Yoshua 14

Yoshua 14

Mgawanyo wa nchi ya magharibi mwa Yordani

1Kisha hizi ndizo nchi ambazo wana wa Israeli walizitwaa katika nchi ya Kanaani, ambazo Eleazari kuhani, na Yoshua mwana wa Nuni, na vichwa vya nyumba za mababa wa makabila ya Israeli, waliwagawanyia,[#Hes 34:17]

2kwa kufuata hiyo kura ya urithi wao, vile vile kama BWANA alivyoamuru kwa mkono wa Musa, kwa ajili ya hayo makabila tisa, na hiyo nusu ya kabila.[#Hes 26:52-56; 33:54; 34:13; Zab 16:5; Mit 16:33; 18:18]

3Kwa kuwa Musa alikuwa amekwisha kuwapa urithi hayo makabila mawili na nusu, ng'ambo ya pili ya Yordani; lakini hakuwapa Walawi urithi wowote kati yao.[#Hes 32:33; 34:14-15; Kum 3:12-17; Yos 13:8]

4Kwa kuwa wana wa Yusufu walikuwa makabila mawili, Manase na Efraimu; nao hawakuwapa Walawi sehemu katika hiyo nchi, isipokuwa waliwapa miji wapate kuikaa, pamoja na viunga vyake kwa ajili ya mifugo wao, na kwa ajili ya riziki zao.[#Mwa 48:5; 1 Nya 5:1,2]

5Vile vile kama BWANA alivyomwamuru Musa, hao wana wa Israeli walifanya hivyo, nao wakaigawanya hiyo nchi.[#Hes 35:2; Yos 21:2; Eze 45:1-8; 48:8,22]

Kalebu Agawiwa Hebroni

6Wakati huo wana wa Yuda walimwendea Yoshua hapo Gilgali; na Kalebu, mwana wa Yefune, huyo Mkenizi, akamwambia, Wewe wajua hilo neno BWANA alilomwambia Musa, huyo mtu wa Mungu, katika habari zangu, na katika habari zako wewe, tulipokuwa katika Kadesh-barnea.[#Hes 14:24,30; 32:8,12; 13:26; Yos 15:17; Kum 1:19,36]

7Mimi nilikuwa mtu wa miaka arubaini umri wangu, hapo Musa mtumishi wa BWANA aliponituma niende kutoka Kadesh-barnea ili kuipeleleza hiyo nchi; nami nilimletea habari tena, kama ilivyokuwa ndani ya moyo wangu.[#Hes 13:1-30]

8Lakini wale ndugu zangu waliokwea kwenda pamoja nami waliwavunja watu moyo; ila mimi nilimfuata BWANA, Mungu wangu, kwa utimilifu.[#Hes 14:24; Kum 1:36; Ufu 14:4]

9Kisha Musa akaniapia siku hiyo, akasema, Hakika hiyo nchi ambayo miguu yako imekanyaga itakuwa ni urithi kwako wewe, na kwa watoto wako milele, kwa sababu wewe umemfuata BWANA, Mungu wako, kwa utimilifu.[#Hes 14:24; 13:22; Yos 1:3]

10Sasa basi, angalia, yeye BWANA ameniweka hai, kama alivyosema, miaka hii arubaini na mitano, tangu wakati huo BWANA alipomwambia Musa neno hilo, wakati Israeli walipokuwa wanapitia jangwani; na sasa tazama, hivi leo nimetimiza umri wa miaka themanini na mitano.[#Hes 14:30; Kum 31:2; Zab 90:10]

11Hata sasa mimi nina nguvu zangu hivi leo kama nilivyokuwa siku hiyo Musa aliyonituma; kama nguvu zangu zilivyokuwa wakati huo, na nguvu zangu ndivyo zilivyo sasa, kwa vita na kwa kwenda na kurudi.[#Kum 34:7; 31:2]

12Basi sasa unipe mlima huu, ambao BWANA alinena habari zake siku hiyo; kwani wewe ulisikia siku hiyo jinsi Waanaki walivyokuwa huko, na miji ilivyokuwa mikubwa yenye boma; yumkini yeye BWANA atakuwa pamoja nami, nami nitawafukuza watoke nje, kama BWANA alivyonena.[#Hes 21:34; 1 Sam 14:6; 2 Nya 14:11,12; Zab 18:32; 44:3; Rum 8:31; Flp 4:13; Yos 15:14; Amu 1:10]

13Yoshua akambariki, akampa Kalebu, huyo mwana wa Yefune, Hebroni kuwa urithi wake.[#Amu 1:20; Mwa 47:7-10; Yos 22:6; 10:37; 21:11; 1 Nya 6:55]

14Kwa hiyo Hebroni ukawa urithi wa Kalebu, mwana wa Yefune, Mkenizi hata hivi leo, kwa sababu, alikuwa mwaminifu kwa BWANA, Mungu wa Israeli.

15Basi jina la Hebroni hapo kwanza uliitwa Kiriath-arba; huyo Arba alikuwa ni mtu mkubwa kupita wenziwe wote katika hao Waanaki. Hiyo nchi nayo ikatulia, vita vikakoma.[#Mwa 23:2; Yos 15:13; 11:23; #14:15 maana ya neno hili ni ‘mji wa Arba’.]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya