1 Wakorintho 9

1 Wakorintho 9

Haki Ambazo Paulo Hajazitumia

1Mnajua kuwa mimi ni mtu niliye huru. Mnajua kuwa mimi ni mtume na kwamba nilimwona Yesu Bwana wetu. Na ninyi ni kielelezo cha kazi yangu katika Bwana.

2Wengine wanaweza wasikubali kuwa mimi ni mtume, lakini hakika ninyi mnakubali. Ninyi ni uthibitisho kuwa mimi ni mtume wa Bwana.

3Ninataka kuwajibu baadhi ya watu wanaotaka kunichunguza.

4Je! hatuna haki ya kula na kunywa?

5Je! hatuna haki ya kusafiri pamoja na mke aliye mwamini? Mitume wengine wote, wadogo zake Bwana na Petro hufanya hivi.

6Na je, ni mimi na Barnaba tu ndiyo ambao ni lazima tufanya kazi ili tupate kipato cha kutuwezesha kuishi?

7Ni askari gani aendaye vitani kwa gharama zake mwenyewe? Ni nani apandaye mizabibu asiyekula katika matunda yake? Au ni nani achungaye kundi la kondoo na hanywi maziwa?

8Lakini nina mifano mingi kutoka katika maisha ya kila siku inayosisitiza hoja yangu. Sheria ya Mungu inasema vivyo hivyo pia.

9Ndiyo, imeandikwa katika Sheria ya Musa kuwa; “Mnyama wa kazi anapotumika kupura nafaka, usimzuie kula nafaka.” Je! Mungu aliposema hivi, alikuwa anawawazia wanyama pekee? Hapana.[#Kum 25:4]

10Hakika Mungu alizungumza kuhusu sisi. Ndiyo, iliandikwa kwa ajili yetu. Wote wawili, anayelima na anayepura nafaka, wana haki ya kupata nafaka kutokana na kazi yao.

11Ikiwa tulipanda mbegu ya kiroho mioyoni mwenu, je, hatustahili kupata vitu kwa ajili ya maisha haya kutoka kwenu?

12Ikiwa wengine wana haki ya kupata vitu kutoka kwenu, hakika hata sisi tuna haki pia. Lakini hatuitumii haki hii. Tunavumilia katika hali zote ili tusimfanye mtu yeyote akaacha kuitii Habari Njema ya Kristo.

13Hakika mnajua ya kuwa wanaotumika Hekaluni hula chakula kutoka Hekaluni. Na wale wanaotumika madhabahuni hupata sehemu ya yale yanayotolewa madhabahuni.

14Vivyo hivyo kwa wale wenye kazi ya kuhubiri Injili. Bwana ameamuru kuwa nao wataishi kutokana na kazi hiyo.

15Lakini sijatumia haki hizi, na si kwamba ninataka kitu chochote kutoka kwenu. Ijapokuwa ninaandika hivi hilo si lengo langu. Ni bora nife kuliko mtu yeyote kuchukua kutoka kwangu kitu ninachojivunia.

16Sijivuni kwa sababu ya kazi yangu ya kuhubiri Habari Njema kwa sababu ni wajibu wangu ambao ni lazima nifanye; ole wangu nisipowahubiri watu Habari Njema.

17Ikiwa ningehubiri kwa sababu ya utashi kwangu, ningestahili kulipwa. Lakini sikuchagua kufanya kazi hii. Ni lazima nihubiri Habari Njema. Hivyo ninafanya kazi niliyokabidhiwa.

18Sasa, kwa kufanya kazi hii ninapata nini? Thawabu yangu, ni kuwa ninapowahubiri watu Habari Njema, ninawapa bure na sizitumii haki zinazoambatana na kufanya kazi hii.

19Niko huru. Similikiwi na mtu yeyote, lakini ninakuwa mtumwa ili watu wengi waokoke.

20Kwa Wayahudi nilienenda kama Myahudi ili nisaidie Wayahudi wengi waokolewe. Sitawaliwi na sheria, lakini kwa wanaotawaliwa na sheria nilikuwa kama ninayetawaliwa na sheria. Nilifanya hivi kuwasaidia wanaotawaliwa na sheria, ili waokoke.

21Kwa wasio na sheria nilikuwa kama nisiye na sheria, ili niwasaidie wasio na sheria kuokoka. Mimi si kama mtu asiye na Sheria ya Mungu, ninatawaliwa na sheria ya Kristo.

22Kwa waliodhaifu, nilikuwa dhaifu ili niwasaidie kuokoka. Nilifanyika kila kitu kwa watu wote ili nifanye kila kinachowezekana niweze kuwasaidia watu waokolewe.

23Ninafanya kila ninachoweza ili Habari Njema ijulikane na niweze kushiriki katika Habari zake.

24Mnajua kuwa katika riadha, wanariadha wengi hukimbia, lakini mmoja tu hupata zawadi. Hivyo kimbieni hivyo. Kimbieni ili mshinde!

25Wote wanaoshiriki katika mchezo hufanya mazoezi kwa bidii ili waweze kushinda na kupata zawadi. Lakini zawadi wanazopata hazidumu milele. Lakini zawadi yetu ni ile inayodumu milele.

26Hivyo ninakimbia kama mtu mwenye malengo. Ninapigana ngumi kama mpiganaji anayepiga kitu, si kama anayepiga hewa.

27Ninaudhibiti mwili wangu kikamilifu na kuufanya unitiii kwa kila jambo ninalotaka kutenda. Ninafanya hivi ili mimi binafsi nisiikose thawabu baada ya kuwahubiri wengine Habari Njema.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International