Hos 8

Hos 8

Uasi wa Israeli

1Tia baragumu kinywani mwako. Kama tai, anakuja juu ya nyumba ya BWANA; kwa sababu wamelihalifu agano langu, wameiasi sheria yangu.[#Yer 4:13; Hab 1:8]

2Watanililia, Mungu wangu, sisi Israeli tunakujua.[#Zab 78:34; Mt 7:21]

3Israeli ameyatupa yaliyo mema; adui watamfuatia.

4Wamesimamisha wafalme, lakini si kwa shauri langu; wamejifanyia wakuu, lakini nalikuwa sina habari; kwa fedha yao na dhahabu yao wamejifanyizia sanamu, kusudi wakatiliwe mbali.[#1 Fal 12:16-20; 2 Fal 15:13,17,25]

5Amemtupa ndama yako, Ee Samaria; hasira yangu imewaka juu yao; siku ngapi zitapita kabla ya hao kupata hali isiyo na hatia?[#Yer 13:27]

6Maana katika Israeli kimetokea hata na kitu hiki; fundi ndiye aliyekifanya, nacho si mungu kamwe; naam, ndama ya Samaria itavunjika vipande vipande.

7Kwa maana wao hupanda upepo, nao watavuna tufani; nafaka haina bua; machipuko yake hayatoi masuke; hata ikiwa yatoa, wageni watayameza.

8Israeli amemezwa; sasa wamo miongoni mwa mataifa kama chombo kisichopendeza.

9Kwa maana wamekwea kwenda Ashuru, mfano wa punda wa mwituni aliye peke yake; Efraimu ameajiri wapenzi.[#2 Fal 15:19]

10Naam, ijapokuwa waajiri kati ya mataifa, sasa nitawakusanya; nao wanaanza kupunguka kwa sababu ya mzigo wa mfalme wa wakuu.[#Isa 10:8; Eze 26:7; Dan 2:37]

11Kwa kuwa Efraimu ameongeza madhabahu kwa dhambi, madhabahu zimekuwa dhambi kwake.

12Nijapomwandikia sheria yangu katika amri elfu kumi, zimehesabiwa kuwa ni kitu kigeni.[#Kum 4:6; Neh 9:13,14; Mit 22:20; Rum 3:1,2; Ayu 21:14]

13Kwa habari za dhabihu za matoleo yangu, hutoa dhabihu ya nyama na kuila; lakini BWANA hawakubali; sasa ataukumbuka uovu wao, na kuwapatiliza dhambi zao; watarudi kwenda Misri.

14Maana Israeli amemsahau Muumba wake, naye amejenga nyumba za enzi; na Yuda ameongeza miji yenye maboma; lakini nitapeleka moto juu ya miji yake, nao utaziteketeza ngome zake.[#1 Fal 12:31]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania