Marko 16

Marko 16

Kufufuka kwa Yesu

1Na sabato ilipokwisha kupita, Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yakobo, na Salome walinunua manukato wapate kwenda kumpaka.[#Mt 28:1-8; Lk 24:1-12; Yn 20:1-10]

2Na alfajiri mapema, siku ya kwanza ya juma, wakaenda kaburini, jua lilipoanza kuchomoza;

3wakasemezana wao kwa wao, Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe mlangoni pa kaburi?

4Hata walipotazama, waliona ya kuwa lile jiwe limekwisha kuvingirishwa; nalo lilikuwa kubwa mno.

5Wakaingia kaburini wakaona kijana akiwa ameketi upande wa kulia, amevaa vazi jeupe; wakastaajabu.

6Naye akawaambia, Msistaajabu; mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyesulubiwa; amefufuka; hayupo hapa; patazameni mahali walipomweka.

7Lakini nendeni zenu, mkawaambie wanafunzi wake, na Petro, ya kwamba awatangulia kwenda Galilaya; huko mtamwona, kama alivyowaambia.[#Mt 26:32; Mk 14:28]

8Wakatoka nje, wakakimbia kutoka kaburini; kwa maana wameingiwa na hofu na mshangao; wala hawakumwambia mtu neno, maana waliogopa.

Yesu amtokea Mariamu Magdalene

[

9Naye alipofufuka alfajiri siku ya kwanza ya juma, alimtokea kwanza Mariamu Magdalene, ambaye alikuwa amemtoa pepo saba.[#Lk 8:2; Yn 20:11-18]

10Huyo akashika njia akawapasha habari wale waliokuwa pamoja naye, nao wapokuwa wanaomboleza na kulia.

11Lakini hao waliposikia kwamba yu hai, naye amemwona, hawakuamini.

Yesu awatokea wanafunzi wawili

12Baada ya hayo akawatokea wawili miongoni mwao, akiwa na sura nyingine; nao walikuwa wakitembea njiani kwenda mashambani.[#Lk 24:13-35]

13Na hao wakaenda zao wakawapa habari wale wengine; wala hao hawakuwaamini.

Yesu awatuma wanafunzi

14Baadaye akaonekana na wale kumi na mmoja walipokuwa wakila, akawakemea kwa kutoamini kwao na ugumu wa mioyo yao, kwa kuwa hawakuwasadiki wale waliomwona alipofufuka katika wafu.[#Lk 24:36-49; Yn 20:19-23]

15Akawaambia, Nendeni ulimwenguni kote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.[#Mdo 1:8; Mt 28:18-20]

16Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.[#Mdo 2:38]

17Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya;[#Mdo 16:18; 2:4,11; 10:46]

18watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kuua, hakitawadhuru kamwe; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapona.[#Lk 10:19; Mdo 28:3-6; Yak 5:14,15]

Kupaa kwa Yesu

19Basi Bwana Yesu, baada ya kusema nao, akachukuliwa juu mbinguni, akaketi mkono wa kulia wa Mungu.[#Mdo 1:9-11; Lk 24:50-53; 1 Tim 3:16; Zab 110:1; Mdo 7:55; 2 Fal 2:11]

20Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.][#Ebr 2:4]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya