The chat will start when you send the first message.
1Ni neno jema kumshukuru BWANA,
Na kuliimbia jina lako sifa, Ee Uliye Juu.
2Kuzitangaza rehema zako asubuhi,
Na uaminifu wako wakati wa usiku.
3Kwa chombo chenye nyuzi kumi,
Na kwa kinanda,
Na kwa mlio wa kinubi.
4Kwa kuwa umenifurahisha, BWANA,
Kwa kazi yako; nitashangilia
Kwa ajili ya matendo ya mikono yako.
5Ee BWANA, jinsi yalivyo makuu matendo yako![#Isa 28:29; Rum 11:23]
Mawazo yako ni mafumbo makubwa.
6Mtu mjinga hayatambui hayo,[#Zab 73:22]
Wala mpumbavu hayafahamu.
7Hata wasio haki wakichipuka kama majani[#Ayu 21:7; Yer 12:1; Mal 3:15]
Na wote watendao maovu wakastawi.
Mwishowe wataangamizwa milele;
8Bali Wewe, BWANA, U Mtukufu hata milele.
9Maana hao adui zako, Ee BWANA,
Hao adui zako watapotea,
Na watendao maovu watatawanyika wote pia.
10Bali pembe yangu umeiinua kama pembe ya nyati,
Nimepakwa mafuta mabichi.
11Na jicho langu limeona kuanguka kwa adui zangu,
Sikio langu limesikia maangamizi ya waovu walionishambulia.
12Mwenye haki atastawi kama mtende,[#Zab 52:8; Wim 7:7]
Atakua kama mwerezi wa Lebanoni.
13Waliopandwa katika nyumba ya BWANA[#Isa 60:21; Mt 15:13; Yn 15:2,5]
Watastawi katika nyua za Mungu wetu.
14Watazaa matunda hadi wakati wa uzee,
Watajaa utomvu, watakuwa na ubichi.
15Watangaze ya kuwa BWANA ni mwenye adili,[#Kum 32:4; Rum 9:14]
Mwamba wangu, ndani yake hamna udhalimu.