Ayu 24

Ayu 24

Ayubu Alalamikia Udhalimu Duniani

1Mbona nyakati zisiwekwe na Mwenyezi?[#Mdo 1:7]

Na hao wamjuao mbona hawazioni siku zake?

2Wako waziondoao alama za mipaka;[#Kum 19:14]

Huyachukua makundi kwa jeuri na kuyalisha.

3Humfukuza punda wake asiye baba,[#Kum 24:6,10,12,17]

Humtwaa rehani ng’ombe wake mwanamke mjane.

4Humgeuza mhitaji aiache njia;[#Mit 28:28]

Maskini wa nchi hujificha pamoja.

5Tazama, kama punda-mwitu jangwani

Wao hutoka kwenda kazini mwao, wakitafuta chakula kwa bidii;

Jangwa huwapa chakula cha watoto wao.

6Hukata nafaka zao mashambani;

Na kuokota zabibu za waovu.

7Hujilaza usiku kucha uchi pasipo nguo,[#Kut 22:26; Kum 24:12; Isa 58:7]

Wala hawana cha kujifunika baridi.

8Hutota kwa manyunyo ya milimani,[#Omb 4:5]

Na kuambatana na jabali kwa kukosa sitara,

9Wako wamwondoao matitini kwa nguvu huyo asiye na baba,

Na kutwaa rehani kwa maskini;

10Hata wazunguke uchi pasipo mavazi,

Nao wakiwa na njaa huchukua miganda;

11Hushindika mafuta ndani ya makuta ya watu hao;

Wakanyaga mashinikizo, nao wana kiu.

12Watu huugua toka mji ulio na watu wengi,[#Mhu 8:11]

Na roho yake aliyejeruhiwa hupiga ukelele;

Wala Mungu hauangalii upumbavu.

13Hawa ni katika hao waliouasi mwanga;

Hawazijui njia zake,

Wala hawakai katika mapito yake.

14Mwuaji huamka asubuhi kukipambauka, huwaua maskini na wahitaji;

Tena wakati wa usiku yu kama mwivi.

15Tena jicho lake mzinifu hungojea wakati wa giza-giza,

Akisema, Hapana jicho litakaloniona;

Naye huuficha uso wake.

16Wao hutoboa nyumba gizani;[#Yn 3:20]

Hujifungia ndani wakati wa mchana;

Hawaujui mwanga.

17Kwani asubuhi kwao wote ni kama giza tupu;

Kwani wao wavijua vitisho vya hiyo giza tupu.

18Mwasema, Yeye ni mwepesi juu ya uso wa gharika;

Sehemu yao inalaaniwa duniani;

Hageuki kwenda njia ya mizabibuni.

19Chaka na hari hukausha maji ya theluji;

Kuzimu nako hao ambao wamefanya dhambi.

20Tumbo lililomzaa litamsahau; buu litamla na kuona tamu;[#Mit 10:7]

Hatakumbukwa tena;

Na udhalimu utavunjwa kama mti.

21Naam, yeye huwala walio tasa wasiozaa;

Wala hamtendei mema mwanamke mjane.

22Lakini Mungu huwadumisha wenye uwezo kwa nguvu zake;

Huinuka, wasiokuwa na tumaini la kuishi.

23Huwapa kuwa na salama, nao wapumzika kwayo;

Na macho yake ya juu ya njia zao.

24Wao wametukuzwa; lakini kitambo kidogo hutoweka;[#Zab 37:35,36]

Naam, hushushwa, na kuondolewa njiani kama wengine wote,

Nao hukatwa kama vile masuke ya ngano.

25Na kama sivyo sasa, ni nani atakayenihukumu kuwa ni mwongo,

Na kuyafanya maneno yangu kuwa si kitu?

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania