The chat will start when you send the first message.
1Jitunze mguu wako uendapo nyumbani kwa Mungu;[#Kut 3:5; Yos 5:15; Zab 89:7; Isa 1:12; 1 Sam 15:22; Zab 50:8; Mit 15:8; Hos 6:6]
Maana ni heri kukaribia ili usikie,
Kuliko kutoa kafara ya wapumbavu;
Ambao hawajui kuwa wafanya mabaya.
2Usiseme maneno ya ujinga kwa kinywa chako, wala moyo wako usiwe na haraka kunena mbele za Mungu; kwa maana, Mungu yuko mbinguni, na wewe upo chini, Kwa hiyo maneno yako na yawe machache.[#Zab 39:1; Mit 10:19; Mt 6:7]
3Kwa maana ndoto huja kwa sababu ya shughuli nyingi; na sauti ya mpumbavu kwa njia ya wingi wa maneno.
4Wewe ukimwekea Mungu nadhiri, usikawie kuiondoa; kwa kuwa yeye hawi radhi na wapumbavu; basi, uiondoe hiyo uliyoiweka nadhiri.[#Zab 66:13-14; Mwa 28:20; Hes 30:2; Zab 50:14; Isa 19:21; Yon 2:9]
5Ni afadhali usiweke nadhiri,[#Mit 20:25; Mdo 5:4]
Kuliko kuiweka usiiondoe.
6Usikiache kinywa chako kuukosesha mwili wako; wala usiseme mbele ya huyo malaika ya kwamba umepitiliwa; kwani Mungu akukasirikie sauti yako, na kuiharibu kazi ya mikono yako?[#1 Kor 11:10; 1 Tim 5:21]
7Maana ndivyo ilivyo katika habari za wingi wa ndoto, na ubatili, na maneno mengi; walakini wewe umche Mungu.[#Kum 10:12; Mit 23:17; Mhu 12:13; Ebr 12:28]
8Ujapokuwa unaona maskini kuonewa, na hukumu na haki kuondolewa kwa jeuri katika jimbo, usilistaajabie jambo hilo; kwa sababu,[#Mhu 3:16; Zab 12:5; Isa 57:15]
Aliye juu kuliko walio juu huangalia;
Tena wako walio juu kupita hao.
9Lakini, pamoja na hayo, manufaa ya nchi kwa kila njia ni mfalme anayejibidiisha kwa ajili ya shamba.
10Apendaye fedha hatashiba fedha,
Wala apendaye wingi hatashiba nyongeza.
Hayo pia ni ubatili.
11Mali yakiongezeka, hao walao nao waongezeka na mwenyewe hufaidiwa nini, ila kuyatazama kwa macho yake tu?
12Usingizi wake kibarua ni mtamu, kwamba amekula kidogo, au kwamba amekula kingi; lakini kushiba kwake tajiri hakumwachi kulala usingizi.
13Kuna na balaa mbaya sana niliyoiona chini ya jua, nayo ni hii, mali alizoziweka mwenyewe kwa kujinyima;[#Mhu 6:1]
14na mali hizo zimepotea kwa bahati mbaya; naye akiwa amezaa mwana, hamna kitu mkononi mwake.
15Alivyotoka tumboni mwa mamaye, atakwenda tena tupu-tupu kama alivyokuja; asichume kitu cho chote kwa ajili ya kazi yake, hata akichukue mkononi mwake.[#Ayu 1:21; Zab 49:17; 1 Tim 6:7]
16Hiyo ndiyo balaa mbaya sana, ya kwamba kama vile alivyokuja, vivyo hivyo atakwenda zake; naye amefaidiwa nini mwenye kujitaabisha kwa ajili ya upepo?[#Mhu 1:3; Mit 11:29]
17Siku zake zote hula gizani, mwenye fadhaa nyingi, mwenye ugonjwa na uchungu.[#Zab 127:2]
18Tazama, mimi niliyoyaona kuwa ndiyo mema na ya kufaa, ni mtu kula na kunywa, na kujiburudisha kwa mema katika kazi yake yote anayoifanya chini ya jua, siku zote za maisha yake alizopewa na Mungu; maana hilo ndilo fungu lake.
19Tena, kwa habari za kila mwanadamu, ambaye Mungu amempa mali na ukwasi, akamwezesha kula katika hizo, na kuipokea sehemu yake, na kuifurahia amali yake; hiyo ndiyo karama ya Mungu.
20Kwa kuwa mtu hatazikumbuka mno siku za maisha yake; kwa sababu Mungu humtakabali katika furaha ya moyo wake.[#Kut 23:25]