Mt 25

Mt 25

Mfano wa Wanawali Kumi

1Ndipo ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali kumi, waliotwaa taa zao, wakatoka kwenda kumlaki bwana arusi.[#Lk 12:35; Ufu 19:7]

2Watano wao walikuwa wapumbavu, na watano wenye busara.

3Wale waliokuwa wapumbavu walizitwaa taa zao, wasitwae na mafuta pamoja nao;

4bali wale wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao.

5Hata bwana arusi alipokawia, wote wakasinzia wakalala usingizi.

6Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki.

7Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao.

8Wale wapumbavu wakawaambia wenye busara, Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika.

9Lakini wale wenye busara wakawajibu, wakisema, Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie.

10Na hao walipokuwa wakienda kununua, bwana arusi akaja, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye arusini; mlango ukafungwa.

11Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, Bwana, Bwana, utufungulie.[#Lk 13:25]

12Akajibu akasema, Amin, nawaambia, siwajui ninyi.[#Mt 7:23]

13Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa.[#Mt 24:42]

Mfano wa Talanta

14Maana ni mfano wa mtu atakaye kusafiri, aliwaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake.[#Lk 19:11-27; #Mt 21:33]

15Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri.[#Rum 12:6]

16Mara yule aliyepokea talanta tano akaenda, akafanya biashara nazo, akachuma faida talanta nyingine tano.

17Vile vile na yule mwenye mbili, yeye naye akachuma nyingine mbili faida.

18Lakini yule aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaificha fedha ya bwana wake.

19Baada ya siku nyingi akaja bwana wa watumwa wale, akafanya hesabu nao.

20Akaja yule aliyepokea talanta tano, akaleta talanta nyingine tano, akisema, Bwana, uliweka kwangu talanta tano; tazama, talanta nyingine tano nilizopata faida.

21Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako.[#Mt 25:23; Mt 24:45-47; Lk 16:10]

22Akaja na yule aliyepokea talanta mbili, akasema, Bwana, uliweka kwangu talanta mbili; tazama, talanta nyingine mbili nilizopata faida.

23Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako.[#Mt 25:21]

24Akaja na yule aliyepokea talanta moja, akasema, Bwana, nalitambua ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya;

25basi nikaogopa, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi; tazama, unayo iliyo yako.

26Bwana wake akajibu, akamwambia, Wewe mtumwa mbaya na mlegevu, ulijua ya kuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya;

27basi, ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake.

28Basi, mnyang’anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliye nazo talanta kumi.

29Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa.[#Mt 13:12; Mk 4:25; Lk 8:18]

30Na mtumwa yule asiyefaa, mtupeni mbali katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.[#Mt 8:12; 22:13; Lk 13:28]

Hukumu kwa Mataifa

31Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake;[#Mt 16:27; 19:28; Zek 14:5; Ufu 20:11-13]

32na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi;[#Rum 14:10]

33atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto.[#Eze 34:17]

34Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu;

35kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha;[#Isa 58:7]

36nalikuwa uchi, mkanivika nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia.

37Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha?[#Mt 6:3]

38Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika?

39Ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au kifungoni, tukakujia?

40Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.[#Mit 19:17; Ebr 2:11]

41Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake;[#Mt 7:23; Ufu 20:10,15]

42kwa maana nalikuwa na njaa, msinipe chakula; nalikuwa na kiu, msininyweshe;

43nalikuwa mgeni, msinikaribishe; nalikuwa uchi, msinivike; nalikuwa mgonjwa, na kifungoni, msije kunitazama.

44Ndipo hao pia watajibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona wewe una njaa, au una kiu, au u mgeni, au u uchi, au u mgonjwa, au u kifungoni, tusikuhudumie?

45Naye atawajibu, akisema, Amin, nawaambia, Kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo, hamkunitendea mimi.

46Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele.[#Dan 12:2; Yn 5:29]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania