The chat will start when you send the first message.
1Akatoka huko, akafika mpaka nchi ya kwao; wanafunzi wake wakamfuata.[#Mt 13:53-58; Lk 4:15-30]
2Na ilipokuwa sabato, alianza kufundisha katika sinagogi; wengi waliposikia wakashangaa, wakisema, Huyu ameyapata wapi haya? Na, Ni hekima gani hii aliyopewa huyu? Na, Ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake?[#Yn 7:15]
3Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? Na maumbu yake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake.
4Yesu akawaambia, Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake.[#Yn 4:44]
5Wala hakuweza kufanya mwujiza wo wote huko, isipokuwa aliweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache, akawaponya.[#Mk 6:13]
6Akastaajabu kwa sababu ya kutokuamini kwao. Akazunguka-zunguka katika vile vijiji, akifundisha.
7Akawaita wale Thenashara, akaanza kuwatuma wawili wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu;[#Mt 10:1,9-15; Lk 9:1-6; #Lk 10:1]
8akawakataza wasichukue kitu cha njiani isipokuwa fimbo tu; wala mkate, wala mkoba, wala pesa za bindoni;[#Lk 10:4-11]
9lakini wajifungie viatu; akasema, Msivae kanzu mbili.
10Akawaambia, Mahali po pote mtakapoingia katika nyumba, kaeni humo hata mtakapotoka mahali pale.
11Na mahali po pote wasipowakaribisha ninyi wala kuwasikia, mtokapo huko, yakung’uteni mavumbi yaliyo chini ya miguu yenu, kuwa ushuhuda kwao.[#Mdo 13:51]
12Wakatoka, wakahubiri kwamba watu watubu.
13Wakatoa pepo wengi, wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza.[#Yak 5:14,15]
14Naye Mfalme Herode akasikia habari; kwa maana jina lake lilikuwa kutangaa, akasema, Yohana Mbatizaji amefufuka katika wafu, na kwa hiyo nguvu hizi zinatenda kazi ndani yake.[#Mt 16:14; Mk 8:28; Lk 9:19; #Lk 3:19,20]
15Wengine walisema, Ni Eliya. Wengine walisema, Huyu ni nabii, au ni kama mmoja wa manabii.
16Lakini Herode aliposikia, alisema, Yohana, niliyemkata kichwa, amefufuka.
17Kwa maana Herode mwenyewe alikuwa ametuma watu, akamkamata Yohana, akamfunga gerezani, kwa ajili ya Herodia, mkewe Filipo ndugu yake, kwa kuwa amemwoa;[#Lk 3:19-20]
18kwa sababu Yohana alimwambia Herode, Si halali kwako kuwa na mke wa nduguyo.[#Law 18:16]
19Naye yule Herodia akawa akimvizia, akataka kumwua, asipate.
20Maana Herode alimwogopa Yohana; akimjua kuwa ni mtu wa haki, mtakatifu, akamlinda; na alipokwisha kumsikiliza alifadhaika sana; naye alikuwa akimsikiliza kwa furaha.
21Hata ilipotokea siku ya kufaa, na Herode, sikukuu ya kuzaliwa kwake, alipowafanyia karamu wakubwa wake, na majemadari, na watu wenye cheo wa Galilaya;
22ndipo binti yake yule Herodia alipoingia, akacheza, akampendeza Herode na wale walioketi pamoja naye karamuni. Mfalme akamwambia yule kijana, Niombe lo lote utakalo, nitakupa.
23Akamwapia, Lo lote utakaloniomba nitakupa, hata nusu ya ufalme wangu.[#Est 5:3-6]
24Basi akatoka, akamwuliza mamaye, Niombe nini? Naye akasema, Kichwa cha Yohana Mbatizaji.
25Mara akaingia kwa haraka mbele ya mfalme, akaomba akisema, Nataka unipe sasa hivi katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji.
26Mfalme akafanya huzuni sana, lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya hao walioketi karamuni, hakutaka kumkatalia.
