Zaburi 53

Zaburi 53

Kushutumiwa kwa wasiomwamini Mungu

1Mpumbavu husema moyoni, Hakuna Mungu;[#Rum 3:10-12; Zab 10:4]

Ni wafisadi, na wametenda mambo ya kuchukiza,

Hakuna atendaye mema.

2Toka mbinguni MUNGU aliwachungulia wanadamu,[#Zab 33:13; 2 Nya 15:2]

Aone kama yuko mtu mwenye hekima,

Amtafutaye Mungu.

3Kila mtu amepotoka, wameoza wote pamoja,[#Mhu 7:29]

Hakuna atendaye mema,

La! Hata mmoja.

4Je! Wafanyao maovu hawajui?[#Yer 4:22]

Walao watu wangu kama walavyo mkate,

Hawakumwita MUNGU.

5Hapo waliingiwa na hofu pasipokuwapo hofu,

Maana Mungu ameitawanya mifupa yake aliyekuhusuru.

Umewatia aibu,

Kwa sababu MUNGU amewadharau.

6Laiti wokovu wa Israeli utoke katika Sayuni!

MUNGU awarudishapo wafungwa wa watu wake;

Yakobo atashangilia,

Israeli atafurahi.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya