Mambo ya Walawi 12

Mambo ya Walawi 12

Utakaso wa wanawake baada ya kujifungua

1Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,

2Nena na hao wana wa Israeli, uwaambie, Mwanamke akitunga mimba na kuzaa mtoto wa kiume, ndipo atakuwa najisi siku saba; kama katika siku za kutengwa kwake kwa ajili ya hedhi ndivyo atakavyokuwa najisi.[#Lk 2:22; Law 15:19]

3Siku ya nane mtoto atatahiriwa govi ya zunga lake.[#Mwa 17:12; Lk 1:59; 2:21; Yn 7:22,23]

4Na huyo mwanamke atakaa muda wa siku thelathini na tatu ili kutakata damu yake.

5Lakini kama amezaa mtoto wa kike naye atakaa muda wa siku sitini na sita ili kutakata damu yake.

6Kisha hizo siku za kutakaswa kwake zitakapotimia, kwa ajili ya mtoto wa kiume, au kwa ajili ya mtoto wa kike ataleta mwana-kondoo wa mwaka mmoja kuwa sadaka ya kuteketezwa na kinda la njiwa, au hua, kuwa sadaka ya dhambi, awalete mlangoni pa hema ya kukutania, na kumpa kuhani;[#Lk 2:22; Isa 53:7; Lk 24:26,27; Yn 1:29,36; 1 Pet 1:18,19; Ufu 5:6-8; 7:14]

7na yeye atawasongeza mbele za BWANA, na kufanya upatanisho kwa ajili yake; naye atatakasika. Hii ndiyo amri yake huyo azaaye, awe ni mtoto wa kiume au wa kike.[#Ebr 9:9-28; 10:1-12]

8Kama mali yake huyo mwanamke haimudu mwana-kondoo, hapo ndipo atakapochukua hua wawili, au makinda mawili ya njiwa; mmoja kuwa sadaka ya kuteketezwa, na wa pili kuwa sadaka ya dhambi; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atakuwa safi.[#Lk 2:24; Law 5:7; 2 Kor 8:9; Law 4:26]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya