1 Pet 5

1 Pet 5

Kuchunga Kundi la Mungu

1Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye;[#2 Yoh 1:1; 3 Yoh 1:1; Rum 8:17; Ufu 1:9]

2lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo.[#Yn 10:12; 21:15-17; Flm 1:14; Tit 1:11; Mdo 20:28; 1 Tim 3:2-7]

3Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi.[#2 Kor 1:24; Tit 2:7; Flp 3:17; 1 The 1:7]

4Na Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka.[#1 Pet 2:25; Ebr 13:20; 1 Kor 9:25; 2 Tim 4:8]

5Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.[#Mit 3:34; Efe 5:21; Mt 23:12; Yn 13:4,14; Yak 4:6]

6Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;[#Mt 23:12; Lk 14:11; 18:14; Ayu 22:29; Yak 4:10]

7huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.[#Zab 55:22; Mt 6:25; Flp 4:6]

8Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.[#1 The 5:6; Lk 18:3; Yak 4:7]

9Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani.[#Efe 6:11-13]

10Na Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo, mkiisha kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na kuwatia nguvu.[#1 Pet 1:6; 1 The 2:12]

11Uweza una yeye hata milele na milele. Amina.

Salamu za Mwisho na Baraka

12Kwa mkono wa Silwano, ndugu mwaminifu kama nionavyo, nimewaandikia kwa maneno machache, kuonya na kushuhudia ya kuwa hii ndiyo neema ya kweli ya Mungu. Simameni imara katika hiyo.[#Mdo 15:22,40; Ebr 13:22]

13Mwenzenu mteule hapa Babeli awasalimu, na Marko mwanangu.[#Mdo 12:12,25; 13:13; 15:37-39; Kol 4:10; Flm 1:24; 2 Tim 4:11]

14Salimianeni kwa busu la upendo.[#1 Kor 16:20]

Amani na iwe kwenu nyote, mlio katika Kristo. Amina.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania