The chat will start when you send the first message.
1Lile lililokuwako tangu mwanzo, tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama, na mikono yetu ikalipapasa, kwa habari ya Neno la uzima;[#Yn 1:1,14]
2(na uzima huo ulidhihirika, nasi tumeona, tena twashuhudia, na kuwahubiri ninyi ule uzima wa milele, uliokuwa kwa Baba, ukadhihirika kwetu);[#Yn 1:4,14]
3hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo.
4Na haya twayaandika, ili furaha yetu itimizwe.[#Yn 15:11; 16:24]
5Na hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake, na kuihubiri kwenu, ya kwamba Mungu ni nuru, wala giza lo lote hamna ndani yake.[#Yak 1:17]
6Tukisema ya kwamba twashirikiana naye, tena tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli;[#1 Yoh 2:4; Yn 3:21]
7bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.[#Ebr 9:14; Ufu 1:5; 7:14]
8Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.
9Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.[#Mit 28:13]
10Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu.