The chat will start when you send the first message.
1Mwenye kujilipiza kisasi ataona kisasi kutoka kwa BWANA; hakika Yeye atamfungia dhambi zake.
2Umsamehe jirani yako dhara alilokufanyia, hivyo nawe utasamehewa dhambi zako wakati utakaposali.[#Mt 6:17; Mk 11:25]
3Mwanadamu humkasirikia mwanadamu, je! Atatafuta kuponywa na BWANA?
4Hamrehemu mwanadamu aliye mwenzake, je! Atalalamika kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe?
5Aliye mwili na damu tu huilisha hasira yake, je! Ni nani atakayempatanisha yeye kwa makosa yake?
6Basi kumbuka mwisho wako, uuache uadui; kumbuka uoza na mauti, ujiepushe na kutenda dhambi.
7Kumbuka zile amri, usikasirike na jirani yako; nawe ulikumbuke agano lake Aliye Juu, umwachilie ujinga wake.
8Acha ugomvi, nawe utazipunguza dhambi zako; maana mwenye ghadhabu kuchochea ugomvi,
9na mchongezi huhangaisha rafiki, hata kupenyeza hitilafu kati yao wakaao kwa amani.
10Kama zilivyo kuni zake, ndivyo moto utakavyowaka; na kama ilivyo sababu ya ugomvi, ndivyo huo utakavyozidi. Kama cheo cha mtu, kadhalika ghadhabu yake; na kama uwezo wake, kadhalika ataizidisha hasira.
11Ugomvi ulioanzishwa na haraka huwasha moto, na mapigano ya ghafla humwaga damu.
12Vuvia cheche, itawaka;
Tema juu yake, itazimika;
Na yote mawili yatoka kinywani mwako.
13Mlaani mchongezi aliye mnafiki, madhali amewaharibu wengi waliokaa kwa amani.[#Sira 51:2-6; Yak 3:5-12]
14Ulimi wa msingiziaji umewatikisa wengi, na kuwatawanya toka taifa hata taifa; umebomoa miji yenye nguvu, na kuangamiza nyumba za watu mashuhuri.
15Ulimi wa msingiziaji umewatupa nje wanawake hodari, na kuwanyima kazi zao.
16Wala yeye aliyeusikiliza haoni raha, wala hatakaa katika utulivu.
17Pigo la mjeledi huchapa ngozi, lakini pigo la ulimi laweza kuvunja mifupa.
18Ni wengi walioanguka kwa upanga, lakini wengi zaidi kwa sababu ya ulimi.
19Heri aliyesitiriwa nao, asiyeipitia ghadhabu yake asiyeivuta nira yake, wala kufungwa kwa kamba zake.
20Kwa kuwa nira yake ni ya chuma, na kamba zake za shaba.
21Mauti uiletayo ni kufa kubaya, kuna raha kuzimuni zaidi ya na huo.
22Huo hautatawala wenye haki, wala hawataungua katika miali ya moto wake;
23wale waliomwacha BWANA watautumbukia, nao utawaka kati yao, usizimike. Kama simba utawashambulia, na mfano wa chui utawararua.
24Tazama, ulizungushie shamba lako boma la miiba, na kufunga salama fedha yako na dhahabu;
25fanya mizani na mawe kwa maneno yako, fanya mlango na komeo kwa kinywa chako.
26Angalia usije ukateleza kwa ulimi wako; ukaanguka mbele yake anayekuotea.