1 Nya 10

1 Nya 10

Kifo cha Sauli na Wanawe

1Basi Wafilisti wakapigana juu ya Israeli; nao watu wa Israeli wakakimbia mbele ya Wafilisti, wakaanguka wameuawa katika mlima Gilboa.[#1 Sam 7:7; 13:5; 31:1]

2Nao Wafilisti wakamfuatia sana Sauli na wanawe; Wafilisti wakawaua Yonathani, na Abinadabu, na Malkishua, wana wa Sauli.

3Tena vita vilikuwa vikali sana juu ya Sauli, na wapiga upinde wakampata; hata akafadhaika sana kwa sababu ya wapiga upinde.

4Ndipo Sauli akamwambia yule mchukua silaha zake, Futa upanga wako, unichome nao, wasije watu hawa wasiotahiriwa wakanisimanga. Lakini huyo mchukua silaha zake akakataa; kwa sababu aliogopa sana. Basi Sauli akautwaa upanga wake, akauangukia.[#Amu 16:21]

5Na mchukua silaha zake alipoona ya kuwa Sauli amekufa, yeye naye akauangukia upanga wake, akafa.

6Hivyo Sauli akafa, na wanawe watatu; na nyumba yake yote wakafa pamoja.

7Kisha watu wote wa Israeli, waliokuwa huko bondeni, walipoona ya kuwa wamekimbia, na ya kuwa Sauli na wanawe wamekufa, wakaiacha miji yao, wakakimbia; nao Wafilisti wakaenda wakakaa humo.

8Hata ikawa siku ya pili yake Wafilisti walipokwenda kuwateka nyara hao waliouawa, walimwona Sauli na wanawe wameanguka juu ya mlima Gilboa.

9Wakamvua mavazi, wakamtwalia kichwa, na silaha zake, kisha wakapeleka wajumbe kwenda nchi ya Wafilisti pande zote, ili kutangaza habari kwa sanamu zao, na kwa watu.

10Wakaziweka silaha zake nyumbani mwa miungu yao, wakakikaza kichwa chake nyumbani mwa Dagoni.[#1 Sam 31:10; Isa 48:5]

11Na watu wote wa Yabesh-gileadi waliposikia hayo yote Wafilisti waliyomtenda Sauli,

12wakainuka mashujaa wote, wakautwaa mwili wake Sauli, na miili ya wanawe, wakaileta Yabeshi, wakaizika mifupa yao chini ya mwaloni huko Yabeshi, nao wakafunga muda wa siku saba.

13Basi Sauli alikufa kwa sababu ya kosa lake alilomkosa BWANA, kwa sababu ya neno la BWANA, asilolishika; na tena kwa kutaka shauri kwa mwenye pepo wa utambuzi, aulize kwake,[#1 Sam 13:13; 15:23; 1 Fal 18:18; 2 Nya 16:9; Kut 22:18; Law 19:31; 20:27; Kum 18:11; 2 Fal 21:6; Isa 8:19; 1 Sam 28:7]

14asiulize kwa BWANA; kwa hiyo akamwua, na ufalme akamgeuzia Daudi, mwana wa Yese.[#1 Sam 13:14; 15:28]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania