Zekaria 5

Zekaria 5

Maono ya sita: Gombo linalopuruka

1Basi, nikainua macho yangu tena, nikaona, na tazama, gombo la kitabu lirukalo.

2Akaniuliza, Unaona nini? Nikajibu, Naona gombo la kitabu lirukalo; na urefu wake ni dhiraa ishirini, na upana wake dhiraa kumi.

3Ndipo akaniambia, Hii ndiyo laana itokayo kwenda juu ya uso wa nchi yote; maana kwa hiyo kila aibaye atakatiwa mbali kama ilivyoandikwa upande, na kwa hiyo kila aapaye kwa uongo atakatiliwa mbali kama ilivyo andikwa upande wa pili.[#Mit 3:33; Isa 24:6; Mal 4:6; Gal 3:10,13; Ebr 6:8; #5:3 Maneno ‘kwa uongo’ yameongezwa kutoka kwa mstari wa 4.]

4Nitaituma itokee, asema BWANA wa majeshi, nayo itaingia katika nyumba ya mwizi, na katika nyumba ya yeyote aapaye kwa uongo kwa jina langu; nayo itakaa katika nyumba yake, na kuiteketeza, pamoja na boriti zake na mawe yake.[#Law 19:12; 14:45; Mt 5:33-36; Yak 5:12]

Maono ya saba: Mwanamke akiwa katika kikapu

5Ndipo yule malaika aliyesema nami akatokea, akaniambia, Inua macho yako sasa, uone ni kitu gani kitokeacho.

6Nikasema, Ni kitu gani? Akasema, Kitu hiki ni efa itokeayo. Tena akasema, Huu ndio uovu wao katika nchi hii yote;

7na tazama, kifuniko cha risasi kiliinuliwa; na tazama, mlikuwa na mwanamke ndani ya kikapu.[#5:7 Katika Kiebrania ni ‘talanta’.]

8Akasema, Huyu ni Uovu; akamsukuma ndani ya kile kikapu; akalitupa lile jiwe la risasi juu ya mdomo wa ile efa.

9Ndipo nikainua macho yangu, nikaona, na tazama, wanawake wawili walitokea, nao upepo ulikuwa katika mabawa yao; na mabawa yao yalikuwa kama mabawa ya korongo; wakaiinua ile efa kati ya dunia na mbingu.

10Ndipo nikamwambia yule malaika aliyesema nami, Hawa wanaipeleka wapi efa hii?

11Akaniambia, Wanakwenda kumjengea nyumba katika nchi ya Shinari; tena ikiisha kutengenezwa, atawekwa huko mahali pake mwenyewe.[#Yer 29:5; #5:11 Ni jina la zamani la Babeli.]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya