Yeremia 36

Yeremia 36

Gombo lasomwa katika hekalu

1Ikawa katika mwaka wa nne wa Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hili likamjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, kusema,

2Twaa gombo la kitabu, ukaandike ndani yake maneno yote niliyokuambia juu ya Israeli, na juu ya Yuda, na juu ya mataifa yote, tangu siku ile niliponena nawe, tangu siku za Yosia, hata siku hii ya leo.[#Isa 8:1; Hab 2:2; Yer 30:2; 25:3,15]

3Huenda nyumba ya Yuda watasikia mabaya yote niliyokusudia kuwatenda; wapate kurudi, kila mtu akaiache njia yake mbaya; nami nikawasamehe uovu wao na dhambi yao.[#Yer 18:8; Eze 12:3; Sef 2:3; Isa 55:7; Yon 3:8; Mdo 26:20]

4Kisha Yeremia akamwita Baruku, mwana wa Neria; naye Baruku akaandika katika gombo la kitabu maneno yote ya BWANA, yaliyotoka kinywani mwa Yeremia, ambayo BWANA alikuwa amemwambia.[#Yer 32:12; 45:1]

5Yeremia akamwagiza Baruku, ya kwamba, Mimi nimefungwa, siwezi kuingia katika nyumba ya BWANA.

6Basi, nenda wewe, ukasome katika gombo la kitabu, ambacho umeandika ndani yake, maneno ya BWANA yaliyotoka kinywani mwangu, ukiyasoma katika masikio ya watu, ndani ya nyumba ya BWANA, siku ya kufunga; pia utayasoma masikioni mwa watu wote wa Yuda, watokao katika miji yao.[#Law 16:29; 23:4; Neh 8:14,15]

7Labda wataomba dua zao mbele za BWANA, na kurudi, kila mtu akiiacha njia yake mbaya; kwa maana hasira na ghadhabu ni kuu sana, alizotamka BWANA juu ya watu hawa.[#Kum 28:15; 29:18]

8Basi, Baruku, mwana wa Neria, akafanya sawasawa na hayo yote, ambayo Yeremia, nabii, amemwagiza, akisoma katika kitabu hicho, maneno ya BWANA, ndani ya nyumba ya BWANA.

9Basi, ikawa katika mwaka wa tano wa Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, katika mwezi wa tisa, watu wote waliokuwa katika Yerusalemu, na watu wote waliokuja Yerusalemu kutoka miji yote ya Yuda, wakapiga mbiu ya kufunga mbele za BWANA.[#Amu 20:26; 1 Sam 7:6; 2 Nya 20:3]

10Basi, wakati huo Baruku akayasoma maneno ya Yeremia katika nyumba ya BWANA, katika chumba cha Gemaria, mwana wa Shafani, mwandishi, katika ua wa juu, mahali pa kuingilia kwa lango jipya la nyumba ya BWANA, akiyasoma katika masikio ya watu wote.

Gombo la kitabu lasomwa katika kasri

11Basi, Mikaya, mwana wa Gemaria, mwana wa Shafani, aliposikia maneno yote ya BWANA yaliyokuwa katika kitabu hicho,

12akashuka, akaingia katika nyumba ya mfalme, katika chumba cha mwandishi, na, tazama, wakuu wote wameketi humo, nao ni hawa, Elishama, mwandishi, na Delaya, mwana wa Shemaya, na Elnathani, mwana wa Akbori, na Gemaria, mwana wa Shafani, na Sedekia, mwana wa Hanania, na wakuu wote.

13Naye Mikaya akawaeleza maneno yote aliyoyasikia, hapo Baruku alipokuwa akikisoma kitabu masikioni mwa watu.

14Basi, wakuu wote wakamtuma Yehudi, mwana wa Nethania, mwana wa Shelemia, mwana wa Kushi, aende kwa Baruku, kumwambia, Litwae mkononi mwako gombo lile ulilolisoma masikioni mwa watu, uje huku. Basi, Baruku, mwana wa Neria, akalitwaa gombo lile mkononi mwake, akaenda kwao.[#Eze 2:6]

15Nao wakamwambia, Keti sasa, ukalisome masikioni mwetu. Basi, Baruku akalisoma masikioni mwao.

16Ikawa, walipoyasikia maneno hayo yote, wakatazamana kwa hofu, wakamwambia Baruku, Hatuna budi kumwambia mfalme maneno haya yote.[#1 Sam 3:11; Mdo 24:25]

17Wakamwuliza Baruku, wakisema, Tuambie sasa; ulipataje kuyaandika maneno haya yote kinywani mwake?

18Baruku akawajibu, Alinitamkia maneno haya yote kwa kinywa chake, nami nikayaandika kwa wino kitabuni.[#Isa 8:12; Yer 1:8; Mt 10:16-32; Rum 1:16; 1 Pet 3:14,15]

19Ndipo hao wakuu wakamwambia Baruku, Nenda ukajifiche, wewe na Yeremia, wala mtu asipajue mlipo.

Yehoyakimu achoma gombo la kitabu

20Wakaenda kwa mfalme ukumbini; lakini walikuwa wameliweka lile gombo katika chumba cha Elishama, mwandishi wakayanena maneno hayo yote masikioni mwa mfalme.

21Basi, mfalme akamtuma Yehudi aende akalilete lile gombo; naye akalitoa katika chumba cha Elishama, mwandishi. Yehudi akalisoma masikioni mwa mfalme, na masikioni mwa wakuu waliosimama mbele ya mfalme.

22Basi mfalme alikuwa ameketi katika nyumba iliyotumika wakati wa baridi, mwezi wa tisa; na pale palikuwa na moto wa makaa mbele yake.[#Amu 3:20; Amo 3:15]

23Hata ikawa, Yehudi alipokuwa amekwisha kusoma kurasa tatu nne, mfalme akalikata kwa kijembe, akalitupa katika moto wa makaa, hata gombo lote likawa limekwisha kuteketea katika huo moto wa makaa.[#1 Fal 22:8; Isa 29:21; 2 Tim 4:3]

24Lakini hawakuogopa, wala hawakurarua mavazi yao, wala mfalme, wala watumishi wake hata mmoja waliosikia maneno hayo yote.[#Mwa 37:29,34; 2 Sam 1:11; 2 Fal 22:11; Isa 36:22]

25Hata hivyo Elnathani, na Delaya, na Gemaria, walikuwa wamemsihi mfalme asiliteketeze gombo lile, lakini hakukubali kuwasikia.[#Mwa 37:26; Isa 53:12; Mt 27:24; Rum 8:34; Efe 5:7,11; Ebr 7:25]

26Mfalme akamwamuru Yerameeli, mwana wa mfalme, na Seraya, mwana wa Azrieli, na Shelemia, mwana wa Abdeeli, wamkamate Baruku, mwandishi, na Yeremia, nabii; lakini BWANA aliwaficha.[#1 Fal 19:14; Mt 23:34,37; Zab 34:19,20; 46:1; Yer 1:19; 2 Pet 2:9]

Yeremia atoa imla ya gombo lingine

27Ndipo neno la BWANA likamjia Yeremia, hapo mfalme alipokuwa amekwisha kuliteketeza gombo lile, na maneno yale aliyoyaandika Baruku, yaliyotoka katika kinywa cha Yeremia, kusema,[#Mit 21:30]

28Haya! Twaa wewe gombo lingine, ukaandike ndani yake maneno yote ya kwanza, yaliyokuwa katika gombo la kwanza, ambalo Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, ameliteketeza.

29Na kuhusu Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, utasema, BWANA asema hivi, Umeliteketeza gombo hili, ukisema, Mbona umeandika ndani yake, ukisema, Bila shaka mfalme wa Babeli atakuja, na kuiharibu nchi hii, na kukomesha mwanadamu na mnyama pia ndani yake?[#Amo 5:10]

30Basi, BWANA aseme hivi, kuhusu Yehoyakimu, mfalme wa Yuda; Hatakuwa na mtu wa kukaa katika kiti cha enzi cha Daudi; na maiti yake itatupwa nje wakati wa mchana ipigwe na joto, na wakati wa usiku ipigwe na baridi.[#2 Fal 24:8,12; Yer 22:19,30]

31Nami nitamwadhibu yeye, na wazao wake, na watumishi wake, kwa sababu ya uovu wao, nami nitaleta juu yao, na juu ya wenyeji wa Yerusalemu, na juu ya watu wa Yuda, mabaya yote niliyoyatamka juu yao, lakini hawakukubali kusikiliza.

32Ndipo Yeremia akatwaa gombo lingine, akampa Baruku, mwandishi, mwana wa Neria, naye akayaandika maneno yote yaliyotoka katika kinywa cha Yeremia, ya kitabu kile alichokiteketeza Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, katika moto; tena maneno mengi zaidi kama yale yakatiwa ndani yake.[#Kut 4:15; Rum 16:22]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya