The chat will start when you send the first message.
1Kila rafiki atasema, Mimi nami ni rafiki; bali yuko aliye rafiki aliyeitwa tu jina hili.
2Si huzuni, hata kufa, iliyoko, yeye aliye rafiki mwaminifu atakapogeuka kuwa adui?
3Ewe wazo ovu la asili, ya nini kufanyika kwako, hata kufunika nchi kavu kwa hila!
4Yuko mjanja, apendaye kutazamia meza ya rafiki yake, bali wakati wa shida atakaa mbali naye.
5Ndiye rafiki hasa, ambaye atashindana na mgeni kwa ajili yako, na kuishika ngao juu ya adui.
6Usimsahau rafiki yako wakati wa mashindano yako, wala usikose kumkumbuka upatapo mateka yako.
7Aliye mshauri huyakuza mashauri yake; bali yuko atoaye shauri kwa ajili yake mwenyewe.
8Ujihadhari na mshauri, ujue kwanza kama anahitaji kitu, (kwa maana atatoa shauri kwa ajili yake mwenyewe);
9asije akakunasa, akakuambia, Shauri lako li jema; kisha atasimama upande ili aone yatayokupata.
10Usifanye shauri na mtu anayekushuku; na yeye anayekuhusudu umfiche shauri lako.
11Aidha, usifanye shauri na mwanamke juu ya mwenzake; wala na mwoga katika mambo ya vita; wala na mfanya biashara kuhusu bei ya bidhaa; wala na mnunuzi katika habari ya kuuza kitu; wala na bahili juu ya upaji; wala na mkatili juu ya upole; wala na mvivu kwa habari ya kazi yoyote; wala na mtu wa mshahara kuhusu wakati wa kupanda; wala na mtumishi mlegevu juu ya shughuli nyingi; watu hao usiwasikilize katika shauri lolote.
12Bali afadhali sikuzote usuhubiane na mtu mtauwa, unayemjua ya kwamba anazishika amri za BWANA, na moyo wake ni sawasawa na moyo wako, naye atahuzunika pamoja nawe ukipatikana na msiba.
13Lakini ulisimamishe shauri la moyo wako mwenyewe; kwa maana hakuna mtu aliye mwaminifu kwako kuliko moyo wako;
14yaani, pengine moyo wa mtu humwarifu wakati wa kufaa, hata kupita walinzi saba wakaao juu ya mnara.
15Na zaidi ya hayo yote umwombe Aliye Juu, ili Yeye akuongoze hatua zako katika kweli.
16Busara itangulie kila kazi, na mashauri yatangulie kila tendo.
17Shina la mashauri ya moyoni huchipuza matawi manne;
18mema na mabaya, uzima na mauti; na daima mtawala wake ni ulimi.
19Kuna mwenye busara, mkufunzi wa wengi, ila hawezi kujifaidia nafsi yake.
20Kuna mwingine, mwerevu wa maneno, lakini anachukiwa; huyu atakosa riziki;
21kwa jinsi alivyonyimwa hekima, mradi hakupewa na BWANA msemo wa neema.
22Kuna mwenye hekima hasa, naye anaonesha hekima kwa habari ya nafsi yake, na matunda ya ufahamu wake katika mwili wake.
23Kuna mwenye hekima kweli kweli, naye awafundisha watu wake, na matunda ya ufahamu wake ni amini.
24Mwenye hekima atashiba baraka, na wote wamwonao wamwita heri.
25Maisha ya mwanadamu mmoja inahesabika kwa siku, lakini siku za Israeli hazina hesabu;
26tena mwenye hekima miongoni mwa watu atarithi utukufu, na jina lake litadumu milele.
27Mwanangu, jijaribu nafsi yako maadamu u mzima, uviangalie vitu visivyokufaa, usijipatie hivyo.
28Kwa maana si vitu vyote viwafaavyo watu wote, wala siyo kila mtu apendezwaye na kila kitu.
29Usione uchu wa anasa yoyote, wala usiwe na choyo kwa habari ya vyakula vyako.
30Yaani, katika wingi wa vyakula kuna ugonjwa, na ulafi uzidio waleta msokoto wa tumbo.
31Wengi wamekufa kwa sababu ya kula kwa pupa, bali mwenye kujihadhari atauzidisha uzima wake.