Zab 31

Zab 31

Sala na Sifa kwa Kukombolewa kutoka kwa Adui

1Nimekukimbilia Wewe, BWANA,

Nisiaibike milele.

Kwa haki yako uniponye,

2Unitegee sikio lako, uniokoe hima.[#Zab 71:2; Mit 22:17]

Uwe kwangu mwamba wa nguvu,

Nyumba yenye maboma ya kuniokoa.

3Ndiwe genge langu na ngome yangu;[#Zab 23:3; Yer 14:7]

Kwa ajili ya jina lako uniongoze, unichunge.

4Utanitoa katika wavu walionitegea kwa siri,

Maana Wewe ndiwe ngome yangu.

5Mikononi mwako naiweka roho yangu;[#Lk 23:46; Mdo 7:59; 2 Tim 1:12; Ebr 6:18]

Umenikomboa, Ee BWANA, Mungu wa kweli.

6Nawachukia wao washikao yasiyofaa yenye uongo;

Bali mimi namtumaini BWANA.

7Na nishangilie, nizifurahie fadhili zako,[#Yn 10:27]

Kwa kuwa umeyaona mateso yangu.

Umeijua nafsi yangu taabuni,

8Wala hukunitia mikononi mwa adui;[#Zab 18:19]

Miguu yangu umeisimamisha panapo nafasi.

9Ee BWANA, unifadhili, maana ni katika dhiki,

Jicho langu limenyauka kwa masumbufu,

Naam, mwili wangu na nafsi yangu.

10Maana maisha yangu yamekoma kwa huzuni,

Na miaka yangu kwa kuugua.

Nguvu zangu zinatetemeka kwa uovu wangu,

Na mifupa yangu imekauka.

11Kwa sababu ya watesi wangu nimekuwa laumu,[#Zab 88:8]

Naam, hasa kwa jirani zangu;

Na kitu cha kutisha kwa rafiki zangu;

Walioniona njiani walinikimbia.

12Nimesahauliwa kama mfu asiyekumbukwa;

Nimekuwa kama chombo kilichovunjika.

13Maana nimesikia masingizio ya wengi;[#Yer 20:3; Omb 2:22; Mt 27:1]

Hofu ziko pande zote.

Waliposhauriana juu yangu,

Walifanya hila wauondoe uhai wangu.

14Lakini mimi nakutumaini Wewe, BWANA,

Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.

15Nyakati zangu zimo mikononi mwako;

Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia.

16Umwangaze mtumishi wako[#Hes 6:25; Zab 4:6; Dan 9:17]

Kwa nuru ya uso wako;

Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako.

17Ee BWANA, nisiaibishwe, maana nimekuita;[#Zab 25:2]

Waaibishwe wasio haki, wanyamaze kuzimuni.

18Midomo ya uongo iwe na ububu,[#Zab 12:3]

Imneneayo mwenye haki maneno ya kiburi,

Kwa majivuno na dharau.

19Jinsi zilivyo nyingi fadhili zako[#Isa 64:4; 1 Kor 2:9]

Ulizowawekea wakuchao;

Ulizowatendea wakukimbiliao

Mbele ya wanadamu!

20Utawasitiri na fitina za watu[#Zab 27:5; Ayu 5:21]

Katika sitara ya kuwapo kwako;

Utawaficha katika hema

Na mashindano ya ndimi.

21BWANA ahimidiwe; kwa maana amenitendea

Fadhili za ajabu katika mji wenye boma.

22Nami nalisema kwa haraka yangu,

Nimekatiliwa mbali na macho yako;

Lakini ulisikia sauti ya dua yangu

Wakati nilipokulilia.

23Mpendeni BWANA,[#1 Pet 1:5]

Ninyi nyote mlio watauwa wake.

BWANA huwahifadhi waaminifu,

Humlipa atendaye kiburi malipo tele.

24Iweni hodari, mpige moyo konde,

Ninyi nyote mnaomngoja BWANA.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania