Yoshua Mwana wa Sira 40

Yoshua Mwana wa Sira 40

Umaskini wa Binadamu

1Taabu nyingi sana Mungu amemgawia kila mtu, na nira nzito ipo juu ya wanadamu; tangu siku yao ya kutoka tumboni mwa mama zao, hata siku ile watakapoirudia nchi, mama wa wote walio hai.

2Kutazamia mambo yatakayokuja, na siku ya kufariki, huwahangaisha mawazo yao, na kuwaletea hofu ya moyoni;

3tangu yeye aketiye juu ya kiti cha utukufu, hata yeye naye ajidhiliye katika mavumbi na majivu;

4tangu yeye aliyevikwa kilemba au taji, hata yeye naye aliyevaa mavazi ya nywele. Hakuna ila wivu, na matata, na udhia, na hofu ya mauti, na ghadhabu, na ugomvi.

5Hata na wakati wa mtu kupata raha kitandani pake, usingizi wake wa usiku hutaabisha fahamu zake.

6Ama hupata raha kidogo tu, ama hapati; na baadaye katika usingizi wake, kama katika zamu ya kukesha, amefadhaika katika maono ya moyo wake, kama mtu aliyeokoka na ghasia ya vita;

7naam, wakati ule ule wa kuokoka huamka, na kushangaa kuona ya kuwa hofu yake si kitu.

8Ndivyo ilivyo kwa wote wenye mwili, binadamu na hayawani; hata zaidi mara saba juu ya wenye dhambi.

9Mauti, na kumwaga damu, na ugomvi, na upanga; misiba, njaa, dhiki, na tauni;

10mambo hayo yote yaliumbwa kwa ajili ya waovu; pia na kwa sababu yao kulikuja gharika.

11Yote yaliyo ya nchi yairudia nchi, na yote yaliyotoka juu yatarudi huko tena.

Asiye Haki Hatafaulu

12Rushwa na udhalimu utafutiwa mbali,

Bali uaminifu utakaa hata milele.

13Mapato ya mwovu yatakauka kama mto.

Na kama ngurumo penye mvua yatapita.

14Kwa kufumbua mkono mtu atafurahishwa,

Bali wanyimivu watapotelea mbali.

15Watoto wa waasi hawana chipukizi,

Na shina la wasio haki li juu ya jabali.

16Nyasi ya mtoni iotayo ukingoni mwa maji

Itang'olewa kutangulia majani yote.

17Bali ukunjufu ni bustani ya mibaraka,

Na kutoa sadaka kunadumu milele.

Furaha za Maisha

18Mtenda kazi ana maisha mema

Naye pia aliyeona radhi,

Naye aonaye dafina hupita wote wawili.

19Watoto na kujenga mji

Hulithibitisha jina la mtu,

Naye apataye hekima hupita wote wawili,

Kufuga ng'ombe na ulimaji

Hulifanikisha jina la mtu,

Naye mke mpendwa kupita yote mawili.

20Kunywa mvinyo na kuimba

Kunachangamsha moyo,

Na upendano wa rafiki hupita yote mawili.

21Filimbi na kinubi

Hutoa sauti nzuri,

Na ulimi wenye neema hupita vyote viwili.

22Neema na uzuri

Hulifurahisha jicho,

Na jani bichi la mpunga hupita yote mawili.

23Rafiki na mwenzake

Hawakutani vibaya,

Na mke na mumewe hupita wote wawili.

24Udugu na msaada

Hufaa siku ya taabu,

Na sadaka huokoa kupita yote mawili.

25Dhahabu na fedha

Huuimarisha mguu wako,

Na shauri lina staha kupita vyote viwili.

26Mali na nguvu

Vitauinua moyo wako,

Na kumcha BWANA hupita vyote viwili.

Hakuna upungufu katika kumcha BWANA,

Wala hakuna haja kutafuta msaada zaidi;

27Kumcha BWANA ni bustani ya baraka,

Nayo humfunika mtu kupita utukufu wote.

Aibu ya Kuombaomba

28Mwanangu, usiishi maisha ya mwombaji

Ni afadhali kufa kuliko kuomba.

29Mtu anayetazamia meza ya mgeni, maisha yake si maisha. Atainajisi roho yake kwa vyakula vya mtu mwingine, walakini mtu mwenye ufahamu ataviona vinaleta uchungu.

30Kinywani pake mwenye choyo kuomba ni kutamu; bali tumboni mwake huwashwa moto.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya