Yoshua Mwana wa Sira 22

Yoshua Mwana wa Sira 22

Mvivu

1Mvivu hufanana na jiwe litiwalo mavi,

Kila mtu atamfyonya katika aibu yake.

2Mvivu hufanana na uchafu wa jaani,

Kila augusaye atakung'uta mkono.

Watoto Wapotovu

3Ni aibu ya baba kuzaa mwana aliye juha,

Na binti asiye na akili ni hasara yake.

4Binti mwenye busara ni tunu kwa mumewe;

Bali aletaye aibu ni huzuni ya mzazi wake.

5Aliye mtundu huwaaibisha baba na mume,

Naye atadharauliwa na wote wawili.

6-7-8Mafundisho wakati usiofaa ni ngoma kwenye kilio;

Bali mapigo na adhabu ni hekima wakati wowote.

Hekima na Ujinga

9Amfundishaye mpumbavu ni kama mwenye kuunga vigae;

Kama mwenye kumwamsha mtu alalaye usingizi mzito.

10Mtu anayezungumza pamoja na mpumbavu amefanana na yeye anayezungumza na mwenye kusinzia; mwishowe atasema, Nini?

11Umlilie aliyefariki,

Kwa maana amepotewa na nuru;

Umlilie mpumbavu naye

Kwa maana amepotewa na akili.

Umlilie kiasi aliyefariki,

Kwa maana ameingia rahani;

Bali maisha ya upumbavu

Ni mabaya kuliko mauti.

12Siku saba ndizo siku za kilio chake aliyefariki;[#Mwa 50:10; Ydt 16:24]

Bali kwa mpumbavu ni siku zote za maisha yake.

13Usizidi kuongea na mpumbavu,

Wala usimwendee asiye na akili.

Ujihadhari naye usije ukapata matata; wala usitiwe unajisi atakapojikung'uta. Ujigeuzie mbali naye, nawe utapata raha; wala hutakuja kuchoka kwa ajili ya wazimu wake.

14Nini iliyo nzito kuliko risasi?

Na jina lake nani? Ila mpumbavu!

15Mchanga na chumvi na chuma kitupu,

Ni rahisi kuhimili kuliko mpumbavu.

16Maboriti yaliyokazwa katika jengo hayatalegalega wakati wa tetemeko; vivyo hivyo moyo uliothibitishwa katika shauri lenye njia hautaogopa wakati wa hatari.

17Moyo uliokazwa juu ya akili zingativu umefanana na pambo la lipu juu ya ukuta uliokatuka.

18Mbwe juu ya ukuta mrefu hazitakaa mbele ya upepo; vivyo hivyo na moyo mwoga katika wazo la mpumbavu hautasimama mbele ya hofu yoyote.

Jinsi ya Kutunza Urafiki

19Alitiaye jicho jeraha hutokeza machozi, naye autiaye moyo jeraha huvunja urafiki.

20Mwenye kuwatupia ndege mawe huwafukuza, naye anayemkaripia rafiki huondoa urafiki.

21Ukiwa umefuta upanga juu ya rafiki, usikate tamaa,

Yawezekana kuwa kurudiana;

22Ukiwa umefumbua kinywa juu ya rafiki, usiogope,

Yawezekana kuwa kupatana tena.

Isipokuwa kwa ajili ya lawama na jeuri,

Na kuifunua siri yake,

Na mapigo yaliyotendeka katika uhaini;

Kwa hayo kila rafiki hukimbia.

23Upate kuaminiwa na jirani yako wakati wa umaskini wake, ili wakati atakapofanikiwa upate nawe kuchangamka; uwe thabiti kwake wakati anapoteswa, ili uwe mrithi pamoja naye katika urithi wake.

24Upo moshi wa tanuri kabla ya moto; kadhalika yapo matukano kabla ya kumwaga damu.

25Usione haya kumsitiri rafiki yako, wala usijifiche machoni pake;

26akikuambia siri usiitangaze, mtu asikiaye asije akakudhania u mfitini.

Sala ya Kusaidiwa juu ya Dhambi

27Nani ataweka mlinzi kinywani pangu,

Na mhuri midomoni mwangu?

Nisije nikaanguka kwa ajili yake,

Na ulimi wangu ukaniangamiza.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya