The chat will start when you send the first message.
1Yesu akaenda zake, akatoka hekaluni; wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonyesha majengo ya hekalu.[#Mk 13:1-37; Lk 21:5-36]
2Naye akajibu akawaambia, Hamyaoni haya yote? Amin, nawaambieni, Halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa.[#Lk 19:44]
3Hata alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamwendea kwa faragha, wakisema, Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia?
4Yesu akajibu, akawaambia, Angalieni, mtu asiwadanganye.
5Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi.[#Mt 24:24; Yn 5:43; Mdo 5:36,37; 1 Yoh 2:18]
6Nanyi mtasikia habari za vita na matetesi ya vita; angalieni, msitishwe; maana hayo hayana budi kutukia; lakini ule mwisho bado.[#Dan 2:28]
7Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na njaa, na matetemeko ya nchi mahali mahali.[#Isa 19:2; 2 Nya 15:6]
8Hayo yote ndiyo mwanzo wa utungu.
9Wakati huo watawasaliti ninyi mpate dhiki, nao watawaua; nanyi mtakuwa watu wa kuchukiwa na mataifa yote kwa ajili ya jina langu.[#Mt 10:17,22; Yn 16:2]
10Ndipo wengi watakapojikwaa, nao watasalitiana, na kuchukiana.[#Dan 11:41]
11Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi.[#Mt 7:15; 1 Yoh 4:1]
12Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa.[#2 The 2:10; 2 Tim 3:1-5]
13Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka.[#Mt 10:22; Ufu 13:10]
14Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.[#Mt 28:19; 10:18]
15Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu),[#Dan 9:27; 11:31; 12:11]
16ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani;
17naye aliye juu ya dari asishuke kuvichukua vitu vilivyomo nyumbani mwake;[#Lk 17:31]
18wala aliye shambani asirudi nyuma kuichukua nguo yake.
19Ole wao wenye mimba na wanyonyeshao siku hizo!
20Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato.[#Mdo 1:12]
21Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe.[#Dan 12:1; Ufu 7:14; Yoe 2:2]
22Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo.
23Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki.
24Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule.[#Mt 5:11; Kum 13:1-3; 2 The 2:8,9]
25Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele.
26Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki.[#Lk 17:23-24]
27Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.
28Kwa kuwa po pote ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai.[#Ayu 39:30; Hab 1:8; Lk 17:37]
29Lakini mara, baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka mbinguni, na nguvu za mbinguni zitatikisika;[#Isa 13:10; 34:4; Eze 32:7; Yoe 2:10; 3:4,15; Ufu 6:12-13; 2 Pet 3:10]
30ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi.[#Dan 7:13; Zek 12:10-14; Ufu 1:7; 19:11; Mt 26:64]
31Naye atawatuma malaika zake pamoja na sauti kuu ya parapanda, nao watawakusanya wateule wake toka pepo nne, toka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho huu.[#1 Kor 15:52; 1 The 4:16; Ufu 8:1,2; Isa 27:13; Zek 2:6; Kum 30:4]
32Basi kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno u karibu;
33nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni.
34Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia.
35Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe.[#Mt 5:18]
36Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake.[#1 The 5:1,2]
37Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.[#Mwa 6:5-8; Lk 17:26,27]
38Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina,[#2 Pet 3:5,6; Mwa 7:7]
39wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.[#Mwa 7:6-24]
40Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa;[#Lk 17:35,36]
41wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.
42Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu.[#Mt 25:13]
43Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa.[#Lk 12:39-40]
44Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja.[#Ufu 16:15]
45Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake?
46Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo.
47Amin, nawaambieni, atamweka juu ya vitu vyake vyote.[#Mt 25:21,23]
48Lakini mtumwa yule mbaya akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia;[#Mhu 8:11]
49akaanza kuwapiga wajoli wake, na kula na kunywa pamoja na walevi;
50bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani, na saa asiyojua,
51atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wanafiki; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.[#Mt 8:12]