Hekima ya Sulemani 15

Hekima ya Sulemani 15

Faida za kumwabudu Mungu wa kweli

1Lakini Wewe, Mungu wetu, U mwenye neema na kweli, mvumilivu, na katika rehema unaratibisha mambo yote.

2Kwa maana ikiwa sisi twatenda dhambi, tu wako, tukiujua utawala wako; walakini sisi hatutatenda dhambi, tukijua ya kuwa tumehesabiwa kuwa wako;

3kwa sababu kukufahamu Wewe ni haki tupu, na kuujua utawala wako ni shina la kuishi milele.

4Kwa maana hatukupotoshwa kwa sanamu ya ufundi mbaya wa wanadamu, au kazi bure ya wapiga picha, sura ya kitu iliyopakwa rangi mbalimbali;

5hata kuitazama huongoza wajinga kunako tamaa, na shauku yao ni sura isiyo na pumzi ya sanamu isiyo na uhai.

6Wazifanyao ni wapenda maovu, wastahilio matumaini ya namna hiyo, pia na wao wazitamanio, na wao waziabuduo.

Upumbavu wa kuabudu miungu ya sanamu

7Kwa maana mfinyanzi, akikanda udongo laini, huumba kwa kazi ya kuchosha kila chombo kwa matumizi yetu; naam, kwa udongo ule ule huviumba vyombo vyenye utume safi na utume usio safi, naye fundi mwenyewe ndiye mkata neno.

8Tena, akifanya kazi kwa nia mbaya, huumba mungu hafifu katika udongo ule ule, naam, yeye aliyefanyizwa mwenyewe katika udongo hivi karibu, ambaye baada ya muda kitambo atakwenda zake kuurudia ule udongo ambao alitwaliwa ndani yake, atakapotakiwa kuurudisha uhai wake alioazimwa.

9Walakini hujisumbua sana, si kwa sababu nguvu zake zafifia, wala si kwa sababu maisha yake ni mafupi, ila anashindana na mafundi wa dhahabu na fedha, na kuiiga kazi yao wasubuo shaba, naye huona fahari kuwa anafinyanga miigo.

10Moyo wake ni majivu, na taraja lake lina thamani ndogo kuliko ardhi, na uhai wake umepungukiwa na heshima kuliko udongo;

11kwa sababu hakumtambua Yeye aliyemuumba, akampulizia roho ya wepesi katika kutenda, akamtilia pumzi ya nafsi hai.

12Bali aliuhesabu uhai wetu kuwa mchezo, na maisha yetu kuwa tamasha iletayo faida; maana alisema ya kama imempasa mtu apate faida awezavyo, ingawa ni kwa njia mbaya.

13Mtu huyo kuliko watu wengine wote ajua ya kwamba atenda dhambi, mradi katika ule udongo huumba vyombo vilivyo vyepesi kuvunjika, tena na sanamu za miungu.

Upumbavu wa Wamisri waabudu sanamu

14Lakini walikuwa wapumbavu kuliko wote, na wenye roho dhaifu kuliko watoto wachanga, hawa wote, adui za watu wako, waliowatesa mara kwa mara,

15kwa kuwa walihesabu sanamu zote za mataifa kuwa miungu; ambazo hazitumii macho kwa kuona, wala pua kwa kuvuta pumzi, wala masikio kwa kusikia, wala vidole kwa kupapasa, tena miguu yake haifai kitu kwa kutembea.

16Kwa kuwa ni mwanadamu aliyezifanyiza, na mtu ambaye ameazimiwa roho yake aliziumba. Mradi hakuna awezaye, naye ni mwanadamu, kuumba mungu kama mwenyewe, ila, akiwa ni mwenye kufa, afanyiza kitu chenye kufa kwa kazi isiyo halali ya mikono yake.

17Naam, yeye mwenyewe anayo faida kuliko zile aziabuduzo, kwa jinsi yeye kweli alikuwa na uhai, bali hizo hazina kamwe.

Nyoka katika jangwa

18Tena hao pia waviabudu viumbe hai vilivyo makuruhi mno, ambavyo kwa habari ya upungufu wa akili vyachukiza kuliko vyote vingine,

19wala kwa kuvilinganisha na vingine havina uzuri hata mtu avitamani; bali vimeepukana na masifio ya Mungu na baraka yake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya