Yak 1

Yak 1

Salamu

1Yakobo, mtumwa wa Mungu, na wa Bwana Yesu Kristo, kwa kabila kumi na mbili waliotawanyika; salamu.[#Mt 13:55; Mk 6:3; Mdo 15:13,23; 1 Pet 1:1; Gal 1:19]

Imani na Hekima

2Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali;[#Rum 5:3-5; 1 Pet 1:6]

3mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi.[#1 Pet 1:7]

4Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno.

5Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa.[#Mit 2:3-6]

6Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku.[#Mk 11:24]

7Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana.

8Mtu wa nia mbili husita-sita katika njia zake zote.

Umaskini na Utajiri

9Lakini ndugu asiye na cheo na afurahi kwa kuwa ametukuzwa;[#Yak 2:5]

10bali tajiri kwa kuwa ameshushwa; kwa maana kama ua la majani atatoweka.[#Isa 40:6-7; 1 Pet 1:24]

11Maana jua huchomoza kwa hari, huyakausha majani; ua lake huanguka, uzuri wa umbo lake hupotea; vivyo hivyo naye tajiri atanyauka katika njia zake.

Majaribu na Mateso

12Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, Bwana aliyowaahidia wampendao.[#Dan 12:12; 2 Tim 4:8; 1 Pet 5:4; 1 Kor 9:25; Ufu 2:10]

13Mtu ajaribiwapo, asiseme, Ninajaribiwa na Mungu; maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu, wala yeye mwenyewe hamjaribu mtu.

14Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa.[#Rum 7:7-10]

15Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti.

16Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike.

17Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeuka-geuka.[#1 Yoh 1:5; Mt 7:11]

18Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake.[#Yn 1:13; 1 Pet 1:23]

Kusikia na Kutenda Neno

19Hayo mnajua, ndugu zangu wapenzi. Basi kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema; wala kukasirika;[#Mhu 7:9]

20kwa maana hasira ya mwanadamu haiitendi haki ya Mungu.[#Efe 4:26]

21Kwa hiyo wekeeni mbali uchafu wote na ubaya uzidio, na kupokea kwa upole neno lile lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu.[#Kol 3:8; 1 Pet 2:1]

22Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.[#Mt 7:26; Rum 2:13]

23Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo.

24Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.

25Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake.[#Yak 2:12; Rum 8:2; Yn 13:17]

26Mtu akidhani ya kuwa anayo dini, wala hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hali akijidanganya moyo wake, dini yake mtu huyo haifai.[#Zab 34:13]

27Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania