wote;[#Yer 46:2]

20na watu wote waliochanganyika pamoja, na wafalme wote wa nchi ya Uzi, na wafalme wote wa nchi ya Wafilisti, na Ashkeloni, na Gaza, na Ekroni, na mabaki ya Ashdodi;[#Ayu 1:1; Isa 20:1]

21Edomu, na Moabu, na wana wa Amoni;

22na wafalme wote wa Tiro, na wafalme wote wa Sidoni, na wafalme wote wa kisiwa kilicho ng'ambo ya pili ya bahari;

23Dedani, na Tema, na Buzi, na watu wote wakatao denge;

24na wafalme wote wa Arabuni, na wafalme wote wa watu waliochanganyika wakaao jangwani;[#2 Nya 9:14; Yer 50:37]

25na wafalme wote wa Zimri, na wafalme wote wa Elamu, na wafalme wote wa Wamedi;

26na wafalme wote wa kaskazini, walio mbali na walio karibu, wote pamoja; na falme zote za dunia, zilizoko katika dunia; na mfalme wa Sheshaki atakunywa baada yao.[#Yer 51:41; #25:26 yaani Babeli, kwa fumbo.]

27Nawe utawaambia hivi, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nyweni, na kulewa, na kutapika, na kuanguka msiinuke tena, kwa sababu ya upanga nitakaoutuma kati yenu.[#Hab 2:16]

28Tena itakuwa, kama wakikataa kukipokea kikombe kile mkononi mwako, wanywe, ndipo utakapowaambia, BWANA wa majeshi asema hivi, Lazima mtakunywa.

29Maana angalieni, ninaanza kutenda mabaya katika mji uitwao kwa jina langu, je! Mtaachiliwa ninyi msiadhibiwe? Hamtaachiliwa msiadhibiwe; kwa maana nitauita upanga ule uwapige wote wakaao katika dunia, asema BWANA wa majeshi.[#Mit 11:31; Yer 49:12; Oba 1:16; Lk 23:31; 1 Pet 4:17; Eze 38:21]

30Basi, tabiri wewe maneno haya yote juu yao, na kuwaambia,[#Isa 42:13; Yoe 3:16; Amo 1:2; Zab 68:16]

BWANA atanguruma toka juu,

Naye atatoa sauti yake toka patakatifu pake;

Atanguruma sana juu ya zizi lake;

Atapiga kelele kama mtu akanyagaye zabibu,

Juu ya wenyeji wote wa dunia.

31Mshindo utafika hata mwisho wa dunia;[#Hos 4:1; Mik 6:2; Yoe 3:2]

Maana BWANA ana mashindano na mataifa,

Atateta na watu wote wenye mwili;

Na waovu atawatoa wauawe kwa upanga; asema BWANA.

32BWANA wa majeshi asema hivi, Tazama, uovu utatokea toka taifa hata taifa, na tufani kuu itainuliwa toka pande za mwisho wa dunia.

33Na waliouawa na BWANA siku ile watakuwapo, toka upande mmoja wa dunia hata upande wa pili; hawataliliwa, wala kukusanywa, wala kuzikwa; watakuwa samadi juu ya uso wa nchi.[#Isa 34:2-8; Yer 12:12; Ufu 19:17-21]

34Ombolezeni, enyi wachungaji, na kulia; na kugaagaa katika majivu, enyi mlio hodari katika kundi; maana siku za kuuawa kwenu zimetimia kabisa, nami nitawavunja vipande vipande, nanyi mtaanguka kama chombo cha anasa.

35Nao wachungaji watakuwa hawana njia ya kukimbia, wala walio hodari katika kundi hawataokoka.

36Sauti ya kilio cha wachungaji, na sauti ya kuomboleza kwao walio hodari katika kundi, kwa maana BWANA anayaharibu malisho yao.

37Na mazizi yenye amani yamenyamazishwa, kwa sababu ya hasira kali ya BWANA.[#Zab 97:1-3; Isa 66:15; Ebr 12:29]

38Ameacha mahali pake pa kujificha, kama simba; maana nchi yao imekuwa kitu cha kushangaza, kwa sababu ya ukali wa upanga uoneao, na kwa sababu ya hasira yake kali.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya