The chat will start when you send the first message.
1Wakati nitakapo kumponya Israeli, ndipo yafunuliwapo maovu ya Efraimu, na ubaya wa Samaria; maana wanatenda uongo, na mwivi huvunja nyumba za watu, na kundi la wanyang’anyi hushambulia nje.
2Wala hawafikiri mioyoni mwao ya kwamba naukumbuka uovu wao wote; sasa matendo yao wenyewe yamewazunguka pande zote; yako mbele za uso wangu.[#Mit 5:22; Zab 90:8]
3Humfurahisha mfalme kwa uovu wao, na wakuu wao kwa uongo wao.[#Rum 1:32]
4Hao wote ni wazinzi; wamekuwa kama tanuu iliyotiwa moto na mwokaji; huacha kuuchochea moto, tangu kuukanda unga hata umekwisha kutiwa chachu.
5Sikukuu ya mfalme wetu, wakuu walijitapisha kwa ukali wa divai; alinyosha mkono wake pamoja na wenye mzaha.
6Maana wamefanya moyo wao kuwa tayari kama tanuu, wakati waoteapo; hasira yao hulala usiku kucha; asubuhi yawaka kama moto utoao miali.
7Wote wamepata moto kama tanuu, nao hula makadhi wao; wafalme wao wote wameanguka; hakuna hata mmoja wao aniitaye mimi.[#2 Fal 15:10; Isa 9:13]
8Efraimu ajichanganya na mataifa; Efraimu ni mkate usiogeuzwa.[#Zab 106:35]
9Wageni wamekula nguvu zake, naye hana habari; naam, nywele za mvi zimeonekana huko na huko juu yake, naye hana habari.
10Na kiburi cha Israeli chamshuhudia mbele ya uso wake; ila hata hivyo hawakumrudia BWANA, Mungu wao, wala hawakumtafuta kwa ajili ya hayo yote.
11Naye Efraimu amekuwa kama njiwa mpumbavu, asiye na fahamu; humwita Misri, huenda Ashuru.
12Watakapokwenda nitatandika wavu wangu juu yao; nitawashusha kama ndege wa angani; nitawarudi, kama vile mkutano wao ulivyosikia.[#Law 26:14]
13Ole wao! Kwa kuwa wamenikimbia; uharibifu na uwapate! Kwa kuwa wameniasi; ingawa ninataka kuwakomboa, hata hivyo wamenena uongo juu yangu.
14Wala hawakunililia kwa moyo, lakini wanalalamika vitandani mwao; hujikutanisha ili kupata nafaka na divai; huniasi mimi.[#Ayu 35:9; Zab 78:34-37; Isa 29:13; Yer 3:10]
15Ingawa nimewafundisha na kuwatia nguvu mikono yao, hata hivyo hukusudia udhalimu juu yangu.
16Wao hurudi, lakini si kwake Aliye juu; wamekuwa kama upinde usiotumainika; wakuu wao wataanguka kwa upanga, kwa sababu ya jeuri ya ndimi zao; jambo hili litakuwa kwao sababu ya kuchekwa katika nchi ya Misri.[#Zab 73:9]