Yeremia 6

Yeremia 6

Kukaribia kwa uvamizi na hofu yake

1Kimbieni mpate kuwa salama, enyi wana wa Benyamini; tokeni katika Yerusalemu, pigeni tarumbeta katika Tekoa, simamisheni ishara juu ya Beth-hakeremu; kwa maana mabaya yanachungulia toka kaskazini, na uharibifu mkuu.[#Yos 18:28; Amu 1:21; Neh 3:14]

2Binti Sayuni aliye mzuri, mwororo, nitamkatilia mbali.

3Wachungaji na makundi yao ya kondoo watamjia; watapiga hema zao karibu naye pande zote; watalisha kila mmoja mahali pake.[#2 Fal 25:1]

4Takaseni vita juu yake; inukeni, na tupande juu wakati wa adhuhuri. Ole wetu, kwa kuwa mchana umeanza kupungua, vivuli vya jioni vinazidi kuwa virefu.

5Inukeni, na tupande juu wakati wa usiku, tukayaharibu majumba yake.

6Maana BWANA wa majeshi asema hivi, Jikatieni miti, mjenge boma juu ya Yerusalemu. Mji huu ni mji unaojiwa; dhuluma tupu imo ndani yake.[#2 Fal 21:16]

7Kama vile kisima kitoavyo maji yake, ndivyo utoavyo uovu wake; jeuri na kuharibu kwasikiwa ndani yake; ugonjwa na jeraha zi mbele zangu daima.[#Zab 55:9-11; Yer 20:8; Eze 7:11; Mik 7:2,3]

8Uonyeke, Ee Yerusalemu, nafsi yangu, isije ikafarakana nawe; nisije nikakufanya ukiwa, nchi isiyokaliwa na watu.[#Eze 23:18; Hos 9:12]

9BWANA wa majeshi asema hivi, Wataokota mabaki ya Israeli kama mzabibu; rudisha mkono wako ndani ya vikapu, kama mchuma zabibu.

10Niseme na nani na kushuhudia, wapate kusikia? Tazama, sikio lao halikutahiriwa, wala hawawezi kusikiliza; tazama, neno la BWANA limekuwa matukano kwao; hawalifurahii.[#Kut 6:12; Mdo 7:51; Yer 7:26; 20:8; Lk 11:45; 2 Tim 4:3,4]

11Lakini nimejaa ghadhabu ya BWANA; nimechoka kwa kujizuia; imwageni juu ya watoto walio njiani, na juu ya kusanyiko la vijana pia; maana hata mume atatwaliwa pamoja na mkewe, mzee pamoja na yeye aliyetimiza siku zake.[#Yer 8:10; Sef 1:13]

12Na nyumba zao zitakuwa mali za watu wengine, mashamba yao na wake zao pamoja; kwa kuwa nitaunyosha mkono wangu juu ya wenyeji wa nchi hii, asema BWANA.[#Yer 8:10-12; Sef 1:13]

13Kwa maana, tangu aliye mdogo hata aliye mkubwa miongoni mwao, kila mmoja ni mtamanifu; na, tangu nabii hata kuhani, kila mmoja hutenda mambo ya udanganyifu.[#Isa 56:11; Mik 3:5]

14Wameliponya jeraha la watu wangu kwa juu juu tu, wakisema, Amani, Amani, wala hapana amani.[#Eze 13:10]

15Je! Walitahayarika, walipokuwa wameunda machukizo? La, hawakutahayarika hata kidogo, wala hawakuweza kuona haya usoni; basi, wataanguka miongoni mwa hao waangukao; wakati nitakapowajia wataangushwa chini, asema BWANA.[#Yer 3:3]

16BWANA asema hivi, Simameni katika njia kuu, mkaone, mkaulize habari za mapito ya zamani, Iko wapi njia iliyo njema? Mkaende katika njia hiyo, nanyi mtajipatia raha katika nafsi zenu. Lakini walisema, Hatutaki kwenda katika njia hiyo.[#Yer 18:15; Mal 4:4; Lk 16:29; Isa 28:12; Mt 11:29]

17Nami niliweka walinzi juu yenu, wakisema, Isikilizeni sauti ya tarumbeta; lakini walisema, Hatutaki kusikiliza.[#Isa 21:11; Yer 25:4; Hab 2:1]

18Kwa sababu hiyo sikilizeni, enyi mataifa, mkajue, Ee kusanyiko, ni jambo gani litokealo kati yao.

19Sikia, Ee nchi; tazama, nitaleta mabaya juu ya watu hawa, naam, matunda ya mawazo yao, kwa sababu hawakuyasikiliza maneno yangu; tena kwa habari ya sheria yangu, wameikataa.[#Mit 1:31]

20Yafaa nini niletewe ubani kutoka Sheba, na udi kutoka nchi iliyo mbali? Sadaka zenu za kuteketezwa hazikubaliwi, wala dhabihu zenu haziniridhii.[#Isa 66:3; 60:6; Mik 6:6]

21Basi, kwa hiyo, BWANA asema hivi, Tazama, nitaweka makwazo mbele ya watu hawa, na baba na wana wao watajikwaa pamoja; jirani ya mtu na rafiki yake watapotea.[#Ayu 5:12; Isa 8:14; Yer 13:16]

22BWANA asema hivi, Tazama, watu wanakuja, wakitoka katika nchi ya kaskazini; na taifa kubwa litaamshwa, litokalo katika pande za mwisho wa dunia.

23Washika upinde na mkuki; ni wakatili, hawana huruma; sauti yao huvuma kama bahari, nao wamepanda farasi wao; kila mmoja kama mtu wa vita amejipanga juu yako, Ee binti Sayuni.[#Isa 5:30]

24Tumesikia habari zake; mikono yetu inalegea; dhiki imetushika, na uchungu kama wa mwanamke wakati wa kuzaa kwake.[#Zab 48:6; Isa 21:3; Yer 4:31; 13:21; 30:6; 49:24]

25Msitoke kwenda mashambani, wala msitembee njiani, kwa maana upanga wa adui uko huko; hofu ziko pande zote.[#Amu 5:6]

26Ee binti wa watu wangu, ujivike nguo ya magunia, na kugaagaa katika majivu; fanya maombolezo, kama maombolezo kwa ajili ya mwana wa pekee, maombolezo ya uchungu mwingi; maana mwenye kuteka nyara atakuja juu yetu ghafla.[#Isa 32:11; Yer 4:8; Mik 1:10; Zek 12:10]

27Nimekuweka uwe mnara na ngome kati ya watu wangu; upate kuijua njia yao na kuijaribu.

28Ni waasi kupita kiasi wote pia, waendao huku na huko wakisingizia, ni shaba na chuma hao, hutenda dhuluma wote pia.[#Eze 22:18]

29Mifuo inafukuta kwa nguvu; risasi tu inatoka katika moto huo; mfua fedha ameyeyusha bure tu; maana wabaya hawaondolewi mbali.

30Watu watawaita taka za fedha, kwa sababu BWANA amewakataa.[#Hos 9:17; Zek 11:8]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya