Est 3

Est 3

Hamani Apanga Kuwaangamiza Wayahudi

1Baada ya hayo mfalme Ahasuero alimwongezea cheo Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, akampandisha, akamwekea kiti chake juu ya maakida wote waliokuwapo pamoja naye.[#Hes 24:7; 1 Sam 15:8]

2Nao watumishi wote wa mfalme, walioketi mlangoni pa mfalme, wakainama na kumsujudia Hamani, maana ndivyo alivyoamuru mfalme kwa habari zake. Bali Mordekai hakuinama, wala kumsujudia.[#Est 2:19; Mwa 41:42; Kum 25:19; Flp 2:10; Kut 1:17; Zab 15:4]

3Basi watumishi wa mfalme walioketi mlangoni pa mfalme wakamwambia Mordekai, Mbona wewe waihalifu amri ya mfalme?

4Ikawa, waliposema naye kila siku asiwasikilize, wakamwarifu Hamani, ili kuona kama mambo yake Mordekai yatasimama; maana alikuwa amewaambia ya kuwa yeye ni Myahudi.

5Hata Hamani alipoona ya kwamba Mordekai hainami wala kumsujudia, alighadhibika sana.[#Est 5:9; 1:12; Ayu 5:2; Mit 12:16; Dan 3:19]

6Akaona si shani kumtia mikono Mordekai peke yake; maana wamemjulisha kabila yake Mordekai; kwa hiyo Hamani alitaka kuwaangamiza Wayahudi wote waliokuwa wakikaa katika ufalme wote mzima wa Ahasuero, yaani, watu wake Mordekai.[#Zab 83:4]

7Basi mwezi wa kwanza, ndio mwezi wa Nisani, mwaka wa kumi na mbili wa mfalme Ahasuero, wakapiga Puri, yaani kura, mbele yake Hamani; siku kwa siku, na mwezi kwa mwezi, hata mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari.[#Est 9:24; Mt 27:35; Mdo 1:26]

8Basi Hamani akamwambia mfalme Ahasuero, Kuna taifa moja waliotawanyika na kukaa mahali mahali katikati ya mataifa walioko katika majimbo yote ya ufalme wako. Nao sheria zao zimefarakana na sheria za kila taifa; wala hawazishiki amri za mfalme; kwa hiyo haimpasi mfalme kuchukuliana nao.[#Ezr 4:13; Mdo 16:20]

9Basi, mfalme akiona vema, na iandikwe kwamba waangamizwe; nami nitalipa talanta kumi elfu za fedha mikononi mwao watakaosimamia shughuli hiyo, waziweke katika hazina ya mfalme.

10Ndipo mfalme alipoivua pete yake mkononi, akampa Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, adui ya Wayahudi.[#Mwa 41:42; Est 8:2,8]

11Kisha mfalme akamwambia Hamani, Hiyo fedha umepewa, na watu pia, fanya uonavyo vema.

12Basi, waandishi wa mfalme wakaitwa, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kwanza; na barua zikaandikwa, kama vile Hamani alivyoagiza vyote, kwa maakida wa mfalme, na maliwali waliokuwa juu ya kila jimbo, na wakuu wa kila taifa; kila jimbo kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake; zikaandikwa kwa jinsi la mfalme Ahasuero, na kutiwa muhuri kwa pete yake.[#Est 8:8-10; 1:22; 1 Fal 21:8; Dan 6:8]

13Barua zikapelekwa kwa mikono ya matarishi mpaka majimbo yote ya mfalme kuwaangamiza Wayahudi wote, na kuwaua, na kuwafisha, vijana kwa wazee, watoto wachanga na wanawake pia, siku moja, yaani, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili ndio mwezi wa Adari; na kuyachukua mali yao kuwa nyara.[#Est 8:10-12; Rum 3:15; Isa 10:6]

14Nakili ya andiko, ya kupigwa mbiu katika kila jimbo, ilitangazwa kwa mataifa yote wawe tayari siku ile ile.[#Est 8:13,14]

15Matarishi wakaondoka wakaenda haraka kwa amri ya mfalme; kukapigwa mbiu huko Shushani ngomeni. Mfalme na Hamani wakaketi ili kunywa divai; bali mji wa Shushani ukafadhaika.[#Mwa 37:24,25; Zab 14:4; Mit 30:20-22; Hos 7:3; Amo 6:6; Mt 14:6; Est 8:15; Mit 29:2]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania