The chat will start when you send the first message.
1Kuhusu wana wa Amoni. BWANA asema hivi, Je, Israeli hana wana? Je! Hana mrithi? Basi, mbona Malkamu anamiliki Gadi, na watu wake wanakaa katika miji yake?[#Eze 21:28-32; 25:1-7; Amo 1:13-15; Sef 2:8-11]
2Basi, kwa sababu hiyo, tazama, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapofanya kishindo cha vita kisikike juu ya Raba, mji wa Amoni, nao utakuwa magofu ya ukiwa, na binti zake watateketezwa kwa moto; ndipo Israeli watawamiliki wao waliokuwa wakimmiliki, asema BWANA.[#Amo 1:14]
3Omboleza, Ee Heshboni,[#Isa 32:11; Yer 48:7]
Kwa maana Ai umeangamizwa;
Lieni, enyi binti za Raba,
Mjivike nguo za magunia;
Ombolezeni, mkipiga mbio
Huko na huko kati ya maboma;
Maana Malkamu atakwenda kuhamishwa,
Makuhani wake na wakuu wake pamoja.
4Mbona unajisifu kwa sababu ya mabonde, bonde lako litiririkalo, Ee binti mwenye kuasi? Utumainiaye hazina zako, ukisema, Ni nani atakayenijia?[#Yer 21:13]
5Tazama, nitaleta hofu juu yako, asema Bwana, BWANA wa majeshi, itakayotoka kwa wote wakuzungukao; nanyi mtafukuzwa nje, kila mtu mbali kabisa, wala hapana mtu wa kuwakusanya wapoteao.
6Lakini baada ya hayo nitawarudisha wana wa Amoni walio utumwani, asema BWANA.[#Yer 48:47]
7Kuhusu Edomu. BWANA wa majeshi asema hivi, Je! Hakuna tena hekima katika Temani? Mashauri yamewapotea wenye busara? Je! Imetoweka hekima yao?[#Amo 1:11; Ayu 5:12-14; Oba 1:8; Isa 19:11]
8Kimbieni, rudini nyuma, kaeni chini sana, enyi mnaokaa Dedani; maana nitaleta msiba wa Esau juu yake, wakati nitakapomwangalia.[#Isa 2:19; Yer 25:23]
9Je! Kama wachuma zabibu wangekujia, wasingeacha zabibu ziokotwe? Kama wangekujia wezi usiku, wasingeharibu hata watakapopata vya kutosha?[#Isa 17:6]
10Lakini nimemwacha akiwa hana kitu Esau, nimepafunua mahali pake pa siri, wala hataweza kujificha; kizazi chake kimeangamizwa, na ndugu zake, na jirani zake, naye mwenyewe hayuko.[#Isa 17:14]
11Waache watoto wako wasio na baba, mimi nitawahifadhi hai, na wajane wako na wanitumaini mimi.
12Maana BWANA asema hivi, Tazama, wale wasioandaliwa kunywea kikombe, watakinywea, ni hakika; na wewe je! U mtu ambaye hataadhibiwa kabisa? Hukosi utaadhibiwa, naam, kunywa utakunywa.[#Yer 25:29; Oba 1:16]
13Kwa maana nimeapa kwa nafsi yangu, asema BWANA, kwamba Bozra utakuwa ajabu, na aibu, na ukiwa, na laana; na miji yake yote itakuwa ukiwa wa daima.[#Mwa 22:16; Isa 45:23; 34:6; Amo 6:8; 1:12]
14Nimepata habari kwa BWANA,[#Oba 1:1,2]
Na mjumbe ametumwa kati ya mataifa,
Akisema, Jikusanyeni, mkaujie,
Mkainuke kwenda vitani.
15Maana nimekufanya mdogo kati ya mataifa,
Na kudharauliwa katika watu.
16Kuhusu kuogofya kwako,[#Ayu 39:27; Mit 15:25; Amo 9:2]
Kiburi cha moyo wako kimekudanganya,
Wewe ukaaye katika pango za majabali,
Ushikaye kilele cha milima;
Ujapofanya kiota chako juu sana kama tai,
Nitakushusha kutoka huko; asema BWANA.
17Na Edomu atakuwa ajabu; kila mtu apitaye atashangaa, na kuzomea, kwa sababu ya mapigo yake yote.[#Yer 18:16; 50:13]
18Kama vile vilivyotokea wakati wa kuangushwa Sodoma na Gomora, na miji iliyokuwa karibu nayo, asema BWANA; hapana mtu atakayekaa huko, wala hapana mwanadamu atakayekaa huko kama mgeni akaavyo.[#Mwa 19:24-25; Kum 29:23; Yer 50:40; Amo 4:11]
19Angalia, atapanda kama simba toka kiburi cha Yordani juu ya malisho yasiyonyauka; lakini nitamkimbiza ghafla ayaache; na yeye aliye mteule nitamweka juu yake; maana ni nani aliye kama mimi? Tena ni nani atakayeniandikia muda? Tena ni mchungaji yupi atakayesimama mbele zangu?[#Yer 4:17; 12:5; Zek 11:3; Kut 15:11; Zab 89:6-8; Ayu 41:10]
20Basi, lisikieni shauri la BWANA;[#Yer 50:45]
Alilolifanya juu ya Edomu;
Na makusudi yake aliyoyakusudia
Juu yao wakaao Temani;
Hakika watawaburura, naam, wadogo wa kundi;
Hakika malisho yao yatafadhaika kwa ajili yao.
21Nchi yatetemeka kwa sauti ya kuanguka kwao;
Kuna kilio, sauti yake yasikiwa katika Bahari ya Shamu.
22Tazama, atapanda na kuruka kama tai, na kutandaza mabawa yake juu ya Bozra; na mioyo ya mashujaa wa Edomu siku hiyo itakuwa kama moyo wa mwanamke akiwa katika uchungu wa kujifungua.[#Yer 4:13]
23Kuhusu Dameski.[#Isa 17:1-3; Amo 1:3-5; Zek 9:1]
Hamathi umetahayarika, na Arpadi pia;
Maana wamesikia habari mbaya;
Wameyeyuka kabisa;
Wamesumbuka kama bahari, isiyoweza kutulia.
24Dameski umedhoofika;[#Isa 13:8]
Umejigeuza kukimbia; tetemeko limeushika;
Dhiki na huzuni zimeupata,
Kama za mwanamke katika uchungu wake.
25Imekuwaje mji wa sifa haukuachwa, mji wa furaha yangu?[#Yer 51:41]
26Kwa hiyo vijana wake wataanguka katika njia zake kuu, na watu wote wa vita watanyamazishwa katika siku hiyo, asema BWANA wa majeshi.
27Nami nitawasha moto katika ukuta wa Dameski, nao utayateketeza majumba ya Ben-hadadi.[#Amo 1:4; 2 Fal 13:3]
28Kuhusu Kedari, na falme za Hazori, ambazo Nebukadneza, mfalme wa Babeli, alizipiga. BWANA asema hivi, Ondokeni, pandeni hadi Kedari, mkawateke nyara wana wa mashariki.[#Ayu 1:3]
29Hema zao na makundi yao watayatwaa; watachukulia mbali mapazia yao kwa faida yao wenyewe, na vyombo vyao vyote, na ngamia wao; nao watawapigia kelele wakisema, Hofu ziko pande zote.[#Zab 120:5]
30Kimbieni ninyi, nendeni mbali mkitangatanga, kaeni chini sana, enyi mkaao Hazori, asema BWANA; maana Nebukadneza, mfalme wa Babeli, amefanya shauri juu yenu, naye amekusudia neno juu yenu.
31Ondokeni, pandeni hata taifa lililo katika hali ya raha, likaalo bila kuhangaika, asema BWANA; wasio na malango wala makomeo, wakaao peke yao.[#Hes 23:9; Kum 33:28; Amu 18:28; Mik 7:14]
32Na ngamia wao watakuwa mateka, na wingi wa makundi yao utakuwa nyara; nami nitawatawanya katika pande zote watu wale wanyoao denge; nami nitaleta msiba wao toka pande zao zote, asema BWANA.[#Kum 28:64; Eze 5:10; Yer 25:23]
33Na Hazori utakuwa kao la mbwamwitu; ukiwa milele; hakuna mtu atakayekaa huko, wala hakuna mwanadamu atakayekaa huko kama mgeni akaavyo.[#Yer 9:11; Mal 1:3]
34Neno la BWANA lililomjia Yeremia, nabii, juu ya Elamu, mwanzo wa kumiliki kwake Sedekia, mfalme wa Yuda, kusema,[#Mwa 10:22; Yer 25:25]
35BWANA wa majeshi asema hivi, Tazama nitauvunja upinde wa Elamu, ulio mkuu katika nguvu zao.[#Mwa 14:1; Ezr 4:9; Isa 21:2; Dan 8:2]
36Na juu ya Elamu nitazileta pepo nne, toka pembe nne za mbinguni, nami nitawatawanya katika pande zote nne, wala hakuna taifa ambalo hawatalifikia watu wa Elamu waliofukuzwa.
37Nami nitawafadhaisha watu wa Elamu mbele ya adui zao, na mbele ya hao wanaowatafuta roho zao; nami nitawaletea mabaya, naam, hasira yangu kali, asema BWANA; nami nitautuma upanga uwafuatie, hadi nitakapowaangamiza;[#Yer 48:2]
38nami nitaweka kiti changu cha enzi huko Elamu, nami nitawaharibu, mfalme na wakuu, watoke huko, asema BWANA.[#Yer 43:10; Dan 7:9]
39Lakini itakuwa, katika siku za mwisho, nitawarudisha wafungwa wa Elamu, asema BWANA.