Yoshua Mwana wa Sira 20

Yoshua Mwana wa Sira 20

Kunyamaza na Kusema

1Kuna kumhoji mtu nako si wajibu; tena kuna mtu anyamazaye naye anayo busara.

2Jinsi vilivyo vizuri kumhoji mtu mahali pa kumkasirikia,

3naye akiriye atahifadhika asipate hasara.

4Kama towashi akitaka kumkumbatia bikira, ndivyo alivyo mtu yeyote anayetekeleza hukumu kwa ujeuri.

5Yuko anyamazaye akaonekana ana hekima; yuko naye mwenye maneno mengi akachukiwa.

6Yuko anyamazaye kwa sababu hana la kujibu; yuko naye anyamazaye ambaye anajua wakati ufaao.

7Mwenye hekima atanyamaza hata wakati wake utakapowadia; bali mjigamba mpumbavu ataikosa nafasi yake.

8Mtu wa maneno mengi atachukiza, na mwenye kujidai mamlaka nayo atakirihiwa. Mwenye hekima ya usemi atajipendekeza, bali ubishi wa wapumbavu ni kazi bure.

Pambanisho la maneno

9Kuna mtu aonaye nafuu katika masaibu; tena kuna faida nayo hugeuka kuwa hasara.

10Kuna kipawa kisichokufaidia; tena kuna kipawa na malipo yake ni maradufu.

11Kuna unyonge utokao katika utukufu; tena yuko aliyeinuliwa kichwa kutoka unyonge.

12-13Tena anunuaye wingi kwa haba aweza pengine kuulipia mara saba.

14Kipawa cha mpumbavu si faida kwako,

Maana macho yake ni mengi si moja.

15Atatoa kidogo tu, na kukaripia kwa wingi; atapanua kinywa chake kama mpiga mbiu; leo atatoa na kesho atataka tena; mtu wa namna hiyo ni makuruhu.

16Mpumbavu husema, mimi sina rafiki;

Sitolewi asante kwa ukarimu wangu;

17Walao mkate ni bahili wa shukrani.

Je! Mara ngapi watu wangapi watamdhihaki huyo!

Kusema Isivyofaa

18Kuteleza sakafuni si kuteleza kwa ulimi;

Kadhalika wazembe huanguka kwa ghafla.

19Hadithi iliyosimuliwa wakati usiofaa ni mfano wa mkia wa kondoo wenye mafuta uliwapo pasipo chumvi.

20Katika kinywa cha mpumbavu hata mfano utakataliwa, mahali hatanena wakati ufaao.

21Yuko aliyezuiwa na dhiki asikose,

Atakapostarehe hataona fadhaa.

22Pia yuko mwenye kuiharibu roho yake kwa kuona haya; pia na kwa sura ya ubaradhuli aweza kuiharibu.

23Tena kwa kuona haya kuna mtu mwenye kumwahidia rafiki yake, na kumgeuza kuwa adui bure.

Kusema Uongo

24Uongo ni waa la unajisi katika mtu;

Utakuwamo daima kinywani mwa mjinga.

25Afadhali mwizi kuliko mwongo wa daima; lakini wote wawili watarithi maangamizi.

26Sifa ya mwongo ni fedheha, na aibu yake inadumu daima.

Heshima na hatari ya mtu mwenye Hekima

27Mwenye hekima ya usemi atajikweza,

Na mwenye busara atawapendeza wakuu.

28Alimaye shamba atalundisha chungu yake iwe kubwa; tena mtu awapendezaye wakuu atasamehewa makosa.

29Zawadi na vipawa vyaweza kuwapofusha hata wenye hekima, na kama kufunga mdomo kinywani hugeuzia mbali makaripio.

30Hekima iliyofichika,

Na mali iliyostirika,

Mna faida gani ndani yake zote mbili?

31Afadhali aufichaye upumbavu,

Kuliko aifichaye hekima yake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya