Marko 11

Marko 11

Yesu aingia Yerusalemu kwa shangwe

1Walipokaribia Yerusalemu karibu na Bethfage na Bethania, kukabili mlima wa Mizeituni, aliwatuma wawili katika wanafunzi wake,[#Mt 21:1-9; Lk 19:29-38; Yn 12:12-16]

2akawaambia, Nendeni mpaka kile kijiji kinachowakabili; na katika kuingia ndani yake, mara mtaona mwanapunda amefungwa, asiyepandwa na mtu bado; mfungueni, kamleteni.

3Na mtu akiwaambia, Mbona mnafanya hivi? Semeni, Bwana anamhitaji na mara atamrudisha tena hapa.[#Mk 14:14]

4Wakaenda zao, wakamwona mwanapunda amefungwa penye mlango, nje katika njia kuu, wakamfungua.

5Baadhi ya watu waliosimama huko wakawaambia, Mnafanya nini kumfungua mwanapunda?

6Wakawaambia kama Yesu alivyowaagiza, nao wakawaruhusu.

7Wakamletea Yesu yule mwanapunda, wakatandika mavazi yao juu yake; akaketi juu yake.

8Watu wengi wakatandaza mavazi yao njiani, na wengine matawi waliyoyakata mashambani.

9Nao watu waliotangulia na wale waliofuata wakapaza sauti, Hosana; ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana;[#Zab 118:25-26]

10umebarikiwa na ufalme ujao, wa baba yetu Daudi. Hosana juu mbinguni.

11Naye akaingia Yerusalemu hata ndani ya hekalu; na alipokwisha kutazama yote pande zote, kwa kuwa ni wakati wa jioni, akatoka, akaenda Bethania pamoja na wale Kumi na Wawili.[#Mt 21:12-22; Lk 19:45-48]

Yesu aulaani mtini

12Siku iliyofuata walipokuwa wakitoka Bethania, aliona njaa.

13Akaona kwa mbali mtini wenye majani, akaenda ili labda aone kitu juu yake; na alipoufikia hakuona kitu ila majani; maana si wakati wa tini.[#Lk 3:9; 13:6-9]

14Akajibu, akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako. Wanafunzi wake wakasikia.[#Mk 11:20]

Yesu atakasa hekalu

15Wakafika Yerusalemu, naye akaingia ndani ya hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza na kununua ndani ya hekalu, akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao wauzao njiwa;[#Yn 2:14-16]

16wala hakumruhusu mtu yeyote kupitia katika hekalu akiwa amebeba kitu.

17Akafundisha, akasema, Je! Haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote? Bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi.[#Isa 56:7; Yer 7:11]

18Wakuu wa makuhani na waandishi wakapata habari wakatafuta jinsi ya kumwangamiza; maana walimwogopa, kwa sababu mkutano wote walishangazwa na mafundisho yake.

19Na kulipokuwa jioni alitoka mjini.[#11:19 Makala zingine zinaongeza ‘pamoja na wanafunzi wake’.]

Fundisho kutoka kwa mtini ulionyauka

20Na asubuhi walipokuwa wakipita, waliuona ule mtini umenyauka toka shinani.[#Mk 11:14]

21Petro akakumbuka habari yake, akamwambia, Rabi, tazama, mtini ulioulaani umenyauka.

22Yesu akajibu, akamwambia, Mwaminini Mungu.[#Yn 14:1]

23Amin, nawaambia, yeyote atakayeuambia mlima huu, Ng'oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake.[#Mt 17:20; 1 Kor 13:2; Lk 17:6]

24Kwa sababu hiyo nawaambia, Yoyote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.[#Mt 7:7; Yn 14:13; 16:23]

25Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. [[#Mt 5:23; 6:14-15]

26Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.]

Yesu aulizwa juu ya mamlaka yake

27Wakafika Yerusalemu tena; hata alipokuwa akitembea hekaluni, walimwendea wakuu wa makuhani, na waandishi, na wazee,[#Mt 21:23-27; Lk 20:1-8]

28wakamwambia, Ni kwa mamlaka gani unatenda mambo haya? Naye ni nani aliyekupa mamlaka hii uyatende haya?

29Yesu akawaambia, Nitawauliza neno moja, nanyi mnijibu, kisha nitawaambia ni kwa mamlaka gani nayatenda haya.

30Ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu? Nijibuni.

31Wakasemezana wao kwa wao, wakisema, Kama tukisema, Ulitoka mbinguni, atasema, Mbona, basi, hamkumwamini?

32Ila tukisema, Ulitoka kwa wanadamu – waliogopa watu; maana watu wote walimwona Yohana kuwa nabii halisi.

33Wakamjibu Yesu, wakasema, Hatujui. Yesu akawaambia, Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa mamlaka gani nayatenda haya.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya