The chat will start when you send the first message.
1Akaanza kufundisha tena kando ya ziwa. Kundi kubwa sana la watu wakamkusanyikia, hata yeye akapanda katika mashua, akakaa ziwani, watu wote walikuwa katika nchi kavu kando ya ziwa.[#Mt 13:1-28; Lk 8:4-15; #Lk 5:1-3]
2Akawafundisha mambo mengi kwa mifano, akawaambia katika mafundisho yake,
3Sikilizeni; Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda;
4ikawa alipokuwa akipanda, mbegu nyingine ilianguka kando ya njia, wakaja ndege wakaila.
5Nyingine ikaanguka penye mwamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara ikaota kwa kuwa na udongo haba;
6hata jua lilipozuka iliungua, na kwa kuwa haina mizizi ikanyauka.
7Nyingine ikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea ikaisonga, isizae matunda.
8Nyingine zikaanguka penye udongo ulio mzuri, zikazaa matunda, zikimea na kukua, na kuzaa, moja thelathini, moja sitini, na moja mia.
9Akasema, Aliye na masikio ya kusikilia, na asikie.
10Naye alipokuwa peke yake, wale watu waliomzunguka, na wale Kumi na Wawili, walimwuliza kuhusu ile mifano.
11Akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuijua siri ya ufalme wa Mungu, bali kwa wale walio nje, yote hufanywa kwa mifano,[#1 Kor 5:12]
12ili wakitazama watazame, wasione;[#Isa 6:9,10; Yn 12:40; Mdo 28:26]
Na wakisikia wasikie, wasielewe;
Wasije wakaongoka, na kusamehewa.
13Akawaambia, Hamjui mfano huu? Basi mifano yote mtaitambuaje?
14Mpanzi huyo hulipanda neno.
15Hawa ndio walio kando ya njia lipandwapo neno; nao, wakiisha kusikia, mara huja Shetani, akaliondoa lile neno lililopandwa mioyoni mwao.
16Kadhalika na hawa ndio wapandwao penye miamba, ambao kwamba wakiisha kulisikia lile neno, mara hulipokea kwa furaha;
17ila hawana mizizi ndani yao, bali hudumu muda mchache; kisha ikitokea dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara hujikwaa.
18Na hawa ndio wale wapandwao penye miiba; ni watu walisikiao lile neno,
19na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali, na tamaa za mambo mengine zikiingia, hulisonga lile neno, likawa halizai.[#Mk 10:23,24]
20Na hawa ndio waliopandwa penye udongo ulio mzuri; ni watu walisikiao lile neno na kulipokea, na kuzaa matunda, mmoja thelathini, mmoja sitini, na mmoja mia.
21Akawaambia, Mwaonaje? Taa huja ili kuwekwa chini ya pishi, au mvunguni? Si kuwekwa juu ya kiango?[#Lk 8:16-18; #Mt 5:15; Lk 11:33]
22Kwa maana hakuna neno lililositirika, ila kusudi lije kudhihirika; wala hakuna lililofichwa, ila kusudi lije kutokea wazi.[#Mt 10:26; Lk 12:2]
23Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie.
24Akawaambia, Angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa.[#Mt 7:2; Lk 6:38]
25Kwa maana mwenye kitu atapewa, naye asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa.[#Mt 13:12; 25:29; Lk 19:26]
26Akasema, Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi;
27akawa akilala na kuondoka, usiku na mchana, nayo mbegu ikamea na kukua, asivyojua yeye.[#Yak 5:7]
28Maana nchi huzaa yenyewe; kwanza jani, tena suke, kisha ngano pevu katika suke.
29Hata matunda yakiiva, mara atapeleka mundu, kwa kuwa mavuno yamefika.[#Yoe 3:13]
30Akasema, Tuulinganishe na nini ufalme wa Mungu? Au tuutie katika mfano gani?[#Mt 13:31,32,34; Lk 13:18,19]
31Ni kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi,
32lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake.[#Dan 4:12,21; Eze 17:23; 31:6]
33Kwa mifano mingi ya namna hii alikuwa akisema nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulisikia;
34wala pasipo mfano hakusema nao; lakini akawaeleza wanafunzi wake mwenyewe mambo yote kwa faragha.
35Siku hiyo kulipokuwa jioni, Yesu akawaambia, Na tuvuke mpaka ng'ambo.[#Mt 8:18,23-27; Lk 8:22-25; #4:35 Katika Kigiriki hakuna Yesu.]
36Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile alivyokuwa katika mashua. Na mashua zingine zilikuwako pamoja naye.
37Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakaipiga mashua hata ikaanza kujaa maji.
38Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia?
39Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu.
40Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?
41Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?