Matendo 24

Matendo 24

1BAADA ya siku tano, Anania, kuhani mkuu, akatelemka na baadhi ya wazee pamoja nae, na msemi mmoja, Tertullo nao wakamweleza liwali khabari za Paolo.

2Na alipoitwa Tertullo akaanza kumshitaki, akisema,

3Kwa kuwa tunapata amani nyingi chini yako, ee Feliki il aziz, na kwa maangalizo yako mambo mabaya yanatengenezwa kwa ajili ya taifa hili, bassi tunayapokea killa wakati na killa mahali, kwa shukrani yote.

4Lakini nisikuudhi zaidi, nakusihi utusikilize maneno machache kwa fadhili zako.

5Kwa maana tamemwona mtu huyu mkorofi, muanzishaji wa fitina katika Mayahudi waliomo duniani, tena ni kichwa cha uzushi wa Wanazorayo.

6Na tena alijaribu kuitia hekalu najis: tukamkamata: tukataka kumhukumu kwa sharia yetu.

7Lakini Lusia jemadari akafika, akampokonya mikononi mwetu kwa nguvu, akawaamuru wale waliomshitaki waje kwako.

8Wewe mwenyewe utaweza kumwuliza na kupata khabari ya mambo yale tunayomshitaki sisi.

9Wayahudi nao wakamshitaki, wakisema ya kuwa ndivyo yalivyo.

10Na liwali alipompungia mkono illi anene, Paolo akajibu, Kwa kuwa ninajua kama wewe umekuwa mwamuzi wa taifa hili kwa muda wa miaka mingi, najitetea nafsi yangu kwa moyo wa furaha.

11Maana waweza kujua ya kuwa hazijapita siku zaidi ya thenashara tangu nilipopanda kwenda Yerusalemi illi kuabudu.

12Watu hawa hawakuniona ndani ya hekalu, nikihujiana na mtu, wala nikifanya fujo katika mkutano, wala katika masunagogi wala ndani ya mji.

13Wala hawawezi kuyathubutisha mambo haya wanayonishitaki sasa.

14Illa neno hili naliungama kwako ya kwamba kwa Njia ile ambayo waiita uzushi, ndivyo ninavyomwabudu Mungu wa baba zetu, nikiyaamini yote yanayopatana na torati na yaliyoandikwa katika vyuo vya manabii.

15Nina tumaini kwa Mungu, na hatta hao nao wanalitazamia, ya kwamba kutakuwa ufufuo wa wafu wenye haki na wasio haki pia.

16Nami ninajizoeza katika neno hili kuwa na dhamiri isiyo na khatiya mbele ya Mungu na mbele ya watu.

17Baada ya miaka mingi nalifika niwaletee watu wa taifa langu sadaka na matoleo.

18Baadhi ya Wayahudi waliotoka Asia wakaniona ndani ya hekalu nikishughulika na mambo haya, nimetakaswa, wala sikuwa pamoja na mkutano wala ghasia.

19Imewapasa hao kuwapo hapa mbele yako na kunishitaki kama wana neno lo lote juu yangu.

20Au watu hawa wenyewe na waseme, ni kosa gani waliloliona kwangu niliposimama mbele ya baraza,

21isipokuwa kwa ajili ya sauti hii moja, nilipolia nikisimama katikati yao, Kwa ajili ya ufufuo wa wafu ninahukumiwa mbele yenu hivi leo.

22Bassi Feliki, alijiokwisha kusikia haya, aliwaakhirisha, kwa sababu alijua khabari za Njia ile kwa usahihi zaidi, akasema, Lusia jemadari, atakapotelemka nitakata maneno yenu.

23Akamwamuru yule akida amlinde Paolo; illa awe na nafasi, wala asimkataze mmojawapo wa rafiki zake kumkhudumu au kuja kumtazama.

24Baada ya siku kadha wa kadha, Feliki akafika pamoja na Drusilla mkewe aliyekuwa Myahudi, akamwita Paolo akamsikiliza khabari za imani ya Kristo.

25Na Paolo alipokuwa akitoa hoja zake katika khabari ya haki na kiasi na hukumu itakayokuja, Feliki akafanya khofu akajihu, Sasa enenda zako, nami nikipata wasaa nitakuita tena.

26Tena alitaraja kwamba atapewa fedha na Paolo illi amfungue: kwa hiyo alimwita marra nyingi akaongea nae.

27Na miaka miwili ilipotimia. Feliki akampokea Porkio Festo atawale badala yake. Na Feliki, akitaka kuwafanyia Wayahudi fadhili, akamwacha Paolo amefungwa.

Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Published by: Bible Society of Tanzania