Wimbo ulio Bora 3

Wimbo ulio Bora 3

Ndoto za mapenzi

1Usiku kitandani nilimtafuta mpendwa wa nafsi yangu,[#Zab 4:6; 6:6; Isa 26:9]

Nilimtafuta, nisimpate.

2Nikasema, Haya, niondoke nizunguke mjini,

Katika njia zake na viwanjani,

Nimtafute mpendwa wa nafsi yangu.

Nikamtafuta, nisimpate.

3Walinzi wazungukao mjini waliniona;[#Wim 5:7; Isa 21:6-8,11,12]

Je! Mmemwona mpendwa wa nafsi yangu?

4Kitambo kidogo tu nilipoachana nao,[#Mit 8:17; 4:13; Rum 8:35,39]

Nikamwona mpendwa wa nafsi yangu;

Nikamshika, nisimwache tena,

Hata nilipomleta nyumbani mwa mamangu,

Chumbani mwake aliyenizaa.

5Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu,[#Wim 2:7]

Kwa paa na kwa ayala wa porini,

Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha,

Hata yatakapoona vema yenyewe.

Bwana arusi na kundi lake wakaribia

6Ni nani huyu apandaye kutoka nyikani,[#Wim 8:5; Yer 2:2]

Mfano wake ni nguzo za moshi;

Afukizwa manemane na ubani,

Na mavumbi ya manukato yote ya mchuuzi?

7Tazama, ni machela yake Sulemani;

Mashujaa sitini waizunguka,

Wa mashujaa wa Israeli.

8Wote wameshika upanga,

Wamehitimu kupigana;

Kila mtu anao upanga wake pajani

Kwa hofu ya kamsa za usiku.

9Mfalme Sulemani alijitengenezea machela

Ya miti ya Lebanoni;

10Nguzo zake alizitengeneza za fedha,[#Mt 22:37; Yn 13:1,34; Rum 5:8; Efe 3:19; 1 Pet 1:7,8]

Na mgongo wake wa dhahabu,

Kiti chake kimepambwa urujuani,

Gari lake limenakishiwa njumu,

Hiba ya binti za Yerusalemu.

11Tokeni, enyi binti za Sayuni,[#Ufu 11:15; Zab 110:3; Isa 62:5]

Mtazameni Mfalme Sulemani,

Amevaa taji alilovikwa na mamaye,

Siku ya posa yake,

Siku ya furaha ya moyo wake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya