2 Wakorintho 8

2 Wakorintho 8

1TENA twawaarifu ninyi, ndugu, kliahari ya neema ya Mungu, waliyopewa makanisa ya Makedonia;

2maana walipokuwa wakijaribiwa kwa shidda nyingi, wingi wa furaha yao na umaskini wao uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa unyofu wao.

3Maana nawashuhudia, kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao,

4kwa khiari yao wenyewe walitoa vitu vyao; wakituomba pamoja na kutusihi tuipokee neema hii, na kushirikiana nao huku kuwakhudumia watakatifu.

5Tena walitenda hivi si kama tulivyotumaini, bali kwanza walijitoa nafsi zao, wakampa Bwana; kiisha wakatupa sisi pia, kwa mapenzi ya Mungu,

6hatta tukamwonya Tito kuwatimilizieni neema hii kama vile alivyoianza.

7Lakini kama mlivyo na wingi wa vitu vyote, imani, na matamko, na elimu, na bidii yote, na mapenzi yenu kwetu sisi; bassi vivyo hivyo mwe na wingi wa neema hii pia.

8Sineni illi kuwaamuru, bali kwa bidii ya watu wengine nijaribu unyofu wa upendo wenu.

9Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yetu, alipokuwa tajiri, illi ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.

10Nami katika neno hili natoa shauri langu; maana neno hili lawafaa ninyi mliotangulia, wapata mwaka, licha ya kutenda hivi, hatta kutaka pia.

11Lakini sasa mkatimize kule kutenda nako, illi kama vile mlivyokuwa tayari kutaka, vivyo hivyo mwe tayari na kutimiza, kwa kadiri ya mlivyo navyo.

12Maana, kama nia ipo, hukubaliwa kwa kadiri ya alivyo navyo mtu, si kwa kadiri ya asivyo navyo.

13Maana sisemi haya, illi wengine waachiliwe ninyi mkalemewe,

14bali mambo yawe sawa sawa: wakati huu wa sasa wingi wenu uwafae upungufu wao, illi na wingi wao uwafae ninyi upungufu wenu; illi mambo yawe sawa sawa.

15Kama ilivyoandikwa, Aliyekusanya vingi, hakuzidi, nae aliyekusanya vichache hakupungukiwa.

16Lakini Mungu ashukuriwe atiae bidii ile ile kwa ajili yenu katika moyo wa Tito.

17Maana alipokea yale maonyo; nae, akizidi kuwa na bidii, alisafiri kwenda kwenu kwa khiari yake mwenyewe.

18Na pamoja nae tukamtuma ndugu yule ambae sifa zake katika Injili zimeenea makanisani mwote.

19Wala si hivyo tu, bali alichaguliwa na makanisa asafiri pamoja nias katika jambo la neema hii inayokhudumiwa nasi, illi Bwana atukuzwe, ikadhihirike ya kuwa mioyo yenu ilikuwa tayari.

20Tukijiepusha na neno hili, mtu asije akatulaumu katika khabari ya karama hii inayokhudumiwa nasi;

21tukitangulia kufikiri yaliyo mema, si mbele ya Bwana tu, bali na mbele ya wana Adamu.

22Nasi pamoja nae tumemtuma ndugu yetu tuliyemwona katika mambo mengi kuwa ana bidii, na sasa ana bidii zaidi sana kwa sababu ya tumaini alilo nalo kwenu.

23Bassi mtu akitaka khabari za Tito, yeye ni mshirika wangu, na mtenda kazi pamoja nami; tena akitaka khabari za ndugu zetu, wao ni mitume ya makanisa, na utukufu wa Kristo.

24Bassi waonyesheni mbele ya makanisa bayana ya upendo wenu, na ya kujisifu kwetu kwa ajili yenu.

Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Published by: Bible Society of Tanzania