27Mara mfalme akatuma askari, akaamuru kuleta kichwa chake. Basi akaenda, akamkata kichwa mle gerezani,
28akakileta kichwa chake katika kombe, akampa yule kijana, naye yule kijana akampa mamaye.
29Wanafunzi wake waliposikia habari, walikwenda, wakauchukua mwili wake, wakauzika kaburini.
30Na mitume wakakusanyika mbele ya Yesu; wakampa habari za mambo yote waliyoyafanya, na mambo yote waliyoyafundisha.[#Lk 9:10; 10:17]
31Akawaambia, Njoni ninyi peke yenu kwa faragha, mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike kidogo. Kwa sababu walikuwako watu wengi, wakija, wakienda, hata haikuwapo nafasi ya kula.
32Wakaenda zao faragha mashuani, mahali pasipokuwa na watu.[#Mt 14:13-21; Lk 9:11-17; Yn 6:1-13]
33Watu wakawaona wakienda zao, na wengi wakatambua, wakaenda huko mbio kwa miguu, toka miji yote, wakatangulia kufika.
34Naye aliposhuka mashuani, akaona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi.[#Hes 27:17; 1 Fal 22:17; 2 Nya 18:16; Eze 34:5; Mt 9:36]
35Hata zilipopita saa nyingi za mchana, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, Mahali hapa ni nyika tupu, na sasa kunakuchwa;[#Mk 8:1-9]
36uwaage watu hawa, ili waende zao mashambani na vijijini kandokando, wakajinunulie chakula.
37Akajibu, akawaambia, Wapeni ninyi chakula. Wakamwambia, Je! Twende tukanunue mikate ya dinari mia mbili ili tuwape kula?
38Akawaambia, Mnayo mikate mingapi? Nendeni mkatazame. Walipokwisha kujua wakasema, Mitano, na samaki wawili.
39Akawaagiza wawaketishe wote, vikao vikao, penye majani mabichi.
40Wakaketi safu safu, hapa mia hapa hamsini.
41Akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama mbinguni, akashukuru, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi wake wawaandikie; na wale samaki wawili akawagawia wote.[#Mk 7:34]
42Wakala wote wakashiba.
43Wakaokota vipande vilivyomegwa vya kuweza kujaza vikapu kumi na viwili; na vipande vya samaki pia.[#Kum 28:5]
44Na walioila ile mikate wapata elfu tano wanaume.
45Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande mashuani, watangulie kwenda ng’ambo hata Bethsaida, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano.[#Mt 14:22-36; Yn 6:15-21]
46Hata alipokwisha kuagana nao akaenda zake mlimani kuomba.
47Na kulipokuwa jioni mashua ilikuwa katikati ya bahari, na yeye yu peke yake katika nchi kavu.
48Akawaona wakitaabika kwa kuvuta makasia, kwa maana upepo ulikuwa wa mbisho; hata ilipopata kama zamu ya nne ya usiku akawaendea, akitembea juu ya bahari; akataka kuwapita.
49Nao walipomwona anatembea juu ya bahari, walidhani ya kuwa ni kivuli, wakapiga yowe,
50kwa kuwa wote walimwona, wakafadhaika. Mara akasema nao, akawaambia, Changamkeni; ni mimi, msiogope.
51Akapanda mle chomboni walimo; upepo ukakoma; wakashangaa sana mioyoni mwao;[#Mk 4:39]
52kwa maana hawakufahamu habari za ile mikate, lakini mioyo yao ilikuwa mizito.
53Hata walipokwisha kuvuka, walifika nchi ya Genesareti, wakatia nanga.
54Nao wakiisha kutoka mashuani, mara watu walimtambua,
55wakaenda mbio, wakizunguka nchi ile yote, wakaanza kuwachukua vitandani walio hawawezi, kwenda kila mahali waliposikia kwamba yupo.
56Na kila alikokwenda, akiingia vijijini, au mijini, au mashambani, wakawaweka wagonjwa sokoni, wakamsihi waguse ngaa pindo la vazi lake; nao wote waliomgusa wakapon[#Mk 5:27,28; Mdo 5:15; 19:11,12]