Ayu 2

Ayu 2

Pigo kwa Afya ya Ayubu

1Tena kulikuwa na siku hao wana wa Mungu walipokwenda kujihudhurisha mbele za BWANA, Shetani naye akaenda kati yao, ili kujihudhurisha mbele za BWANA.

2BWANA akamwuliza Shetani, Umetoka wapi? Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo.

3BWANA akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu; naye hata sasa anashikamana na utimilifu wake, ujapokuwa ulinichochea juu yake, ili nimwangamize pasipokuwa na sababu.[#Ayu 27:5,6; Yak 1:12; 1 Pet 1:7; Mwa 22:1; Mt 7:11; Yn 9:2]

4Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Ngozi kwa ngozi, naam, yote aliyo nayo mtu atayatoa kwa ajili ya uhai wake.

5Lakini sasa nyosha mkono wako, uuguse mfupa wake na nyama yake, naye atakukufuru mbele za uso wako.[#Ayu 19:20; Zab 32:3,4]

6BWANA akamwambia Shetani, Tazama, yeye yumo mkononi mwako; lakini tunza tu uhai wake.

7Basi Shetani akatoka mbele za uso wa BWANA, akampiga Ayubu na majipu mabaya tangu wayo wa mguu hata utosi wa kichwa.

8Naye akashika kigae cha kujikunia; akaketi majivuni.[#2 Sam 13:19; Ayu 42:6; Mt 11:21]

9Ndipo mkewe akamwambia, Je! Wewe hata sasa washikamana na utimilifu wako? Umkufuru Mungu, ukafe.[#Mwa 3:6; 2 Fal 6:33; Mal 3:14; Ayu 21:15]

10Lakini yeye akamwambia, Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! Tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya? Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo yake.[#2 Sam 19:28; Ayu 1:21; Omb 3:38-41; Yn 18:11; Rum 12:12; Ebr 12:9-11; Zab 39:1; Yak 1:12]

Marafiki Watatu wa Ayubu

11Basi ikawa hao rafikize Ayubu watatu walipopata habari ya mabaya hayo yote yaliyomfikilia, wakaja kila mtu kutoka mahali pake; nao ni Elifazi Mtemani, na Bildadi Mshuhi, na Sofari Mnaamathi; wakapatana pamoja ili waende kumlilia Ayubu na kumtuliza moyo.[#Mwa 36:11; Yer 49:7; Mwa 25:2; Ayu 42:11; Rum 12:15]

12Basi walipovua macho yao, nao wakali mbali, wasimtambue, wakainua sauti zao na kulia; kila mmoja akararua joho yake, wakarusha mavumbi juu ya vichwa vyao kuelekea mbinguni.[#Neh 9:1; Omb 2:10]

13Kisha wakaketi nchi pamoja naye muda wa siku saba, mchana na usiku, wala hapana mmoja aliyenena naye neno lo lote; kwa maana waliona ya kuwa mashaka yake aliyo nayo ni makuu mno.[#Mwa 50:12]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania