Mithali 4

Mithali 4

Ushauri wa mzazi

1Wanangu, yasikilizeni mausia ya baba yenu,[#Zab 34:11; Mit 1:8]

Tegeni masikio mpate kujua ufahamu.

2Kwa kuwa nawapa mafundisho mazuri;

Msiiache sheria yangu.

3Maana nilikuwa mwana kwa baba yangu,[#2 Sam 12:24; 1 Nya 29:1]

Mpole, mpenzi wa pekee wa mama yangu.

4Naye akanifundisha, akaniambia,[#1 Nya 28:9; Efe 6:4]

Moyo wako uyahifadhi maneno yangu;

Shika amri zangu ukaishi.

5Jipatie hekima, jipatie ufahamu; usiusahau;

Wala usiyakatae maneno ya kinywa changu.

6Usimwache, naye atakusitiri;[#2 The 2:10]

Umpende, naye atakulinda.

7Bora hekima, basi jipatie hekima;[#Mt 13:44; Lk 10:42]

Naam, kwa mapato yako yote jipatie ufahamu.

8Umtukuze, naye atakukuza;[#1 Sam 2:30; Dan 12:3]

Atakupatia heshima, ukimkumbatia.

9Atakupa neema kuwa kilemba kichwani;

Na kukukirimia taji la uzuri.

Maonyo kuhusu kushika njia ya haki

10Mwanangu, sikiliza, na kuzipokea kauli zangu;

Na miaka ya maisha yako itakuwa mingi.

11Nimekufundisha katika njia ya hekima;

Nimekuongoza katika mapito ya unyofu.

12Uendapo, hatua zako hazitadhiikika,[#Zab 18:36; 91:11; Mit 3:23; 4:19; Yer 13:16; Yn 11:9,10]

Wala ukipiga mbio hutajikwaa.

13Mkamate sana elimu, usimwache aende zake;

Mshike, maana yeye ni uzima wako.

14Usiingie katika njia ya waovu,

Wala usitembee katika njia ya wabaya.

15Jiepushe nayo, usipite karibu nayo,

Igeukie mbali, ukaende zako.

16Maana hawalali isipokuwa wametenda madhara;

Huondolewa usingizi, ikiwa hawakumwangusha mtu.

17Maana wao hula mkate wa uovu,

Nao hunywa divai ya ujeuri.

18Bali njia ya wenye haki ni kama nuru ing'aayo,[#Mt 5:14; Flp 2:15; 2 Sam 23:4]

Ikizidi kung'aa hata mchana mkamilifu.

19Njia ya waovu ni kama giza;[#1 Sam 2:9; Ayu 5:14; Isa 59:9,10; Yer 13:16; Yn 12:35]

Hawajui ni kitu gani kiwakwazacho.

20Mwanangu, sikiliza maneno yangu;

Tega sikio lako, uzisikie kauli zangu.

21Zisiondoke machoni pako;

Uzihifadhi ndani ya moyo wako.

22Maana ni uhai kwa wale wazipatao,

Na afya ya mwili wao wote.

23Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo;

Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.

24Jiepushe na kinywa cha ujeuri,

Na midomo ya upotovu uiweke mbali nawe.

25Macho yako yatazame mbele,

Na kope zako zitazame mbele yako sawasawa.

26Ulisawazishe pito la mguu wako,[#Ebr 12:13]

Na njia zako zote zithibitike;

27Usigeuke kwa kulia wala kwa kushoto;[#Isa 1:16]

Ondoa mguu wako maovuni.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya