The chat will start when you send the first message.
1Afadhali mego kavu pamoja na utulivu,
Kuliko nyumba yenye karamu nyingi pamoja na magomvi.
2Mtumwa atendaye kwa busara atamtawala mwana atendaye mambo ya aibu;
Tena atapata sehemu ya urithi kati ya ndugu.
3Kalibu ni kwa fedha, na tanuri kwa dhahabu;[#Zab 26:2; Mit 27:21; Yer 17:10; Mal 3:3]
Bali BWANA huijaribu mioyo.
4Mtenda mabaya husikiliza midomo ya uovu;
Na mwongo hutega sikio lake kusikiliza ulimi wa madhara.
5Amchekaye maskini humtukana Muumba wake;[#Ayu 31:29; Mit 24:17; Oba 1:12]
Naye aufurahiaye msiba hatakosa adhabu.
6Wana wa wana ndio taji la wazee,
Na utukufu wa watoto ni baba zao.
7Maneno mazuri hayapendezi kinywani mwa mpumbavu;
Sembuse midomo ya uongo kinywani mwa mkuu.
8Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliye nacho;[#Mwa 39:21; Dan 6:3]
Kila kigeukapo hufanikiwa.
9Afunikaye kosa hutafuta kupendwa;
Bali yeye afichuaye siri hutenga rafiki.
10Lawama hupenya moyoni mwa mwenye ufahamu,
Kuliko mapigo mia moyoni mwa mpumbavu.
11Mtu mwovu hataki neno ila kuasi tu;
Kwa hiyo mjumbe mkali atatumwa kwake.
12Afadhali mtu akutwe na dubu jike aliyenyang'anywa watoto wake,
Kuliko na mpumbavu katika upumbavu wake.
13Yeye arudishaye mabaya badala ya mema,[#Yer 18:20; Rum 12:17; 1 The 5:15]
Mabaya hayataondoka nyumbani mwake.
14Mwanzo wa ugomvi ni kama kutoboa penye maji;[#Mit 20:3; Mdo 6:1; Rum 12:18; 1 The 4:11]
Basi acheni ugomvi kabla haujafurika.
15Yeye asemaye kwamba asiye haki ana haki;[#Kut 23:7; Isa 5:23]
naye asemaye kwamba mwenye haki hana haki;
Hao wote wawili ni chukizo kwa BWANA.
16Nini maana yake, mpumbavu kuwa na fedha mkononi mwake ya kununulia hekima,
Ikiwa hana moyo wa ufahamu?
17Rafiki hupenda sikuzote;
Na ndugu amezaliwa kwa siku ya taabu.
18Asiye na hekima hupeana mkono na mtu;
Na kuwa mdhamini wa mtu mwingine.
19Apendaye ugomvi hupenda dhambi;
Auinuaye sana mlango wake hutafuta uharibifu.
20Mtu mwenye moyo wa ukaidi hatapata mema;
Na mwenye ulimi wa upotovu huanguka katika misiba.
21Azaaye mpumbavu ni kwa huzuni yake mwenyewe;
Wala baba wa mpumbavu hana furaha.
22Moyo uliochangamka ni dawa nzuri;
Bali roho iliyopondeka huikausha mifupa.
23Asiye haki hutoa rushwa kifuani,[#Kut 23:8]
Ili kuzipotosha njia za hukumu.
24Hekima huwa machoni pake mwenye ufahamu;[#Mhu 2:14]
Bali macho ya mpumbavu huwa katika ncha za dunia.
25Mwana mpumbavu ni huzuni kwa babaye,
Na uchungu kwa mamaye aliyemzaa.
26Tena kumwadhibu mwenye haki si vizuri;
Wala si vyema kuwapiga wakuu kwa unyofu wao.
27Azuiaye maneno yake ni mwenye maarifa;[#Yak 1:19]
Na mwenye roho ya utulivu ana busara.
28Hata mpumbavu akinyamaza, huhesabiwa hekima;
Akifumba midomo yake, huhesabiwa ufahamu.