Yeremia 41

Yeremia 41

Maasi juu ya Gedalia

1Basi ikawa katika mwezi wa saba, Ishmaeli, mwana wa Nethania, mwana wa Elishama, mmoja wa wazao wa kifalme, tena ni mmoja wa majemadari wa mfalme, na watu kumi pamoja naye, wakamwendea Gedalia, mwana wa Ahikamu, huko Mizpa; nao walikula chakula pamoja huko Mizpa.[#2 Fal 25:25; Yer 40:6,8; Zab 41:9; Lk 22:21]

2Akaondoka huyo Ishmaeli, mwana wa Nethania, na watu wale kumi waliokuwa pamoja naye, wakampiga Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, kwa upanga, wakamwua; yeye ambaye mfalme wa Babeli amemweka kuwa mtawala wa nchi.[#2 Sam 3:27]

3Tena Ishmaeli akawaua Wayahudi wote waliokuwa pamoja naye, yaani, pamoja na Gedalia, huko Mizpa, na hao Wakaldayo walioonekana huko, yaani, watu wa vita.[#Zab 52:1; Mit 1:16; Rum 3:15]

4Ikawa siku ya pili baada ya kumwua Gedalia, wala hapakuwa na mtu aliyejua habari hii,

5wakafika watu kadhaa toka Shekemu, na toka Shilo, na toka Samaria, watu themanini, nao wamenyoa ndevu zao, na kurarua nguo zao, nao wamejikatakata, wakichukua sadaka na ubani mikononi mwao, ili wazilete nyumbani kwa BWANA.[#Mwa 33:18; Yer 7:12-14; Yos 18:1; 24:32; Law 19:27,28; Kum 14:1; Isa 15:2; 2 Fal 25:9; 1 Sam 1:7; Yer 50:4]

6Na Ishmaeli, mwana wa Nethania, akatoka Mizpa kwenda kuwalaki, akilia alipokuwa akiendelea; ikawa alipokutana nao akawaambia, Njooni kwa Gedalia, mwana wa Ahikamu.

7Basi ikawa walipokuwa katikati ya mji, Ishmaeli, mwana wa Nethania, akawaua, akawatupa katika shimo, yeye na watu wale waliokuwa pamoja naye.

8Lakini watu kumi walionekana miongoni mwao, waliomwambia Ishmaeli, Usituue; kwa maana tuna akiba zetu zilizofichwa shambani, za ngano, na shayiri, na mafuta, na asali. Basi, akawaacha, asiwaue watu hao pamoja na ndugu zao.

9Basi, shimo lile, ambalo Ishmaeli amezitupa maiti za watu aliowaua, karibu na Gedalia, (ni lile lile alilolichimba Asa, mfalme, kwa kuwa alimwogopa Baasha, mfalme wa Israeli), Ishmaeli, mwana wa Nethania, akalijaza kwa watu wale aliowaua.[#Yos 10:16-18]

10Kisha Ishmaeli akawachukua mateka watu wote waliosalia, waliokuwa huko Mizpa, yaani, binti za mfalme, na watu wote waliobaki Mizpa, ambao Nebuzaradani, mkuu wa askari walinzi, alikuwa amemkabidhi Gedalia, mwana wa Ahikamu; Ishmaeli, mwana wa Nethania, akawachukua mateka. Akaondoka, ili awaendee wana wa Amoni.[#Yer 43:6; 40:7; Neh 2:10,19]

11Lakini Yohana, mwana wa Karea, na makamanda wote wa majeshi waliokuwa pamoja naye, waliposikia habari za hayo mabaya yote aliyoyatenda Ishmaeli, mwana wa Nethania,[#Yer 40:7,8,13]

12wakawatwaa watu wote, wakaenda ili kupigana na Ishmaeli, mwana wa Nethania, nao wakampata karibu na maji makuu ya Gibeoni.[#2 Sam 2:13]

13Basi, ikawa, watu wote waliokuwa pamoja na Ishmaeli, walipomwona Yohana, mwana wa Karea, na hao makamanda wote wa majeshi waliokuwa pamoja naye, ndipo wakafurahi.

14Basi, watu wote, ambao Ishmaeli amewachukua mateka kutoka Mizpa, wakazunguka, wakarudi, wakamwendea Yohana, mwana wa Karea.

15Lakini Ishmaeli, mwana wa Nethania, akatoroka pamoja na watu wanane, Yohana asimpate, akawaendea wana wa Amoni.[#1 Sam 30:17; 1 Fal 20:30]

16Ndipo Yohana, mwana wa Karea, na viongozi wote wa majeshi waliokuwa pamoja naye, wakawatwaa hao watu wote waliosalia, aliowapata tena katika mikono ya Ishmaeli, mwana wa Nethania, huko Mizpa, baada ya kumwua Gedalia, mwana wa Ahikamu, yaani, watu wa vita, na wanawake na watoto, na matowashi, aliowarudisha toka Gibeoni;

17wakaenda zao, wakakaa katika Geruthi Kimhamu, ulio karibu na Bethlehemu, ili wapate kuingia Misri,[#2 Sam 19:37,38]

18kwa sababu ya Wakaldayo; maana waliwaogopa, kwa sababu Ishmaeli, mwana wa Nethania, amemwua Gedalia, mwana wa Ahikamu, ambaye mfalme wa Babeli amemweka kuwa mtawala juu ya nchi.[#Yer 40:5]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya