The chat will start when you send the first message.
1Ee BWANA, mfalme atazifurahia nguvu zako,
Na wokovu wako ataufanyia shangwe nyingi sana.
2Umempa haja ya moyo wake,[#Yn 11:42]
Wala hukumzuilia matakwa ya midomo yake.
3Maana umemsogezea baraka za heri,
Umemvika taji ya dhahabu safi kichwani pake.
4Alikuomba uhai, ukampa,[#2 Sam 7:19]
Muda mrefu wa siku nyingi, milele na milele.
5Utukufu wake ni mkuu kwa wokovu wako,
Heshima na adhama waweka juu yake.
6Maana umemfanya kuwa baraka za milele,
Wamfurahisha kwa furaha ya uso wako.
7Kwa kuwa mfalme humtumaini BWANA,[#Zab 91:2]
Na kwa fadhili zake Aliye juu hataondoshwa.
8Mkono wako utawapata adui zako wote,
Mkono wako wa kuume utawapata wanaokuchukia.
9Utawafanya kuwa kama tanuru ya moto,[#Kum 32:22]
Wakati wa ghadhabu yako.
BWANA atawameza kwa ghadhabu yake,
Na moto utawala.
10Matunda yao utayaharibu na kuyaondoa katika nchi,
Na wazao wao katika wanadamu.
11Madhali walinuia kukutenda mabaya,
Waliwaza hila wasipate kuitimiza.
12Kwa maana utawafanya kukupa kisogo,
Kwa upote wa uta wako ukiwaelekezea mishale.
13Ee BWANA, utukuzwe kwa nguvu zako,[#Ufu 15:3,4]
Nasi tutaimba na kuuhimidi uweza wako.