Mt 19

Mt 19

Mafundisho kuhusu Talaka

1Ikawa Yesu alipomaliza maneno hayo, akatoka Galilaya akafika mipaka ya Uyahudi, ng’ambo ya Yordani.[#Mk 10:1-12; #Mt 7:28; 11:1; 13:53; 26:1]

2Makutano mengi wakamfuata, akawaponya huko.

3Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamjaribu, wakimwambia, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe kwa kila sababu?[#Mt 5:31,32]

4Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke,[#Mwa 1:27; 5:2]

5akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja?[#Mwa 2:24; Efe 5:31]

6Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.[#1 Kor 7:10,11]

7Wakamwambia, Jinsi gani basi Musa aliamuru kumpa hati ya talaka, na kumwacha?[#Kum 24:1-4; Mt 5:31]

8Akawaambia, Musa, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi.

9Nami nawaambia ninyi, Kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini.[#Mt 5:32; 1 Kor 7:10-11; Lk 16:18]

10Wanafunzi wake wakamwambia, Mambo ya mtu na mkewe yakiwa hivyo, haifai kuoa.

11Lakini yeye akawaambia, Si wote wawezao kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwa.[#1 Kor 7:7,17]

12Maana wako matowashi waliozaliwa hali hiyo toka matumboni mwa mama zao; tena wako matowashi waliofanywa na watu kuwa matowashi; tena wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea neno hili, na alipokee.

Yesu Awabariki Watoto Wadogo

13Ndipo akaletewa watoto wadogo ili aweke mikono yake juu yao na kuwaombea; wanafunzi wake wakawakemea.[#Mk 10:13-16; Lk 18:15-17]

14Lakini Yesu akasema, Waacheni watoto wadogo waje kwangu; wala msiwazuie; kwa maana walio mfano wa hao, ufalme wa mbinguni ni wao.[#Mt 18:2,3]

15Akaweka mikono yake juu yao, akatoka huko.

Mtu Aliyekuwa Tajiri

16Na tazama, mtu mmoja akamwendea akamwambia, Mwalimu, nitende jambo gani jema, ili nipate uzima wa milele?[#Mk 10:17-31; Lk 18:18-30]

17Akamwambia Kwani kuniuliza habari ya wema? Aliye mwema ni mmoja. Lakini ukitaka kuingia katika uzima, zishike amri.[#Lk 10:26-28]

18Akamwambia, Zipi? Yesu akasema, Ni hizi, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo,[#Kut 20:13-16; Kum 5:17-20]

19Waheshimu baba yako na mama yako, na, Mpende jirani yako kama nafsi yako.[#Kut 20:12; Kum 5:16; Law 19:18]

20Yule kijana akamwambia, Haya yote nimeyashika; nimepungukiwa na nini tena?

21Yesu akamwambia, Ukitaka kuwa mkamilifu, enenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.[#Mt 6:20; Lk 12:33]

22Yule kijana alipolisikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.[#Zab 62:10]

23Yesu akawaambia wanafunzi wake, Amin, nawaambieni, ya kwamba itakuwa shida tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni.

24Nawaambia tena, Ni rahisi zaidi ngamia kupenya tundu ya sindano, kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.

25Wanafunzi waliposikia, walishangaa mno, wakisema, Ni nani basi awezaye kuokoka?

26Yesu akawakazia macho, akawaambia, Kwa wanadamu hilo haliwezekani; bali kwa Mungu yote yawezekana.[#Mwa 18:14; Ayu 42:2; Zek 8:6]

27Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?

28Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli.[#Mt 25:31; Lk 22:30; Dan 7:9,10]

29Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele.[#Ebr 10:34]

30Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.[#Mt 20:16; Lk 13:30]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania