Yoshua 2

Yoshua 2

Wapelelezi watumwa Yeriko

1Yoshua, mwana wa Nuni, akawatuma watu wawili kutoka Shitimu kwa siri, ili kupeleleza, akawaambia, Nendeni mkaitazame nchi hii, hasa Yeriko. Wakaenda wakafika nyumbani kwa kahaba mmoja jina lake aliitwa Rahabu, wakalala huko.[#Ebr 11:31; Yak 2:25; Hes 25:1; Mt 1:5]

2Mfalme wa Yeriko akaambiwa, kusema, Tazama, watu wawili wa wana wa Israeli wameingia humu leo usiku, ili kuipeleleza nchi.[#Zab 127:1; Mit 21:30]

3Mfalme wa Yeriko akatuma watu kwa Rahabu, akasema, Watoe watu wale waliokuja kwako, walioingia ndani ya nyumba yako, maana wamekuja ili kuipeleleza nchi.

4Yule mwanamke akawatwaa wale watu wawili, akawaficha, akasema, Naam, wale watu walikuja kwangu, lakini sikujua walikotoka;[#2 Sam 17:19; 2 Fal 6:19]

5ikawa kama wakati wa kufungwa lango la mji, kulipokuwa giza, watu wale wakatoka, wala sijui walikokwenda; wafuateni upesi, maana mtawapata.

6Lakini yeye alikuwa amewapandisha darini, akawaficha kwa mabua ya kitani, aliyokuwa ameyatandika juu ya dari.[#Kut 1:17]

7Basi hao watu wakawafuata kwa njia iendayo Yordani mpaka vivukoni; na mara wale watu waliowafuatia walipokwisha kutoka, wakalifunga lango.

8Tena kabla hawajalala akawaendea juu darini,

9akawaambia wale wanaume, Mimi najua ya kuwa BWANA amewapa ninyi nchi hii, na ya kuwa hofu imetuangukia mbele yenu, na ya kuwa wenyeji wote wa nchi wanayeyuka mbele yenu.[#Mwa 35:5; Kut 15:15; 23:27; Kum 2:25; 11:25]

10Maana tumesikia jinsi BWANA alivyoyakausha maji ya Bahari ya Shamu mbele yenu, hapo mlipotoka Misri, tena mambo hayo mliyowatendea wafalme wawili wa Waamori waliokuwa huko ng'ambo ya Yordani, yaani, Sihoni na Ogu, mliowaangamiza kabisa.[#Kut 14:21; Hes 21:21-35; Yos 4:23]

11Na mara tuliposikia hayo mioyo yetu iliyeyuka, wala haukusalia ujasiri wowote katika mtu awaye yote, kwa sababu yenu; kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, yeye ndiye Mungu, katika mbingu juu na katika nchi chini.[#Kut 15:14,15; Yos 5:1; 7:5; Isa 13:7; Kum 4:30; 1 Fal 8:60; Zab 83:18; 105:21; Yer 16:19,21; Dan 4:34,35; Zek 8:20,23]

12Basi sasa, nawasihi, niapieni kwa BWANA, kwa kuwa nimewatendea hisani, ya kwamba ninyi nanyi mtaitendea hisani nyumba ya baba yangu; tena nipeni alama ya uaminifu;[#1 Sam 20:14-17; Efe 6:1,2; 1 Tim 5:8]

13ya kwamba mtawaponya hai baba yangu na mama yangu, na ndugu zangu wanaume na wanawake, na vitu vyote walivyo navyo, na kutuokoa roho zetu na kufa.

14Wale wanaume wakamwambia, Tutautoa uhai wetu badala ya uhai wenu, ikiwa hamwitangazi habari ya shughuli yetu hii; kisha itakuwa, wakati BWANA atakapotupa nchi hii, tutakutendea kwa hisani na uaminifu.[#Amu 1:24; Mt 5:7]

15Ndipo akawashusha kwa kamba dirishani, maana nyumba yake ilikuwa katika ukuta wa mji; naye alikaa ukutani.[#Mdo 9:25; Ebr 11:31]

16Akawaambia, Nendeni zenu mlimani, wale wanaowafuatia wasije wakawapata; mkajifiche huko siku tatu hadi wao wanaowafuatia watakaporudi; kisha nendeni zenu.

17Wale wanaume wakamwambia, Sisi tunataka tusiwe na hatia kwa ajili ya kiapo hiki ulichotuapisha.[#Kut 20:7]

18Angalia, tutakapoingia katika nchi hii, funga kamba hii nyekundu katika dirisha hili ulilotuteremshia; nawe uwakusanye kwako nyumbani mwako, baba yako, na mama yako, na ndugu zako, na watu wote wa nyumba ya baba yako.[#Mwa 7:1; 19:12,17; Est 8:6; Mdo 11:14; 2 Tim 1:16]

19Itakuwa mtu awaye yote atakayetoka katika mlango wa nyumba yako kwenda njiani, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe, na sisi tutakuwa hatuna hatia; na mtu atakayekuwa ndani ya nyumba yako damu yake itakuwa juu ya vichwa vyetu, mkono wa mtu ukimpata.[#Hes 35:26,27; Mt 27:25]

20Lakini wewe ukitangaza habari yetu hii, ndipo tutakuwa hatuna hatia, katika kiapo hiki ulichotuapisha.

21Naye akasema, Na iwe hivyo kama yalivyo maneno yenu. Akawatoa, nao wakaenda zao; naye akaifunga ile kamba nyekundu dirishani

22Watu hao wakaenda, wakafika mlimani, wakakaa huko siku tatu, hadi wale waliowafuatia walipokuwa wamerudi; na wale waliowafuatia wakawafuatia katika njia ile yote, lakini hawakuwaona.

23Kisha wale watu wakarudi, wakateremka mlimani, wakavuka, wakamwendea Yoshua, mwana wa Nuni, nao wakamwambia habari za mambo yote yaliyowapata.

24Wakamwambia Yoshua, Hakika BWANA ameitia nchi yote katika mikono yetu; tena zaidi ya hayo wenyeji wa nchi wanayeyuka mbele yetu.[#Kut 23:31; Yos 6:2; 21:44; Kut 23:27; Kum 2:25; 11:25]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya