The chat will start when you send the first message.
1Baada ya siku mbili ilikuwa sikukuu ya Pasaka, na mikate isiyochachwa; wakuu wa makuhani na waandishi wakatafuta njia ya kumkamata kwa hila na kumwua.[#Mt 26:1-5; Lk 22:1-2; #Kut 12:1-27]
2Kwa maana walisema, Isiwe kwa wakati wa sikukuu, isije ikatokea ghasia katika watu.
3Naye alipokuwapo Bethania, nyumbani mwa Simoni mkoma, ameketi chakulani, alikuja mwanamke mwenye kibweta cha marhamu ya nardo safi ya thamani nyingi; akakivunja kibweta akaimimina kichwani pake.[#Mt 26:6-13; Yn 12:1-8; #Lk 7:37-38]
4Palikuwa na watu waliochukizwa katika nafsi zao wakisema, Kwani kupoteza marhamu namna hii?
5Maana marhamu hii ingaliweza kuuzwa kwa dinari mia tatu na kuzidi, wakapewa maskini. Wakamnung’unikia sana yule mwanamke.
6Yesu akasema, Mwacheni; mbona mnamtaabisha? Amenitendea kazi njema;
7maana sikuzote mnao maskini pamoja nanyi, na kila mpendapo mwaweza kuwatendea mema; lakini mimi hamnami sikuzote.[#Kum 15:11]
8Ametenda alivyoweza; ametangulia kuupaka mwili wangu marhamu kwa ajili ya maziko.
9Amin, nawaambia, Kila ihubiriwapo Injili katika ulimwengu wote, na hili alilotenda huyu litatajwa kwa kumbukumbu lake.
10Yuda Iskariote, yule mmoja katika wale Thenashara, akaenda zake kwa wakuu wa makuhani, apate kumsaliti kwao.[#Mt 26:14-16; Lk 22:3-6]
11Nao waliposikia walifurahi, wakaahidi kumpa fedha. Akatafuta njia ya kumsaliti wakati wa kufaa.
12Hata siku ya kwanza ya mikate isiyochachwa, walipoichinja pasaka, wanafunzi wake wakamwambia, Ni wapi utakapo tuende tukuandalie uile pasaka?[#Mt 26:17-19; Lk 22:7-13]
13Akatuma wawili katika wanafunzi wake, akawaambia, Nendeni zenu mjini; atakutana nanyi mwanamume amechukua mtungi wa maji; mfuateni;
14na po pote atakapoingia, mwambieni mwenye nyumba, Mwalimu asema, Ki wapi chumba changu cha wageni, niile pasaka humo, pamoja na wanafunzi wangu?[#Mk 11:3]
15Naye mwenyewe atawaonyesha orofa kubwa, imeandikwa tayari; humo tuandalieni.
16Wanafunzi wakatoka, wakaenda mjini, wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa pasaka.
17Basi ilipokuwa jioni yuaja pamoja na wale Thenashara.[#Mt 26:20-29; Lk 22:14-23; Yn 13:21-26]
18Nao walipokuwa wameketi chakulani, wakila, Yesu alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu, naye anakula pamoja nami, atanisaliti.[#Zab 41:9]
19Wakaanza kuhuzunika, wakamwambia mmoja mmoja, Je! Ni mimi?
20Akawaambia, Ni mmoja wa hao Thenashara, ambaye achovya pamoja nami katika kombe.
21Kwa maana Mwana wa Adamu aenda zake kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu; ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa.
22Nao walipokuwa wakila, alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa, akasema, Twaeni; huu ndio mwili wangu.[#1 Kor 11:23-25]
23Akatwaa kikombe, akashukuru, akawapa; wakakinywea wote.
24Akawaambia, Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi.[#Kut 24:8; Yer 31:31-34; Zek 9:11]
25Amin, nawaambia ninyi, Sitakunywa tena kabisa uzao wa mzabibu, hata siku ile nitakapounywa mpya katika ufalme wa Mungu.
26Nao walipokwisha kuimba walitoka kwenda mlima wa Mizeituni.[#Mt 26:30-35; Lk 22:31-34,39; #Zab 113—118]
27Yesu akawaambia, Mtakunguwazwa ninyi nyote kwa ajili yangu usiku huu; kwa kuwa imeandikwa,[#Zek 13:7]
Nitampiga mchungaji, na kondoo watatawanyika.
28Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya.[#Mt 28:16; Mk 16:7]
29Petro akamwambia, Hata wajapokunguwazwa wote, lakini siyo mimi.
30Yesu akamwambia, Amin, nakuambia wewe, Leo, usiku huu, kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu.[#Yn 13:38]
31Naye akazidi sana kusema, Ijaponipasa kufa nawe, hata hivyo sitakukana kamwe. Na wote wakasema vile vile.[#Yn 11:16]
32Kisha wakaja mpaka bustani iitwayo Gethsemane; akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa muda niombapo.[#Mt 26:36-46; Lk 22:40-46; #Yn 18:1]
33Akamtwaa Petro na Yakobo na Yohana pamoja naye, akaanza kufadhaika sana na kuhangaika.
34Akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa mkeshe.[#Yn 12:27; Zab 43:5]
35Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akiomba ya kuwa, ikiwezekana, saa hiyo imwepuke.
36Akasema, Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; walakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe.[#Mk 10:38]
37Akaja akawakuta wamelala usingizi, akamwambia Petro, Je! Simoni, umelala? Hukuweza kukesha saa moja?
38Kesheni mwombe, msije mkaingia majaribuni, roho i radhi ila mwili ni dhaifu.
39Akaenda zake tena, akaomba, akisema neno lilo hilo.
40Akaja tena akawakuta wamelala, maana macho yao yamekuwa mazito, wala hawakujua la kumjibu.
41Akaja mara ya tatu, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike; yatosha, saa imekuja; tazama, Mwana wa Adamu anatiwa mikononi mwao wenye dhambi.
42Ondokeni, twendeni zetu; tazama, yule anayenisaliti amekaribia.[#Yn 14:31]
43Basi alipokuwa katika kusema, mara Yuda alifika, mmoja wa wale Thenashara, na pamoja naye mkutano, wana panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani, na waandishi, na wazee.[#Mt 26:47-58; Lk 22:47-55; Yn 18:2-18]
44Na yule anayemsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni, mkamchukue salama.
45Basi alipokuja, mara akamwendea, akasema, Rabi, akambusu.
46Wakanyosha mikono yao wakamkamata.
47Na mmoja wao waliokuwapo akafuta upanga, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio.
48Yesu akajibu, akawaambia, Je! Ni kama juu ya mnyang’anyi mmetoka wenye panga na marungu, kunitwaa mimi?
49Kila siku nalikuwa mbele yenu hekaluni nikifundisha, msinikamate; lakini haya yamekuwa ili maandiko yapate kutimia.[#Lk 19:47; 21:37]
50Ndipo wakamwacha, wakakimbia wote.
51Na kijana mmoja alimfuata, amejitanda mwili wake nguo ya kitani; wakamkamata;
52naye akaiacha ile nguo ya kitani, akakimbia yu uchi.
53Nao wakamchukua Yesu kwa Kuhani Mkuu; wakamkusanyikia wote, wakuu wa makuhani na wazee na waandishi.
54Naye Petro akamfuata kwa mbali, hata ndani katika behewa ya Kuhani Mkuu; akawa ameketi pamoja na watumishi, anakota moto mwangani.
55Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda juu ya Yesu wapate kumwua; wasione.[#Mt 26:59-68; Lk 22:63-71; Yn 18:19-24]
56Kwa maana wengi walimshuhudia uongo, walakini ushuhuda wao haukupatana.
57Hata wengine wakasimama, wakamshuhudia uongo, wakisema,
58Sisi tulimsikia akisema, Mimi nitalivunja hekalu hili lililofanyika kwa mikono, na katika siku tatu nitajenga jingine lisilofanyika kwa mikono.[#Yn 2:19; 4:21,23]
59Wala hata hivi ushuhuda wao haukupatana.
60Kisha Kuhani Mkuu akasimama katikati, akamwuliza Yesu, akisema, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini?
61Lakini akanyamaza, wala hakujibu neno. Kuhani Mkuu akamwuliza tena, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wake Mtukufu?[#Mk 15:5; Isa 53:7]
62Yesu akasema, Mimi ndiye, nanyi mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija na mawingu ya mbinguni.[#Dan 7:13; Zab 110:1]
63Kuhani Mkuu akararua nguo zake, akisema, Tuna haja gani tena ya mashahidi?
64Mmesikia kufuru yake; mwaonaje ninyi? Wote wakamhukumu kuwa imempasa kuuawa.[#Law 24:16; Yn 19:7]
65Wengine wakaanza kumtemea mate, wakamfunika uso, na kumpiga makonde, na kumwambia, tabiri. Hata watumishi nao wakampiga makofi.
66Na Petro alikuwa chini behewani; akaja mmoja wa vijakazi wa Kuhani Mkuu,[#Mt 26:69-75; Lk 22:56-62; Yn 18:25-27]
67akamwona Petro akikota moto; akamkazia macho, akasema, Wewe nawe ulikuwapo pamoja na yule Mnazareti, Yesu.
68Akakana, akasema, Sijui wala sisikii unayoyasema wewe. Akatoka nje hata ukumbini; jogoo akawika.
69Na yule kijakazi akamwona tena, akaanza tena kuwaambia waliosimama pale, Huyu ni mmoja wao.
70Akakana tena. Kitambo kidogo tena wale waliosimama pale wakamwambia Petro, Hakika u mmoja wao, kwa sababu u Mgalilaya wewe.
71Akaanza kulaani na kuapiza, Simjui mtu huyu mnayemnena.
72Na mara jogoo akawika mara ya pili. Petro akalikumbuka lile neno aliloambiwa na Yesu, Kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu. Na alipolifikiri, akalia. a.[#Mk 14:30]