The chat will start when you send the first message.
1Kazi aliye na hekima atawafundisha watu wake; na utawala wa mwenye ufahamu utakuwa na utaratibu.
2Alivyo mhukumu watu, ndivyo walivyo watumishi wake; na alivyo mkuu wa mji, ndivyo walivyo wakaao humo.
3Mfalme asiye na elimu atawaharibu watu wake; bali mji utathibitishwa kwa ufahamu wa wakuu.
4Mkononi mwa BWANA mna utawala wa dunia; na wakati upasao atainua juu yake mtu wa kufaa.
5Mkononi mwa BWANA mna kufanikiwa kwa mwanadamu; pia juu ya mwandishi ataweka heshima imhusuyo.
6Usimkasirikie jirani yako kwa kila kosa; wala usifanye neno kwa kutenda jeuri.
7Kiburi ni chukizo kwa BWANA, pia kwa wanadamu; maadamu mbele ya wote yasiyo haki ndiyo makosa.
8Kuhusu utawala taifa hupisha taifa kwa ajili ya udhalimu, ujeuri, na tamaa ya fedha.
9Mbona yule aliye udongo na mavumbi tu hufanya kiburi? Naye aweza angali hai kupata mchango wa tumboni;
10ugonjwa ni wa siku nyingi, tabibu hushindwa, leo huyo ni mfalme, na kesho amekufa!
11Kwa maana hakika akiisha kufa, mtu atarithi vitambaavyo na vidudu na mchango.
12Kiini cha kiburi ni mtu kumwacha BWANA; moyo wake umejitenga na Mola wake.
13Yaani, chanzo cha kiburi ni dhambi; yeye aishikaye atafurika machukizo. Ndiyo sababu BWANA alileta juu ya wanadamu misiba ya kutisha, akawaangamiza kabisa;
14BWANA akawaondoa wakuu katika viti vyao, akawakweza wanyonge mahali pao;[#1 Sam 2:8; Lk 1:52]
15BWANA akaing'oa mizizi ya mataifa, akawapanda wanyenyekevu badala yao;
16BWANA akaziharibu hata dalili za mataifa mengine, na mashina yao hata pande za ndani za nchi;
17baadhi yao akawatawanya, akawaharibu, akalikomesha kumbukumbu lao duniani.
18Naam, kiburi sicho kilichoumbwa kwa ajili ya wanadamu, wala ghadhabu kali kwa ajili yao waliozaliwa na wanawake.
19Mzao gani ana heshima?
Wanadamu.
Mzao gani ana heshima?
Wamchao BWANA.
Mzao gani hana heshima?
Wanadamu.
Mzao gani hana heshima?
Waasio amri.
20Miongoni mwa ndugu awatawalaye ana heshima; bali machoni pa BWANA ni wao wamchao.
22Tajiri na mstahiki na maskini, kujisifu kwao wote ni katika kumcha BWANA.
23Si haki kumdharau maskini, naye anao ufahamu; wala si haki kumtukuza tajiri aliye mkosaji.
24Mkuu na kadhi na shujaa watasifiwa, walakini hakuna mmoja wao aliye mkuu kuliko yeye amchaye BWANA.
25Hata walio huru waweza kumhudumia mtumwa mwenye hekima, wala hakuna mwenye ufahamu atakayenung'unika.
26Usijione mtaalamu wakati ufanyapo kazi ya mikono, wala usijikuze wakati uonapo uhitaji;
27afadhali afanyaye kazi na kupata wingi kwayo, kuliko ajikuzaye lakini hana chakula.
28Mwanangu, kujisifu ujisifu katika unyenyekevu, na kujiheshimu mwenyewe sawasawa na stahili zako.
29Nani atamhesabia haki yeye atendaye dhambi juu ya nafsi yake? Nani atakayemtukuza yule mwenye kujiaibisha yeye mwenyewe?
30Maskini hutukuzwa kwa akili zake, na tajiri hutukuzwa kwa mali zake;
31walakini atukuzwaye katika umaskini, si zaidi katika utajiri? Naye aliye na aibu katika utajiri, si zaidi katika umaskini?