Mithali 27

Mithali 27

1Usijisifu kwa ajili ya kesho;[#Yak 4:13-16; Lk 12:19]

Kwa maana hujui yatakayozaliwa na siku moja.

2Mwingine na akusifu wala si kinywa chako mwenyewe;

Mtu mgeni wala si midomo yako wewe.

3Jiwe ni zito, na mchanga hulemea;[#Est 1:12]

Lakini ghadhabu ya mpumbavu ni nzito kuliko hivi vyote viwili.

4Ghadhabu ni kali, na hasira ni gharika;[#1 Yoh 3:12]

Lakini ni nani awezaye kusimama mbele ya wivu.

5Lawama ya wazi ni heri,[#Gal 2:14]

Kuliko upendo uliositirika.

6Majeraha utiwazo na rafiki ni ya kweli;

Bali busu la adui ni udanganyifu.

7Nafsi iliyoshiba hukinai sega la asali;

Bali nafsi yenye njaa huona kila kitu kichungu kuwa kitamu.

8Kama ndege aendaye huku na huko mbali na kitundu chake;[#Ayu 39:14]

Ndivyo alivyo mtu aendaye huku na huko mbali na mahali pake.

9Marhamu na manukato huufurahisha moyo;

Kadhalika utamu wa rafiki ya mtu utokao katika kusudi la moyo wake.

10Usimwache rafiki yako mwenyewe, wala rafiki ya baba yako,

Wala usiende nyumbani mwa ndugu yako siku ya msiba wako.

Afadhali jirani aliye karibu kuliko ndugu aliye mbali.

11Mwanangu, uwe na hekima na kunifurahisha moyo wangu;[#Zab 119:42]

Ili nipate kumjibu anilaumuye.

12Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha;[#Isa 32:2]

Bali wajinga huendelea mbele wakaumia.

13Twaa nguo yake amdhaminiye mgeni;

Mtoza rehani aliye mdhamini wa malaya.

14Mtu ambarikiye mwenzake kwa sauti kuu asubuhi na mapema;[#Zab 12:2]

Itahesabiwa kuwa ni laana kwake.

15Matone daima kudondoka siku ya mvua nyingi,[#Mit 19:13]

Na mwanamke mgomvi ni sawasawa;

16Atakaye kumzuia huyo huuzuia upepo;

Na mkono wake wa kulia hukuta mafuta.

17Chuma hunoa chuma;

Ndivyo mtu aunoavyo uso wa rafiki yake.

18Yeye autunzaye mtini atakula matunda yake;[#Kum 20:6; 1 Fal 11:8; Mit 12:24; 1 Kor 3:8]

Naye amhudumiaye bwana wake ataheshimiwa.

19Kama uso ufananavyo na uso katika maji;

Kadhalika moyo wa mtu na mwenzake.

20Kuzimu na Uharibifu havishibi;[#Mit 30:15,16; Hab 2:5]

Wala macho ya wanadamu hayashibi.

21Kalibu ni kwa fedha, na tanuri kwa dhahabu;

Na mtu hujaribiwa kwa sifa zake.

22Hata ukimtwanga mpumbavu kwa mchi kinuni pamoja na ngano;

Upumbavu wake hautamtoka.

23Fanya bidii kuijua hali ya makundi yako;

Na kuwaangalia sana ng'ombe wako.

24Kwa maana mali haziwi za milele;

Na taji je! Ladumu tangu kizazi hata kizazi?

25Manyasi hukatwa, na majani mabichi huchipua,

Na mboga ya mlimani hukusanywa.

26Wana-kondoo hufaa kwa mavazi yako;

Na mbuzi ni thamani ya shamba.

27Tena yatakuwapo maziwa ya mbuzi,

Ya kukutosha kwa chakula chako,

Na chakula cha watu wa nyumbani mwako,

Na posho la vijakazi vyako.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya