1 Nya 26

Mabawabu wa Hekalu

1Kwa zamu zao mabawabu; wa Wakora; Meshelemia mwana wa Kore, wa wana wa Ebiasafu.[#Hes 16:1,2; 26:9-11; 1 Nya 9:17; 15:18; 2 Nya 23:19; Yud 1:11; 1 Nya 6:39]

2Naye Meshelemia alikuwa na wana; Zekaria mzaliwa wa kwanza, Yediaeli wa pili, Zebadia wa tatu, Yathnieli wa nne;

3Elamu wa tano, Yohana wa sita, Elioenai wa saba.

4Naye Obed-edomu alikuwa na wana; Shemaya mzaliwa wa kwanza, Yehozabadi wa pili, Yoa wa tatu, na Sakari wa nne, na Nethaneli wa tano;

5Amieli wa sita, Isakari wa saba, Peulethai wa nane; kwa jinsi Mungu alivyombariki.[#1 Nya 13:14; Mwa 33:5; Zab 127:3]

6Naye mwanawe Shemaya akazaliwa wana, waliomiliki juu ya mbari ya baba yao; kwa kuwa walikuwa waume mashujaa.

7Wana wa Shemaya; Othni, na Refaeli, na Obedi, na Elzabadi, nduguze walikuwa mashujaa, Elihu, na Semakia.

8Hao wote walikuwa wana wa Obed-edomu; wao na wana wao na ndugu zao, watu hodari wawezao huo utumishi; watu wa Obed-edomu sitini na wawili.

9Naye Meshelemia alikuwa na wana na nduguze, watu mashujaa, kumi na wanane.

10Hosa naye, wa wana wa Merari, alikuwa na wana; Shimri mkuu wao; (kwani ajapokuwa yeye si mzaliwa wa kwanza, babaye alimweka mkuu);[#1 Nya 16:38; Mwa 4:7; 49:3; Kum 21:17; 1 Nya 5:1]

11Hilkia wa pili, Tebalia wa tatu, Zekaria wa nne; wana wote wa Hosa pamoja na nduguze walikuwa watu kumi na watatu.

12Katika hao zilikuwa zamu za mabawabu, yaani, katika hao wakuu, wenye ulinzi sawasawa na ndugu zao, wa kutumika katika nyumba ya BWANA.

13Nao wakatupiwa kura kwa ajili ya kila lango, wadogo sawasawa na wakubwa, kwa kadiri ya mbari za baba zao.[#Yos 18:10; 1 Nya 25:8; 24:5; Mit 18:18; Yon 1:7; Mdo 1:26; 10:34; Gal 3:28; Kol 3:11]

14Kura ya mashariki ya lango ikamwangukia Meshelemia. Ndipo wakamtupia kura Zekaria mwanawe, mshauri mwenye busara; na kura yake ikamtokea ya kaskazini.

15Ya Obed-edomu ya kusini; na ya wanawe nyumba ya akiba.

16Ya Shupimu na Hosa upande wa magharibi, langoni pa Shalekethi, hapo penye daraja ya kupandia, ulinzi kwa ulinzi.[#1 Fal 10:5; 1 Nya 24:31; 25:8; 2 Nya 9:4; Neh 12:24]

17Upande wa mashariki walikuwapo Walawi sita, kaskazini wanne kila siku, kusini wanne kila siku, na wa nyumba ya akiba wawili wawili.

18Penye Parbari upande wa magharibi, walikuwapo wanne darajani, na wawili huko Parbari.

19Hizo ndizo zamu za mabawabu; wa wana wa Wakora, na wa wana wa Merari.

Watunza Hazina, Maofisa na Waamuzi

20Na katika Walawi; Ahia alikuwa juu ya hazina za nyumba ya Mungu, na juu ya hazina za vitu vilivyowekwa wakfu.[#Kum 12:6; 1 Fal 7:51; 14:26; 1 Nya 9:26-29; 22:14-16; Mal 3:10; 2 Nya 31:11,12]

21Wana wa Ladani; wana wa Wagershoni waliokuwa wa Ladani; wakuu wa mbari za mababa waliokuwa wa Ladani, Mgershoni; Yehieli.[#1 Nya 6:17; 23:8]

22Wana wa Yehieli; Zethamu, na Yoeli nduguye, juu ya hazina za nyumba ya BWANA.

23Wa Waamramu, wa Waishari, wa Wahebroni, wa Wauzieli;[#Kut 6:18; Hes 3:19; 1 Nya 23:12]

24na Shebueli, mwana wa Gershomu, mwana wa Musa, alikuwa mtawala hazina zote.[#1 Nya 23:16; 24:20]

25Na nduguze; wa Eliezeri, Rehabia mwanawe, na Ishia mwanawe, na Yoramu mwanawe, na Zikri mwanawe, na Shelomothi mwanawe.[#1 Nya 23:18; 24:22]

26Huyo Shelomothi na ndugu zake walikuwa juu ya hazina zote za vitu vilivyowekwa wakfu, alivyoviweka wakfu mfalme Daudi, na hao wakuu wa mbari za mababa, na maakida wa maelfu na wa mamia, na maakida wa jeshi.

27Katika nyara zilizopatikana vitani, waliweka wakfu sehemu, ili kuitengeneza nyumba ya BWANA.[#Hes 31:50; Yos 6:19,24; 1 Nya 22:14-16; 2 Nya 15:11,18; 2 Fal 12:14; 22:4,5; Neh 10:32]

28Na vyote alivyoviweka wakfu Samweli mwonaji, na Sauli mwana wa Kishi, na Abneri mwana wa Neri, na Yoabu mwana wa Seruya; na mtu ye yote aliyekiweka wakfu kitu cho chote, kilikuwa chini ya mkono wa Shelomothi na nduguze.[#1 Sam 9:9]

29Katika Waishari, Kenania na wanawe walikuwa kwa ajili ya kazi ya nje juu ya Israeli, kuwa maakida na makadhi.[#Kum 1:16; 16:18; 1 Nya 23:4; 2 Nya 19:8-11]

30Katika Wahebroni, Hashabia na nduguze, mashujaa, elfu na mia saba, walikuwa na usimamizi juu ya Israeli ng’ambo ya Yordani upande wa magharibi; kwa ajili ya kazi zote za BWANA, na kwa utumishi wa mfalme.

31Katika Wahebroni Yeria alikuwa mkuu, yaani, wa hao Wahebroni kwa kufuata vizazi vyao kwa mbari za mababa. Katika mwaka arobaini wa kutawala kwake Daudi wakatafutwa, wakaonekana huko Yazeri ya Gileadi miongoni mwao waume mashujaa.[#1 Nya 23:19; 2 Sam 5:4; 1 Fal 2:11; 1 Nya 29:27; Hes 32:1,3,35; Yos 21:39; Isa 16:9; Yer 48:32]

32Na nduguze, mashujaa, walikuwa elfu mbili na mia saba, wakuu wa mbari za mababa, ambao mfalme Daudi aliwaweka wawe wasimamizi juu ya Wareubeni, na Wagadi, na nusu kabila ya Wamanase, kwa ajili ya kila neno lililomhusu Mungu, na kwa mambo ya mfalme.[#2 Nya 19:11]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania