The chat will start when you send the first message.
1Mwanangu, yashike maneno yangu,
Na kuziweka amri zangu akiba kwako.
2Uzishike amri zangu ukaishi,[#Law 18:5; Mit 4:4; Isa 55:3; Kum 32:10]
Na sheria yangu kama mboni ya jicho lako.
3Zifunge katika vidole vyako;[#Kum 6:8; Mit 3:3; Isa 30:8; Yer 17:1; 2 Kor 3:3]
Ziandike juu ya kibao cha moyo wako.
4Mwambie hekima, Wewe ndiwe dada yangu;
Mwite ufahamu jamaa yako mwandani.
5Wapate kukulinda na malaya,
Na mwasherati akubembelezaye kwa maneno yake.
6Maana katika dirisha la nyumba yangu
Nilichungulia katika shubaka yake.
7Nikaona katikati ya wajinga,[#Mit 6:32]
Nikamtambua miongoni mwa vijana,
Kijana mmoja asiyekuwa na akili,
8Akipita njiani karibu na pembe yake,
Akiishika njia iendayo nyumbani kwake,
9Wakati wa magharibi, wakati wa jioni,[#Ayu 24:15]
Usiku wa manane, gizani.
10Na tazama, mwanamke akamkuta,[#1 Tim 2:9]
Ana mavazi ya kikahaba, mwerevu wa moyo;
11Ana kelele, na ukaidi;[#1 Tim 5:13; Tit 2:5]
Miguu yake haikai nyumbani mwake.
12Mara yuko katika njia kuu, mara viwanjani,
Naye huotea kwenye pembe za kila njia.
13Basi akamshika, akambusu,
Akamwambia kwa uso usio na haya,
14Kwangu ziko sadaka za amani;
Leo hivi nimeziondoa nadhiri zangu;
15Ndiyo maana nikatoka nikulaki,
Nikutafute uso wako kwa bidii, nami nimekuona.
16Nimetandika kitanda changu, magodoro mazuri,[#Isa 19:9]
Kwa matandiko ya Kimisri yenye mistari.
17Nimetia kitanda changu manukato,
Manemane na udi na mdalasini.
18Haya, na tushibe upendo hadi asubuhi,
Tujifurahishe nafsi zetu kwa mahaba.
19Maana mume wangu hayumo nyumbani,
Amekwenda safari ya mbali;
20Amechukua mfuko wa fedha mkononi;
Atarudi wakati wa mwezi mpevu.
21Kwa maneno yake mengi na ulaini akamshawishi,
Kwa ubembelezi wa midomo yake akamshinda.
22Huyo akafuatana naye mara hiyo,
Kama vile ng'ombe aendavyo machinjoni;
Au mpumbavu kuadhibiwa katika pingu;
23Hata mshale umchome maini;
Kama ndege aendaye haraka mtegoni;
Wala hajui ya kuwa ni hasara ya nafsi yake.
24Basi, wanangu, nisikilizeni sasa,
Mkayaangalie maneno ya kinywa changu.
25Moyo wako usizielekee njia zake,
Wala usipotee katika mapito yake.
26Maana amewaangusha wengi aliowajeruhi,[#Neh 13:26]
Naam, jumla ya waliouawa naye ni wengi.
27Nyumba yake ni njia ya kwenda kuzimu,[#Mit 2:18; 1 Kor 6:9,10; Ebr 13:4; Ufu 22:15]
Hushuka mpaka vyumba vya mauti.